Wednesday, September 2, 2009

Zijue faida za funga kiafya - 2

Kama tulivyoona wiki iliyopoita kuhusu faida za funga kiafya, mbali na faida za kiroho, wiki hii tunaendelea na makala haya kwa kuangalia ni jinsi gani funga inavyofanyakazi mwilini na kumletea mtu faida hizo. Wakati wa siku za mwanzo za kuanza kufunga, ambazo ndiyo huwa ngumu sana, idadi kubwa ya uchafu wa mwili (waste) hufurika kwenye mfumo wa damu (blood system), tayari kutolewa nje ya mwili kama uchafu kupitia kila aina ya upenyo uliyopo mwilini.

Kwa baadhi ya watu utaona wanapokuwa kwenye funga, midomo yao huwa na utando mweupe kwenye ulimi na hutoa harufu mbaya mdomoni, hiyo ina maana kwamba kazi ya mwili kuondoa uchafu na sumu mwilini imeanza kufanyika.

Siku zinavyoenda, mchakato wa kusafisha mwili huimarika zaidi, mwili huondoa mafuta, chembechembe za mwili ambazo zimeathirika pamoja na uchafu mwingine mzito unaoweza kutolewa kwa njia ya haja kubwa. Funga inapoendelea kwa muda mrefu zaidi, sumu zilizojikusanya kwa muda mrefu kwenye chembechembe hai (cells) za mwili nazo huweza kutoka, zikiwemo chembechembe zilizoathirika, zilizokufa, uchafu wa kwenye utumbo mdogo, kwenye ini na kwenye figo.

Kipindi hiki, mwili hubakiza vitamini na madini muhimu mwilini na kutoa nje sumu na tishu zote zisizohitajika. kiwango cha sumu kinapopungua au kwisha mwilini, utendaji kazi wa seli zilizobaki huongezeka, hali hii huongeza uponyaji mwilini.

Hivyo basi, katika kipindi hiki, mwili huwa katika mtindo wa ‘kuhifadhi nishati’ na ‘kuponya’, ikiwa na maana kwamba mtu huanza kujiona ni mwenye nguvu na afya njema wakati na mara baada ya kumaliza kipindi cha funga.

KWA NINI MTU HUJIONA NA NGUVU BAADA YA KUFUNGA NA KUTOSIKIA NJAA?
Siyo wengi wanafahamu kuwa mwili unahitaji nishati nyingi sana ili iweze kusaga chakula tumboni. Funga hupumzisha mfumo wa usagaji chakula na badala yake nishati iliyokuwa itumike kusagia chakula, hutumika katika kuuponya na kuukarabati mwili.

Usafishaji na uondoaji wa sumu unaofanyika kwenye utumbo mdogo, damu na chembechembe hai za mwili, huuondolea mwili magonjwa mengi. Kwa maana hiyo funga huimarisha kinga ya mwili na kuifanya ifanye kazi yake ipasavyo na husaidia kuboresha afya ya kimwili na kiroho.

FAIDA ZA FUNGA KWA UJUMLA WAKE
Kwa ujumla, funga ina faida nyingi zifuatazo: Hutoa ahueni kwa matatizo mengi ya kiafya pale mtu anapoamua kufanya mabadiliko katika staili ya maisha anayoishi hasa kwa upande wa ulaji.

Funga ni faraja ya kuondoa mazoea (addictions) ya vitu mbalimbali kama vile kahawa, sigara, dawa za kulevya na ulevi (alcohol). Funga husaidia sana kuondoa hali ya kukata tamaa, ambayo ndiyo huwa kikwazo kikubwa kwa watu wengi wanaojaribu kuacha mazoea ya kitu.

Funga husaidia kushusha kolestro mwilini na kuondoa tatizo la presha. Aidha, funga hufanya maajabu katika matatizo ya ukosefu wa choo, gesi na kujaa kwa tumbo kwa kuondoa tatizo.

Funga huboresha umakini, hali hii hujidhihirisha baada ya sumu kuondolewa kwenye mfumo wa damu na tezi. Ulaji kidogo hutumia nishati kidogo katika usagaji chakula hivyo kuacha nishati ya kutosha inayohitajika na ubongo katika kazi za kufikiri.

Faida nyingine anazoweza kuzipata mtu kwa kufunga ni pamoja na kupunguza uzito wa mwili, kuimarisha ngozi na kuimarisha pumzi.

“Funga ni mchakato mkubwa wa kupumzisha viungo vya mwili. Katika kipindi hicho cha mapumziko, funga hukusaidia kurejesha nguvu za utendaji kazi na kurejesha nishati iliyopotea kutokana na pilika za kila siku na tabia isiyofaa ya ulaji vyakula,” anasema D.K Frank Sebastin wa Marekani,
akielezea ufanisi wa funga.

No comments: