Tuesday, May 11, 2010

MNAONYONYESHA WATOTO SOMENI HAPA!


Bila shaka kila mzazi anajua kuwa mtoto mchanga chakula chake ni maziwa, lakini si wote wanaojua maziwa yanayotakiwa ni ya mama tu na siyo mengine. Pia siyo wote wanajua hasara na madhara anayoyapata mtoto asiyenyonya maziwa ya mama yake.

Katika makala ya leo, tutazungumzia umuhimu wa maziwa ya mama kwa mtoto na pia kujifunza ni wakati gani mtoto anapaswa kunyonyeshwa. Ni vyema ikaeleweka kuwa ili mtoto apate faida za maziwa, ni lazima kanuni za unyonyeshaji zizingatiwe.

Kwa mujibu wa jarida moja la masuala ya lishe liitwalo Nutritional Neuroscience, kiwango cha virutubisho vilivyomo kwenye maziwa ya mama hubadilika kila baada ya saa 24 kulingana na mahitaji ya mtoto, kikiwemo kirutubisho kama vile nucleotides, ambacho hurekebisha usingizi wa mtoto.

Kwa maana hiyo, mtoto anapaswa kunyonya maziwa ya mama moja kwa moja kutoka katika chuchu la mama na muda ule ule. Ni makosa makubwa kwa mama kukamua maziwa yake na kuyahifadhi sehemu na kumnywesha mtoto baadaye. Ni makosa makubwa kufanya hivyo.

Kwa kufanya hivyo, siyo tu utakuwa unapoteza virutubisho vyote muhimu, bali pia utakuwa unavuruga hata mfumo wa fahamu wa mtoto, kwani anaweza kuwa analala wakati ambao alipaswa kuwa macho na kuwa macho wakati alipaswa kulala. Kwa sababau kwenye maziwa kuna aina ya virutubisho ambavyo kazi yake ni kurekebisha mfumo wa fahamu wa mtoto.

FAIDA ZA MAZIWA YA MAMA
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema kwamba maziwa ya mama ndiyo chakula bora kuliko vyote kwa mtoto mchanga na kwamba yanakidhi mahitaji yote ya kukua kisaikolojia kwa mtoto katika kipindi cha miezi sita ya kwanza na hivyo mtoto asipewe chakula kingine zaidi ya maziwa ya mama.

Halikadhalika, maziwa siyo tu yanatoa kinga kwa mtoto dhidi ya magonjwa kama mafua, kuharisha na kifo cha ghafla, bali hutoa kinga dhidi ya maradhi mengine ya baadaye kama pumu, unene, ‘aleji’ mbalimbali pamoja na kutoa kinga dhidi ya unene (obesity). Mbali na hayo, maziwa ya mama hukuza ufahamu wa mtoto (Intellectual Development).

Vile vile, maziwa ya mama yana kirutubisho aina ya PSTI, ambacho hulinda na kukarabati utumbo mdogo wa mtoto ambao mwanzo huwa ni laini sana. Inaelezwa kuwa kirutubisho hicho muhimu hupatikana kwa wingi kwenye maziwa ya mama katika siku chache tu baada ya kujifungua.

Faida za maziwa ya mama haziishii kwa mtoto peke yake, bali zinaenda hadi kwa mama pia. Akina mama wanaonyonyesha, hupunguza haraka ule uzito ulioongezeka wakati wa uja uzito na hutoa kinga kwa mama dhidi ya ugonjwa wa kukauka damu (anaemia), shinikizo la damu na mfadhaiko. Vile vile kunyonyesha kunamuepusha mama na saratani ya matiti.

Ewe mama, acha ‘uzungu’, mnyonyeshe mwanao maziwa yako kwa faida yake na yako na pia kwa ustawi wake wa kiakili na kimwili!

1 comment:

Unknown said...

I love this. Hey mama kijachos zingatia hii kwa afya bora za watoto.