Tuesday, August 3, 2010

ZIJUE SIRI ZA KUPUNGUZA UA KUONGEZA UZITO


Baada ya kupata maswali mengi kutoka kwa wasomaji wetu kuhusu suala la kupunguza na kuongeza uzito, leo ninafuraha kuwaletea tena makala haya kuhusu somo hilo ambalo naamini likizingatiwa kwa makini, linaweza kuleta matokeo yanayotarajiwa na mtu.

Inapaswa kukumbukwa kwamba suala la kupunguza uzito linahitaji nia, uvumilivu na uelewa wa vyakula unavyokula. Watu wengi wanafikiri kupunguza uzito ni kupunguza kula tu au kufanya sana mazoezi.

Kitu cha kwanza unachotakiwa kufanya ni kujielewa uzito wako - uko katika kundi gani? Je, wewe una uzito mdogo, uzito wa kawaida, uzito mkubwa au utipwatipwa? Hatua inayofuata ni kuamua kupunguza kilo zilizozidi au kuongeza zilizopungua. Inategemea lengo lako ni nini.

Kwa mfano, kama urefu wako ni futi 5.7, uzito wako unaokubalika kiafya ni kati ya kilo 55 na 70, ukizidi hapo, hasa kuanzia kilo 80 hadi 100, uko katika hatari kubwa ya kupatwa na magonjwa ya moyo na magonjwa mengine ya viungo, hivyo huna budi kuchukua hatua za haraka za kupunguza uzito.

Kitu kingine muhimu cha kuelewa ni kwamba unaweza kuwa na uzito unaokubalika kiafya, lakini ukawa huli matunda, mbogamboga na nafaka halisi hivyo ukawa una upungufu wa virutubisho muhimu mwilini. Kuwa na mwili mchangamfu na wenye afya njema ndiyo kitu muhimu zaidi, bila kujali una uzito gani.

Kwa wale wanaofanya mazoezi makali, kama vile kunyanyua vyuma, kucheza karate, n.k, wanashauriwa kupima upana wa kiuno na siyo kutegemea jeduali la uzito pekee. Wanaume wenye kiuno zaidi ya nchi 40 na wanawake wenye kiuono zaidi ya nchi 35, wako kwenye hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na magonjwa mengine ya moyo.

Ukitaka kupima kiuno chako, chukua tepu ya nguo (measure tape), vua shati ama blauzi kisha jipime eneo la chini ya tumbo kama unavyopimwa na fundi nguo saizi ya kiuno. Bila kubana mwili wako, shusha pumzi, tulia kisha jipime.

Sasa umefika wakati wa kupunguza uzito na unahitaji kujua utapunguza vipi na kitu gani kinatumika kama kichocheo katika suala zima la uzito wako. Kama nilivyowahi kudokeza katika makala zangu zilizopita, kiwango cha kalori (calories) anachokula mtu, ndicho ambacho kinachotawala uzito wa mtu. Unaweza kuuliza kalori nini?

Kwa kifupi, kalori ni njia ya kisayansi inayotumika kupima nishati ya mwili. Unahitaji kukisia kwa siku unaingiza mwilini kalori ngapi na unahitaji kiasi gani cha kalori kutokana na shughuli unazozifanya. Kwa sababu shughuli unazozifanya kila siku na chakula unachokula vinategemeana wakati wa kupunguza uzito. Kwa wastani mtu mzima kwa siku anahitaji kalori 2500 – 3000. Kalori imo kwenye kila mlo unaokula.

Kwa ujumla mazoezi au kujishughulisha kila siku ni muhimu kiafya. Mazoezi huusaidia mwili kufanya kazi yake vizuri na kudhibiti uzito kwa kuchoma kalori unazoingiza mwilini kama chakula na vinywaji kila siku.

FOMULA YA KUIMARISHA UZITO
Iili ubaki na uzito ulionao, kiwango cha kalori (chakula na vinywaji unavyokunywa) lazima kilingane na kalori unazozitoa (kwa njia ya kutumika mwilini, kwa njia ya mazoezi au kazi unazozifanya).
Itaendelea wiki ijayo...

No comments: