Friday, July 10, 2009

IJUMAA SHOWBIZ!

TUNDA & SPARK WAUNGANA NA TMK FAMILY
Ishu mpya iliyotua ndani ya ShowBiz kutoka pande za Temeke na Manzese, Dar es Salaam inasema kwamba, makundi mawili yaliyopo kunako game ya muziki wa kizazi kipya, TMK Wanaume Family na Tip Top Connection yameungana na kuamua kupiga kazi pamoja huku wasanii Tundaman, Spark, Madee, Z-Anto, Kassim, Chegge, Temba, KR, Stiko na wengine wakionesha kufurahia ‘idea’ hiyo.

Baada ya kusikia uvumi huo, safu ilimtafuta kiongozi wa TMK, Said Fella ambaye alisema: “Yeah, ni kweli tumeungana na kuamua kupiga kazi pamoja kwa sababu tunaamini siku zote umoja ni nguvu, ukizingatia kwamba tangu zamani mimi na Abdul Bonge wa Tip Top ni kama mtu na mdogo wake.

“Tulichofanya baada ya kuungana ni kurekodi ngoma ya pamoja yenye jina la ‘Chama Kubwa’ ambayo inatambulisha muungano huo na siku chache zijazo tutaanza ziara katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kuutambulisha umoja wetu. Hatujaishia kwenye kazi hiyo tu, hivi sasa tupo kwenye hatua za mwisho kukamilisha albamu ya pamoja.”

Kwa upande wa uongozi wa Tip Top, safu hii ilipiga stori na Babu Tale ambaye alisema: “Sisi tumeupokea muungano huo kwa mikono miwili kwa kuwa tunaamini nguvu yake itakuwa kubwa, ili kukuhakikishia hilo ntakuletea kazi ya pamoja ‘Chama Kubwa’ ili usikie vijana walivyofanya kazi. Tunatarajia kuanza ziara ya pamoja Julai 24, mwaka huu Sumbawanga, Rukwa, baadaye Mbeya na Iringa itafuata.”
***********
USHER RAYMOND: KILICHOMLIZA MBELE YA JENEZA LA MICHAELJACKSON
Miongoni mwa mastaa wa Marekani waliotokwa na machozi wakati wa zoezo la kumuaga mfalme wa Pop, Michael Jackson ni pamoja na Usher Raymond ambaye kuna wakati alishindwa kuendelea kuimba kabla hajakumbatiwa na ndugu wa Michael ambao walimfariji.

Baada ya tukio hilo, ShowBiz ilifanya uchunguzi na kugundua kwamba ukaribu aliokuwa nao Usher kwa Michael ni mkubwa zaidi na kwamba hata staili ya kucheza anayotumia stejini aliikopi kwa nyota huyo ambaye alizimika ghafla wiki mbili zilizopita.

Kwa mujibu wa mtandao, Usher alikuwa akipata ushauri wa kutosha kuhusu muziki kutoka kwa Michael na hata katika baadhi ya shoo za mkali huyo wa Pop, mchizi alipanda stejini na kupiga kazi ambazo zilimfanya marehemu amkumbatie na kumpongeza huku akimpa moyo kwamba, baadae atakuwa mkali wa dunia katika kucheza.

Inawezekana hayo na mengine mengi ndiyo vitu vilivyomfanya Usher aibuke mafichoni alipokuwa amejichimbia na kuungana na umati wa watu na mastaa mbalimbali katika zoezi la kumuaga Michael Jackson lililofanyika katikati ya wiki hii, Los Angeles, Marekani, kabla hajapanda jukwaani na kumwaga machozi wakati akiimba.
**********

USAILI WASANII WA MUVI MIKOANI WASITISHWA
Kutoka ndani ya Kampuni ya Tollywood ambayo ni waandaaji wa filamu za ukweli nchini, ShowBiz imedondoshewa ishu kwamba kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao, wameshindwa kuendelea na zoezi la usaili kwa wasanii wa mikoa ya Morogoro, Tanga, Arusha, Mwanza na Kisiwa cha Zanzibar kwa ajili ya kupata wasanii watakaoshiriki kwenye muvi mpya zinazotarajiwa kuandaliwa ikiwemo ‘Tears On Valentine Day’.

Akipiga stori na ShowBiz, Mkurugenzi wa Filamu ndani ya kampuni hiyo, Hamie Rajabu alisema kwamba, kutokana na hilo wanawaomba radhi wasanii wote waliojitokeza kujaza fomu kwa usumbufu walioupata, lakini wakaahidi kurudia zoezi hilo baada ya kurekebisha tatizo lililojitokeza.

“Sisi kama Tollywood tunawaomba radhi wasanii wote waliojitokeza kujaza fomu, kinachoendelea kufanyika kwa sasa tunawapigia simu wahusika wote na kuwaita katika vituo walivyochukulia fomu kisha kuwarudishia pesa zao, hata wale ambao simu zao hazipatikani kama watapata nafasi ya kusoma gazetini waende walipojazia fomu ili warudishiwe pesa zao,” alisema Hamie Rajab.

Aidha, mkurugenzi huyo alisema kwamba, wanatarajia kuwapata vijana zaidi ya 30 ambao walishiriki katika zoezo hilo Dar es Salaam na siku kadhaa zijazo watawapigia simu mmoja baada ya mwingine, hususan wale waliofanya vizuri kwenye usaili ambao ulifanyika katika ofisi za Tollywood wiki mbili zilizopita.
********
MKALI WA MWEZI (MONTHLY BEST PERFORMER
Majina 10 ya mastaa wa Bongo yanaoyoendelea kutajwa kuwania ushindi wa mwezi (Mkali wa mwezi) kunako mpambano huu yatatajwa wiki ijayo, kisha wewe msomaji utapata fursa nyingi ya kudondosha kura yako ukimtaja mmoja ambaye unadhani anastahili kuwa mshindi wa mwezi huu wa Julai.

Kabla ya kuyataja majina hayo, ShowBiz inakupa nafasi ya mwisho wiki hii kutuma jina la staa ambaye unadhani anastaili kuwa bingwa. Tutumie SMS kupitia simu namba 0787-110 173. E-mail:mcgeorge@gmail.com.
***********

Ijumaa Sexiest Barchelor inakuja
Shindano la ukweli lililowahi kuwavutia mashabiki wengi, Ijumaa Sexiest Barchelor linaloandaliwa na gazeti hili linakuja tena kwa kasi ya ajabu. Ili kuwapata mastaa wa kiume ambao watashiriki kwenye mpambano huo wewe msomaji na mpenzi wa shindano hilo unahusika.

Unachotakiwa kufanya ni kututumia jina la staa wa kiume ambaye unadhani anastahili kuingia kwenye mpambano huo utakaoanza hivi karibuni. Andika ujumbe mfupi (SMS) ukilitaja jina hilo kisha tuma kwenda simu namba 0787-110 173.
_____
Compiled by mc george

1 comment:

Anonymous said...

Hakukopi Usher alikuwa ni Mwanafunzi wa Michael Jackson ,Usiwe unaandika tuu u should read Magazines Oky!!!!Dnt Copy and Paste unapotosha jamiii for your Information hata Chriss Brown alikuwa mwanafunzi wake Common ooh polizeee dnt write smthing grrrrrrrrrrrrrrrrr