Wednesday, September 16, 2009

Zingatia haya wakati wa kufungua


Baada ya kuangalia faida za kiafya zinazopatikana kwa mtu anayefunga, leo tutakufahamisha mambo muhimu unayopaswa kuzingatia wakati wa kufungua, hasa kwa upande wa faida za kiafya.

Faida kubwa inayopatikana kutokana na kufunga inaweza kupotea na kusababisha madhara kama kanuni za kufungua hazitazingatiwa. Kwa kawaida wakati wa kufungua, kwa mfano magaharibi kwa waislamu, watu hukimbilia kula vyakula vya kila aina na kwa kiasi kikubwa.

Kwa watu waliofunga kwa sababu za kiafya, wanaweza pia kujikuta kwenye matatizo iwapo wataanza kufakamia vyakula bila mpangilio na bila kuzingatia aina vyakula vyenye faida mwilini. Hili linatokana na ukweli kwamba, wakati wa kufungua, mtu hupatwa na hamu kubwa ya kula.

Kwa hakika, faida ya funga inapatikana kwa aina ya chakula utakachokula baada ya kufungua na jinsi gani utakavyoweza kujizuia kula vyakula visivyosahihi baada ya hapo. Wakati wa kufungua mtu anapaswa kuanza kwa kula vyakula vya asili kama vile maji, juisi halisi, matunda au uji wa nafaka, vyakula ambavyo havina kemikali za zumu na baada ya hapo kula mlo ulio sahihi na kwa kiasi cha kawaida.

Ni makosa makubwa kufungua kwa kuingiza tena sumu mwilini, kama vile kufungua kwa kuvuta sigara, kula mishikaki au vyakula vingine vilivyopikwa na mafuta mengi. Aidha, mtu anayefungua anatakiwa, si tu kula vyakula vya asili, bali pia kula kwa kiasi na siyo kula kupita kiasi kwa lengo la kufidia mlo wa mchana kutwa.

Mwisho kabisa, inashauriwa mfungaji kuendelea kuzingatia kanuni za ulaji sahihi, funga itakuwa haina faida yoyote kiafya iwapo wakati wa kufungua unakula kila aina ya chakula unachokiona mbele yako tena kwa kiwango kikubwa, itakuwa sawa na kujaza maji kwenye gunia ambayo kamwe hayawezi kujaa.

Kwa waislamu ambao wamekuwa wakifunga katika mwezi huu wa Ramadhani, kwa kuzingatia nguzo za dini yao na kwa kuzingatia kanuni za ulaji sahihi, bila shaka watakuwa mashahidi wa haya tuliyoyaandika katika mfululizo wa makala yetu, kwani afya zao sasa zimeimarika tofauti na ilivyokuwa kabla. Tunashauriwa kufunga mara kwa mara ili kulinda miili yetu dhidi ya maradhi.

Nawatakia funga na Idd njema waislamu wote duniani na Mungu awabariki!

No comments: