Tuesday, August 24, 2010

ZIJUE FAIDA ZA TENDE NA MAAJABU YAKE

Tende ni tunda maarufu sana katika nchi za Mashariki ya Kati na sehemu zingine duniani. Umaarufu wake umeanzia maelfu ya miaka iliyopita na pengine ndiyo tunda pekee liliotajwa sana hata katika vitabu vitakatifu vya Mungu.

Wakati huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, matumizi yake huongezeka kwa kiwango kikubwa kwa sababu ya kutumiwa na idadi kubwa ya waumini wa dini ya Kiislamu wakati wa kufungua swaumu au wakati wa kufuturu.

Lakini pengine ni vizuri kujua siri ya kupendwa na hata kutajwa sana kwenye vitabu vya Mungu kwa tunda hili. Lina umuhimu na faida gani katika mwili wa binadamu kiasi cha kuwa maarufu hivyo?

FAIDA ZA TENDE
Wanasayansi wa masuala ya vyakula wamelishafanyia utafiti tunda hili na kugundua kwamba sifa yake kubwa ni kuwa chanzo kikubwa cha virutubisho na nishati ya mwili (energy). Mtu ukila tende mwili huweza kupata nguvu mara moja.

Hivyo ni wazi kwamba waumini wanaofunga mchana kutwa wanahitaji kula vyakula vya kurejesha virutubisho na nishati mwilini ambayo ilikosekana kwa siku nzima. Kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha nishati, mtu anaweza kuendelea kuishi kwa kula tende na maji tu.

Tunaelezwa kuwa, tende ina virutibisho muhimu visivyopungua kumi, vikiwemo Calories, Calcium, Protein, Potassium, Magnesium, Phosphorous Vitamin A, Folate, Carbohydrates ambavyo vyote ni muhimu kwa kinga na ustawi wa mwili wa binadamu.

TENDE DAWA YA UKOSEFU WA CHOO
Kwa wale wenye matatizo ya kukosa choo kwa muda mrefu, tende inaweza kuwa suluhisho la tatizo hilo. Imeelezwa na wataalamu kuwa tende ina kiwango kikubwa cha kamba-lishe (fibre) ambazo ni muhimu kwa ulainishaji wa chakula na kuwezesha kupatikana kwa choo kirahisi.

Kama una tatizo sugu na la muda mrefu la ukosefu wa choo, tumia tende kama dawa ya kulainisha choo (laxative) kwa kuloweka kwenye maji usiku kucha, kisha asubuhi zikoroge katika maji hayo na kunywa juisi yake, fanya hivyo kwa wiki mara mbili.

Aidha, tende imegundulika kuwa na uwezo wa kutoa kinga dhidi ya maradhi ya saratani ya tumbo (colon cancer). Vile vile ina uwezo wa kuimarisha afya ya moyo na kuukinga na maradhi mengine kwa kunywa juisi yake ambayo hutengenezwa kwa kulowekwa kama ilivyoelezwa hapo juu.

Kutokana na wingi wa virutubisho vilivyomo, tende huweza pia kutibu magonjwa mengine ya tumbo, yakiwemo kujaa gesi, kuharisha na kuchafuka kwa tumbo. Kwa wale walevi wa kupindukia, ambao miili yao imejaa sumu, tende huweza kuwa na msaada mkubwa wa kuondoa sumu hizo katika miili yao.

Hivyo basi, tende isiliwe mwezi wa Ramadhani peke yake, bali iwe ni chakula ama tunda la kuliwa wakati wote na watu wote, kwa sababu kila mtu anahitaji kuwa na afya bora, bila kujali imani ya dini aliyonayo.

5 comments:

emu-three said...

Aisee, kweli isiliwe tu mwezi wa Ramadhani pekee, iagizwe kwa wingi basiii

tweety said...

Allah akuzidishie. Amin

BabyAmore said...

good news brother sikujua haya kabla sasa ni juice ya tende kwangu kwenda mbele

moloni said...

Ok

msita mbwambo said...

Fact brother