Tuesday, November 10, 2009

Safisha tumbo lako kwa chakula


WAZUNGU wana msemo usemao ‘death begins at colon’, ukiwa na maana kwamba kifo huanzia kwenye utumbo mpana. Matatizo mengi ya kiafya yanayosababisha maradhi sugu na hatari na hatimaye kuchukua uhai wa mtu, huanzia kwenye utumbo (tumboni).

Chanzo cha hali hiyo hutokana na mtu kula chakula kama kawaida na kushindwa kupata choo cha kutosha kwa muda mrefu. Hali hiyo inapoendelea, mabaki ya chakula yaliyopaswa kutolewa nje ya tumbo kwa njia ya haja kubwa, hugeuka na kuwa sumu na kuathiri mfumo mzima wa mwili.

Kwa kuzingatia ukweli huo, ndiyo maana wataalamu wetu wa masuala ya lishe na afya wamesisistiza kufanya linalowezekana kuhakikisha tunasafisha matumbo yetu kwa kupata choo cha kawiada kila siku. Kuna njia nyingi za kusafisha tumbo, ikiwemo ile maarufu ya ‘enema’ ambayo tumeshaieleza zaidi ya mara moja katika makala zetu zilizopita. Lakini katika makala ya leo tutaangalia usafishaji wa tumbo wa asili kwa kutumia vyakula asilia.

Usafishaji wa tumbo unaweza kufanyika ukiwa nyumbani kwako na ukaufanya bila wasiwasi wowote kwa kula tu vyakula vyenye uwezo wa kufisha tumbo.

Njia hii siyo tu ni rahisi kuifanya, lakini pia ni salama na ni ya kiafya zaidi katika suala zima la kusafisha utumbo. Gharama za kusafisha tumbo huwa ni za juu sana iwapo utataka uipate kutoka clinic au kwa wataalamu wengine wa afya, lakini huwa siyo lazima. Unahitaji kujua tu aina ya vyakula vinavyosaidia kusafisha tumbo.

VYAKULA BORA
Vyakula bora vinavyoaminika kufanyakazi nzuri ya kuimarisha mfumo wa usagaji chakula na hatimaye kusaga chakula kirahisi na kwa haraka ni vile vyenye kiwango kikubwa cha ‘fibre’ (kamba lishe). Vyakula hivyo ni pamoja na mboga na matunda mbalimbali.

Kwa mujibu wa wataalamu wetu, matunda na mboga ndiyo yenye kiwango kikubwa cha ‘fibre’ au ufumwele. Matunda aina ya Tufaha (Apple), Peasi (Peas), makomamanga, n.k, yana kiwango kikubwa cha ‘fibre’ hivyo yanafaa kuliwa kwa wingi.

Kwa upande wa mboga-mboga na nafaka, kuna maharage, kunde, ngano na nafaka nyingine zisizokobolewa, vyakula hivi vyote vinaaminika kuwa na kinwago kikubwa cha ‘fibre’. Hivyo ili kulijengea tumbo lako mfumo mzuri wa kusaga chakula na baadae kupata choo chepesi na cha uhakika kila siku, pendelea kula matunda kwa wingi na vyakula vingine vilivyoainishwa hapo juu.
FAIDA ZA KUSAFISHA TUMBO
Baadhi ya wataalmu wa masuala ya afya wanasema kuwa usafishaji wa tumbo hupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya saratani, kidole tumbo na matatizo mengine. Tumbo linapokuwa chafu huathiri uzito wa mwili, afya ya akili na hata ngozi ya mwili.

KIWANGO KINACHOTAKIWA KWA SIKU
Tunapohimizwa kula kwa wingi matunda, mboga na vyakula vingine vyenye kiwango kikibuwa cha ‘fibre’, ni vyema tukajua pia ni kiasi gani kinachopendekezwa. Kwa mujibu wa wataalamu, mtu mzima mwenye umri chini ya miaka 50, anatakiwa kula kiasi cha gramu 38 kila siku. Watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 50 wanatakiwa kula kiasi cha gramu 30. Wanawake wenye umri chini ya miaka 50 wale gramu 25 na wale wa zaidi ya miaka 50, wale gramu 21.

1 comment:

Anonymous said...

asante kwa kutuletea mambo ya afya mara kwa mara, tangu nimesoma article zako kwa kweli nimefatila maadili ya afya na mambo yangu hasa ya kwenda choo yameiprove ile mbaya, thank you so much, hata sikuitaji kwenda kwa doctor baada ya kosoma website yako. keep it up man . and god bless.