Tuesday, September 14, 2010

PRESHA: Muuaji tunayelala na kutembea naye


Kifo cha ghafla kinachotokana na shinikizo la damu hushtua watu na kinapotokea, maneno mengi husemwa na wakati mwingine kuhusishwa na imani potofu.

Lakini ni ukweli uliodhahiri kwamba shinikizo la damu ni ugonjwa hatari sawa na muuaji ambaye tunalala na kutembea naye kila siku bila sisi wenyewe kujijua. Wataalamu walioupachika ugonjwa huu jina la Silent Killer hawakukosea.

JITAMBUE
Binadamu hatuna budi kujitambua afya zetu na kuzingatia sana suala la kula vyakula sahihi ambavyo kila siku vinatajwa kuwa ni matunda, mboga, nafaka halisi, kunywa maji mengi na kufanya mazoezi. Mtu unapokuwa katika kundi la wale wasiozingatia masuala ya ulaji sahihi, huna budi kujitambua kwa kuangalia kama nawe unazo baadhi ya dalili zifuatazo:

Kuumwa kichwa mara kwa mara na kwa muda mrefu. Kusikia kizunguzungu mara kwa mara. Kusikia kichefuchefu na kutapika mara kwa mara. Macho kukosa nguvu na kuona maluelue, ni miongoni mwa dalili za shinikizo la damu. Ingawa dalili hizi zinaweza kusababishwa na jambo lingine, lakini kwa kiasi kikubwa ni ishara tosha ya kukufanya ukapime shinikizo lako la damu (presha).

Kama ukiwa na dalili hizo na ikawa ni kweli zinatokana na kuwa na shinikizo la damu, athari zake ni pamoja na mtu kupatwa na kiharusi (stroke), figo kushindwa kufanya kazi (kidney failure), kupatwa na upofu (blindness) au mstuko wa moyo (heart attack) na hatimaye kupoteza maisha mara moja.

JIKINGE
Mtu anaweza kujikinga na ugonjwa wa shinikizo la juu la damu (High Blood Pressure) kwa kufuata staili sahihi ya maisha na kuzingatia ulaji sahihi. Miongoni mwa vitu vya kuzingatia katika mlo ni kula vyakula vyenye virutubisho vya asili na kuepuka kula vyakula vya mafuta mengi.

Aidha, kuacha tabia ya kupenda kula sana chumvi na hasa kuongeza chumvi ya ziada wakati wa kula chakula mezani. Staili ya maisha unayotakiwa kuifuata ni ile ya kupenda kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuuweka mwili sawa.

Kama una uzito mkubwa, unatakiwa kupunguza uzito na kudumisha uzito unaoendana na umri pamoja na urefu wako. Halikadhalika, kwa wanaokunywa pombe, wanashauriwa kunywa kiasi kidogo na kuacha kuvuta sigara.

Kuwa na tabia ya mara kwa mara ya kucheki afya yako na hasa shinikizo la damu. Shinikizo la damu ni ugonjwa ambao unaweza kudhibitiwa kwa kuzingatia lishe zaidi kuliko dawa, ingawa kwa wale ambao wameshaathirika kwa kiasi kikubwa, dawa ndiyo kimbilio lao la kwanza.

Mwenye kufuata masharti ya ugonjwa huu, huweza kuishi nao kwa maisha yake yote bila kupata athari zingine hatari, kama vile kupatwa na kiharusi, kuharibika figo au kupatwa na upofu na athari nyingine nyingi.

VYAKULA VYA KUEPUKA
Nyama na mayai ni adui mkubwa wa mgonjwa wa presha. Ni wagonjwa wangapi wanafahamu kwamba vyakula hivi ni hatari kwa maisha yao na wakaacha kabisa kuvitumia? Naamini ni wachache sana wanaolifahamu hili na kulizingatia, hasa ukizingatia utamu wa vyakula hivyo.

Inaelezwa kuwa katika vyakula ambavyo mgonjwa wa presha akivila huchangia kupandisha presha ni mayai na nyama, hasa ile itokanyo na ng’ombe, mbuzi, nguruwe na nyingine za jamii hiyo.
Itaendelea wiki ijayo

1 comment:

Anonymous said...

HEBU TUPE HINTS NA KWA UPANDE WA LOW PRESSURE MAANA NAONA HIYO HUWA HAWAITAJI TAJI WAKATI INATUPELEKESHA SISI WENGINE BALAA