Friday, October 9, 2009

Wote hawa kusimama steji moja na A.Y Kesho


Ile siku iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu kubwa na wapenda burudani hatimaye imewadia. Maelfu ya Wabongo na Afrika kwa ujumla tayari macho na masikio yao yameelekezwa kunako sherehe za utoaji tuzo, MTV Africa Music Awards (MAMA) zitakazofanyika Nairobi, Kenya kesho.

Katika sherehe hizo, Wabongo tunayo sababu ya kujivunia kwakuwa tunao wawakilishi wawili, Ambwene Yesaya ‘A.Y’ anayewania tuzo ya Mwana Hip Hop Bora akipambana na kina Jay-Z, Kanye West na M.I huku mwanadada Sara Kais ‘Shaa’ akiwania tuzo ya Msanii anayechipukia.
Mbali na hilo, kijana Ambwene Yesaya atatuwakilisha pia kunako steji kwa kupiga shoo mbili za kusindikiza usiku huo akiwa ni miongoni mwa wasanii wengine kibao kutoka pande mbalimbali waliokula shavu hilo adimu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa waandaaji, wasanii wengine wataokapanda stejini kwa ajili ya burudani ni pamoja na 2Face (Nigeria), Amani (Kenya), Brickz (South Africa), D’Banj & the Mo Hits Allstars, (Nigeria), HHP (South Africa), Nameless (Kenya), Pype (Nigeria), STL (Kenya) na Zebra & Giraffe (South Africa).

Wengine ni Akon (Marekani), Wyclef Jean (Marekani), M.I. (Nigeria), Lizha James, Fally Ipupa (Congo), Blu3 (Unganda), Da LES, Lira, Nameless (Kenya), Samini na Wahu.

Mbali na hayo pia itatolewa tuzo kwa msanii bora anayechipukia kupitia kipengele kilichopewa jina la ‘My Video’ ambapo wasanii wachanga kutoka sehemu mbalimbali Afrika walitakiwa kutuma clip za video zao na baada ya mchujo walipatikana Anita Akuffo (Ghana), Richard Kawesa (Uganda), Debra Phiri (Zambia), Julia Thaitai (Kenya), Bleek Chindime (Malawi), Rosaline Strasser-King (Sierra Leone), Vanessa Bernard (Tanzania), Patricke-Stevie Moungondo (Congo Brazzaville), Sadie Buys (South Africa) na Chinyere Uju (Nigeria).

Kutokana na zali hilo, wasanii hao walijipatia tiketi ya kuhudhuria kwenye sherehe hizo na mmoja kati yao ambaye atakuwa na kura nyingi anaibuka na ‘katuzo’ kake, huwezi jua anaweza akawa Mbongo ambaye ni Vanessa Bernard. Usikose kufuatilia tukio hilo.

No comments: