Tuesday, September 21, 2010

PRESHA: Muuaji tunayelala na kutembea naye-2



WIKI iliyopita tuliangalia jinsi ambavyo ugonjwa wa presha ulivyo hatari na kuzungumzia dalili ambazo mtu mwenye ugonjwa huo anaweza kuwa nazo. Wiki hii tuangalie vyakula ambavyo mgonjwa wa presha au asiyekuwa na presha anatakiwa kuvila ili kuudhibiti au kujiepusha na ugonjwa huo. Endelea...

ZINGATIA VYAKULA HIVI
Ukisha kuwa mgonjwa wa presha, ulaji wa vyakula vitokanavyo na nafaka halisi, matunda na mboga za majani, linakuwa suala la lazima na siyo hiyari. Mgonjwa wa presha anashauriwa kula zaidi vyakula hivyo na kupunguza ulaji wa vyakula vyenye protini nyingi, ikiwemo nyama kama ilivyoolezwa awali.

Katika orodha ndefu ya matunda anayopaswa mgonjwa kula na kupata nafuu, ni pamoja na hii ifuatayo, ambayo huweza kutumika pia kama tiba, kwani matunda haya yameonekana kuwa na virutubisho vingi zaidi vinavyoweza kudhibiti presha:

Vitunguu saumu
Kula vitunguu saumu kwa wingi, hutoa nafuu kubwa kwa mgonjwa. Unaweza kula punje mbili hadi tatu kwa siku na kuchanganya kwenye mboga pia.

Limau
Pia penda kula limau mara kwa mara, nalo ni miongoni mwa matunda yanayotoa nafuu kwa mgonjwa wa presha. Limau lina Vitamin P ambayo utaipata kwa kunywa juisi yake au nyama na maganda yake.

Zabibu mbivu
Zabibu nazo zimeorodheshwa miongoni mwa matunda anayotakiwa kula mgonjwa wa presha ili kupata nafuu, nayo yana vitamin P ambayo huzuia kuziba kwa mishipa ya damu.

Tikiti maji
Tikitimaji nalo ni miongoni mwa matunda anayopaswa kula mgonjwa wa presha. Halikadhalika, mbegu za tikiti maji zinaweza kutengenezwa na kuliwa kama dawa inayoweza kumpa nafuu kubwa mgonjwa. Kausha mbegu zake, kisha zikaange, ziliwe mara kwa mara kama karanga.

Mchele
Mchele una kiwango kidogo cha ‘fat’ na pia una kiwango kidogo cha ‘kolestrol’, hivyo kukifanya kuwa chakula bora kwa mgonjwa wa presha. Hivyo wali ni sawa kuliwa na mgonjwa wa presha, hasa ukipata ule mchele usioondolewa virutubisho vyake (brown rice).

Viazi vitamu
Viazi vitamu, hasa vile vya kupika na maganda yake, vinafaa sana kuliwa na mgonjwa wa presha. Viazi vitamu vina madini mengi ya ‘potasiamu’ na havina madini chumvi.

Juisi ya mboga majani
Ulaji wa mchanganyiko wa juisi ya mboga, hasa karoti na mchicha (spinach) ni nzuri sana kwa mgonjwa wa presha, huweza kutumika pia kama tiba. Kunywa glas moja kutwa mara mbili au tatu.

Kwa kuzingatia ulaji wa vyakula vilivyoanishwa hapo juu na kufanya mazoezi mara kwa mara, mgonjwa wa presha anaweza asisumbuliwe kabisa na tatizo hilo na kujihisi kupona hata bila kutumia dawa. Hata hivyo, hilo linawezekana tu iwapo utajitambua mapema na kuanza kuchukua hatua za ulaji sahihi wa vyakula sasa na siyo baadaye!

MWISHO.


1 comment:

Disminder orig baby said...

Lol nilipitwa kidogo, lakini sasa nimepata asante kaka