Friday, June 11, 2010

IJUMAA SHOWBIZ!

Wahu: Ampoteza Amani Bongo
Binti aliyesimama vyema ndani ya sanaa ya muziki wa kizazi kipya kutoka pande za Kenya, Wahu ambaye juzi kati alidondoka Bongo na kutoa sapoti kwenye uzinduzi wa albamu ya Temba na Chegge, ametajwa kuchukua nafasi ya mwanadada Amani ambaye hivi sasa anaonekana ‘kudrop’ kimtindo.

Baadhi ya wadau wa burudani waliohudhuria kwenye uzinduzi huo uliyofanyika ndani ya Club Sun Cirro,Ubungo Dar mwishoni mwa wiki iliyopita walisema na ShowBiz kwamba hivi sasa Wahu anaonekana yuko juu kuliko wanawake wengine waliopo kwenye game huko nyumbani kwao Kenya.

“Siku hizi siwasikii kwa sana wasanii kama Amani, Nyota Ndogo na wengine waliowahi kuja Bongo na kufunika zaidi ya Wahu ambaye tangu ali poibukia kwenye game hiyo na kufanya vyema na ngoma yake, ‘Sweet Love’ hajawahi kuzimika zaidi ya kusonga mbele.

Akipiga stori na safu hii muda mchache baada ya kushuka stejini, Wahu alisema kwamba anajisikia fahari sana kufanya kazi na wasanii wa Bongo na kualikwa pande hizi mara kadhaa kwa ajili ya shoo. Msanii huyo amewahi kufanya kazi na wasanii kadhaa wa Tanzania wakiwemo Chegge na Temba.
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

shumba: kiongozi wa Makhirikiri
Shumba:alianza kama mcheza shoo, sasa ni staa wa Afrika, kudondoka na Makhirikhiri Mbeya
Kundi la muziki wa asili kutoka Botswana, Matsuwe Tradition Dance maarufu kama Makhirikhiri bado lipo Bongo na kinachofuata hivi sasa ni ziara mkoani Mbeya ambapo litaangusha shoo ndani ya Uwanja wa mpira wa Sokoine Juni 12, mwaka huu kabla ya kumalizia Iringa katika Uwanja wa Samora.

Sisi kama ShowBiz leo tunamcheki kiongozi wa kundi hilo, Moses Malapela ambaye ana a.k.a ya Shumba Ratshega. Wengi hawajui Shumba katoka wapi mpaka kufikia hapa alipo leo kama kiongozi wa kundi la Makhirikhiri mwenye sauti ya kipekee katika ngoma za muziki huo wa asili.

Mchizi alizaliwa 1981 katika kijiji cha Bobonong, nchini Botswana ni miongoni mwa wasanii wa muziki huo waliopitia pilikapilika za hapa na pale. Alianza kama mcheza shoo ndani ya Kundi la Re Tlaa Re Ke Dipitse Cultural Group lililokuwa hapo hapo kijijini kwao.

Baada ya hapo alijimuvuzisha hadi kwenye kundi lingine lililokuwa na jina la Motswedi Cultural Group. Jina la Shumba alilipata kupitia kabila yao, Kalanga likiwa na maana ya Simba huku lile la Ratshega kwa mashabiki wake alipokuwa akipiga shoo.

Alitoa albamu yake ya kwanza kama muimbaji na mchezaji mwaka 2006 ikiwa na jina la Masiela. Albamu hiyo ambayo haikumtambulisha vyema ilifuatiwa na Makhirikhiri 2007 ambayo ilifanya vizuri na kuuzwa katika nchi kibao zikiwemo Botswana yenyewe, Afrika Kusini, Namibia, Zambia na Zimbabwe.

Mwaka huo huo wa 2007, kupitia Tuzo zenye jina la Mascom-Bomu Awards, Makhirikhiri aliibuka na ushindi kama albamu bora ya asili. Mwaka 2008 Shumba aliitambulisha albamu mpya yenye jina la Ntopolela Bichana kupitia wimbo wa Dikhwaere. Mwaka jana wa 2009 akatambulisha albamu nyingine yenye jina la Kukantsu.

Kupitia muziki wake, Shumba ameweza kujiwekea heshima ndani na nje ya nchi yake Botswana, mfano mzuri ni pale alipofanya shoo mbele ya rais wao mwaka 2008 kwenye sherehe za uhuru na kuwaburudisha mawaziri wote wa nchi hiyo kwenye hafla ya chakula cha usiku.

Kupitia kundi lake, Makhirikhiri, Shumba amewahi kufanya shoo Afrika Kusini, China, Namibia, Zambia na Angola kabla ya kuja Tanzania. Kutokana na heshima aliyoijengea nchi yake kabla hajaja Tanzania, Rais wao, Lt General Seretse Khama Ian Khama alimkabidhi bendera kwa ajili ya kuitangza zaidi Botswana.
**********************************
Jaffarai: Demu wangu tayari kideoni
Kutoka pande za Kijitonyama, Dar mchizi aliyewahi kufanya vyema kupitia ngoma yenye jina la ‘Napenda nini’, Jaffari Ally Mshamu a.k.a Jaffarai amesema na ShowBiz kwamba ‘Demu wangu’, ngoma yake inayofanya vyema hivi sasa tayari imetupiwa kwenye kamera za video na muda wowote inaanza kuuza kunako vituo kadhaa vya televisheni.

Akipiga stori zaidi, Jaffarai alisema kwamba video ya ngoma hiyo imefanyika sehemu kadhaa ndani ya Dar es Salaam chini ya mtayarishaji John Kallage huku ikiwauzisha sura mastaa kibao wa Bongo flava na wadau wa muziki huo ambao ni kipenzi cha msanii huyo.

“Bado naamini kuwa ili msanii afanye kazi nzuri hata kama ni mkongwe lazima aumize kichwa kwa kuandika kazi nzuri, ndiyo maana mimi niko ‘bize’ kuhakikisha kila ngoma ninayotoa inakuwa juu kama hii “Demu wangu’ niliyomshirikisha TID ambaye hakufanya masihara kwenye korasi,” alisema Jaffarai.
xxxxxxxxxxxxxxx

Twanga kusheherekea miaka 10
Bendi maarufu ya muziki wa dansi, African Stars a.k.a Twanga Pepeta inatarajia kuadhimisha miaka kumi tangu kuanzishwa kwake kwa sherehe ya kipekee itakayofanyika ndani ya Viwanja vya Leaders Club Juni 27, mwaka huu.

Akipiga stori na ShowBiz, Mkurugenzi wa ASET, Asha Baraka alisema kwamba ishu hiyo ambayo itakwenda sambamba na kusheherekea albamu yao ya kumi, ‘Mwana Dar es Salaam’ itaanza kwa maandamano kutoka kwenye ofisi zao zilizopo Kinondoni mpaka kwenye viwanja hivyo.

“Baada ya kufika uwanjani kutakuwa na michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, mpira wa wavu kwa wanawake, mbio za kuku, burudani ya muziki kutoka kwa wasanii wa ndani na nje ya Bongo na mambo mengine mengi ambayo yataifanya siku hiyo ionekane ya kipekee,” alisema Asha Baraka.

Mengi zaidi kuhusu shughuli hiyo, endelea kufuatilia kwenye magazeti yanayochapishwa na Kampuni ya Global Publishers.
xxxxxxxx

No comments: