ILI mwanadamu awe na afya bora, anapaswa kula nafaka na mboga za majani kwa wingi ambazo ndizo zenye virutubisho vyote muhimu kwa ustawi wa mwili.
Nafaka hizo ni kama vile mahindi, mchele, ngano, mtama, nk., ambao haujaondolewa virutubisho vyake.
Aina hii ya vyakula ndiyo msingi mkubwa wa afya ya binadamu. Pengine kabla ya kuangalia aina nyingine, tuangalia ukweli kuhusu aina hii ya chakula (nafaka), kwa nini kikaitwa ndiyo msingi bora wa afya.
Kwa mujibu wa wanasayansi, mwili wa binadamu una jumla ya chembechembe hai (cells) zaidi ya trioni 70. Katika hizo ndipo ulipo uhai, zinapokufa na binadamu naye hufa, zikiwa dhaifu na mtu naye huwa hivyo hivyo.
Binadamu hawezi kuwa na afya njema kuliko chembechembe zake kwani ndizo zinazopokea virutubisho na kutoa uchafu mwilini, ikiwemo sumu.
Ili chembechembe hizo ziwe hai zinahitaji kula na chakula chake ni virutubisho tu ambavyo asilimia kubwa na muhimu inapatikana katika vyakula vya nafaka. Ndani yanafaka, kama vile mchele, ngano na soya, mbali ya vitu vingine, kuna aina mbili muhimu za mafuta (fats), ambazo ni Lipids na Steroids.
Aina hizo mbili za mafuta ni muhimu sana kwa uhai na ustawi wa chembechembe za mwanadamu. Mafuta aina ya Lipids hufanyakazi ya kulisha na kukarabati ukuta wa chembechembe na Steroids huzalisha nishati zinazompa binadamu nguvu thabiti.
Madhara ya kuwa na chembechembe dhaifu ni makubwa na unaweza kuyasikia mwenyewe. Kwanza mwili huwa mchovu, usio na nguvu, unapotumia dawa hazifanyi kazi upesi mwilini, kama ni dozi ya Malaria, ni lazima utumie zaidi ya moja au dawa kali zaidi! Katika hili wengine wanasema fulani ana Malaria sugu, lakini ukweli ni kwamba chembechembe zako zimekauka, hazina tena uwezo wa kupenyeza kitu na kutoa sumu mwilini.
MATUNDA NA MBOGAMBOGA
Hili ni kundi la pili la chakula ambalo nalo ni muhimu sana. Baada ya kujenga mwili (chembechembe hai), sasa unahitaji kuulinda ili uwe imara na unaofanya kazi yake sawasawa. Kazi hiyo inafanywa kwa kula matunda na mbogamboga kwa wingi, chakula hiki ndicho kinachojenga kinga ya mwili (Body Immunity System), hivyo kuupa mwili wako uwezo wa kujikinga dhidi ya wavamizi, ambao ni maradhi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO), binadamu anatakiwa kula milo ya matunda na mboga kati ya 5-9 kila siku. Mboga na matunda zina virutubisho muhimu vinavyotoa kinga mwilini (Anti-oxidant) ambayo hupambana na kuondoa viini vya magonjwa (free radicals).
Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya watu hula matunda kwa nadra sana na wengine hawali kabisa! Msimu wa matunda unaingia mpaka unaisha, mtu hajala hata tunda moja au kama kala, basi ya kuhesabu, wengine mpaka waagizwe na daktari - hii ni hatari kwa afya yako.
Kwa upande wa mboga za majani hali ni mbaya zaidi, watu hawapendi kula mboga za majani, zinachukuliwa kama chakula cha kimasikini, bila kujua kwamba kwa kuacha kula mboga za majani unaunyima mwili wako kitu muhimu sana.
Ni vizuri ikaeleweka kwamba binadamu hatuwezi kula kama zinavyotaka nafsi zetu, bali tunapaswa kula kama miili yetu inavyotaka. Sisi hatuwezi kuwa muhimu kuliko miili yetu. Mwili ukiamua kugoma huwa hatuna ujanja. Unapopatwa na kiharusi na kupooza mwili, kwa mfano, hapo mwili huwa umegoma kufanyakazi na chanzo huwa ni wewe mwenyewe!
Mwili umeumbwa kama mnyororo, unategemeana sehemu moja na nyingine, sehemu moja inapopatwa na tatizo, mwili mzima unataabika. Ukipatwa na jipu au uvimbe kwenye kidole chako cha mwisho, mwili mzima utakosa raha na hata usingizi unaweza usipate kwasababu ya maumivu! Hivyo hatuna budi kutii miili yetu kwa kula vyakula ambavyo inavihitaji.
No comments:
Post a Comment