Friday, October 15, 2010

IJUMAA SHOWBIZ!

Yatima wa roho: Muvi ya Kibongo itakayotikisa EFF
Pazia la tamasha kubwa la filamu lijulikanalo kama European Film Festival EFF limefunguliwa rasmi jana ndani ya Ukumbi wa New World Cinema Mwenge, jijini Dar es Salaam, Hemed Kisanda anashuka nayo.

Katika ufunguzi huo mashabiki lukuki walijitokeza kushuhudia filamu zenye mafunzo na utamaduni kutoka nchi za Ulaya, tayari kwa kutoa mwelekeo kwa wadau wa tasnia hiyo hapa nchini ili waweze kujua njia sahihi za kukukuza filamu za hapa nyumbani.

Katika maonesho hayo yatakayoendelea kwa majuma matatu ndani ya ukumbi huo na baadaye kuhamia Arusha kwa wiki moja, mataifa zaidi ya 15 kutoka Jumuiya ya Ulaya ‘EU’ yanatarajiwa kuleta filamu zao.

Tanzania ikiwa nchi mwenyeji wa tamasha hilo inatarajia kuingiza filamu zake tatu katika maonesho hayo ambazo ni Vita, Unsung Heroines inayohusu maisha na historia ya Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha Rose Migiro na nyingine ikiwa ni Yatima wa Roho.

Akiisifia sinema ya Yatima wa Roho Tayana Tibenda amesema ni filamu nzuri na yenye kusikitisha lakini inakuacha na mafunzo kibao pindi unapomaliza kuitizama kwani inaonesha watoto wadogo watano wakichukuliwa kama yatima ili kwenda kupewa makazi na chakula.

Akiendelea kusimulia kisa hicho, Tibenda amesema katika safari ya watoto hao wanakuwa na matumaini ya maisha mema kwa kila mmoja wao, lakini siku zilivyozidi kusonga mbele, ndoto hizo zikabadilika na kuwa machungu na mateso ya kukatisha tamaa. Amesema kwamba mahali ambapo palitakiwa kuwa eneo la usalama kwa watoto hao , panakuwa jela na kufanyishwa kazi ngumu.

“Hii ni simulizi nzuri kuhusu juhudi za yatima ambapo vijana watano walitoroka kutoka katika eneo hilo lililoonekana kuwa la usalama na kujikuta katika mitaa yenye “ukatili” wa kutisha hapa nchini Tanzania,” amesema .

Kwa mujibu wa msemaji huyo filamu hii imeongozwa na Barnaba Elias, Tatu Mzee, Mwinyi na Jasmine Nurdin na amemaliza kwa kuwataka wapenzi wa filamu kufuatilia ratiba za maonesho kwenye vyombo vya habari.
***********************************
Dj Snox wa Mabaga Fresh alivyomzika baba yake
Na Richard Bukos
Msanii wa muziki wa kizazi kipya anayeunda Kundi la Mabaga Fresh, Christoms Mwingira a.k.a DJ Snox juzi Jumatano, alijumuika na waombolezaji wengine katika shughuli ya mazishi ya baba yake mzazi, Fabian Mwingira.

Akizungumza na ShowBiz msibani hapo Snox alisema kuwa msiba huo ni pigo kubwa maishani mwake hasa baada ya kupoteza wazazi wake wote wawili kwani mama yake pia alifariki hivi karibuni.
**********************************
Ms. Triniti Kuipaisha Bongo Ulaya
Kupitia kwa wakali wawili wa muziki wa Bongo Fleva, Ambwene Yesaya ‘A.Y’ na Ilunga Khalifa ‘Cpwaa’ upo uwezekano mkubwa kwa mwanadada Ms. Triniti mwenye asili ya Trinidadi na Amerika kuipeperusha Bongo mbali zaidi, Jelard Lucas anashuka nayo.


Kauli hiyo ilithibishwa na A.Y alipokuwa akigonga ishu mbili tatu na ShowBiz juzi ambapo alisema kwamba, kolabo aliyofanya na staa huyo wa kimataifa huenda ikazaa matunda kwa wasanii wa Bongo kupata dili nyingi katika nchi za mbali.


“Nimefanya naye ngoma yenye jina la ‘Goog Look’ ambayo video yake tumepiga Uganda, naamini ataipeleka mbali zaidi na kutufanya Wabongo tutambulike kimataifa,” alisema Ambwene ambaye Jumapili wiki hii atawarusha mashabiki wake ndani ya Club Bilicanas.

Msanii mwingine aliyepiga kolabo na Ms. Triniti aliyekuja Bongo hivi karibuni kwa ajili ya shoo kadhaa ni ‘Cpwaa’.
******************************************
Top C: Amtupia Riyama pale kati
Top C
Riyama
Kutoka ndani ya lebo ya Shalobalo iliyomtoa ‘dogo’ Nassib Abdull ‘Diamond’ kuna ishu mpya imedondoka pande hizi ikichana kwamba, staa mpya wa lebo hiyo, Mohamed Zimbwe Kassim a.k.a Top C ambaye hivi sasa anasimamia miguu miwili ya ngoma yenye jina la ‘Anko’ amemtupia staa wa Bongo muvi, Riyama Ally kunano video ya ngoma hiyo.

Tofauti na mastaa wengine wa Bongo Fleva ambao kwenye video zao huwapa shavu mamisi na werembo, Top C yeye amesema kwamba alichoangalia ni kipaji cha mwanadada Riyama ambacho kilitakiwa zaidi kwenye video yake.

“Warembo wengine pia wamo kwenye video hiyo ambayo inaendelea kufanya vizuri, lakini nilihitaji kipaji cha kweli kutokana na stori yenyewe jinsi ilivyo kitu ambacho Riyama amekioneshea uhalisia. Baada ya kazi hiyo nimeachia ngoma nyijgine yenye jina la Haya iliyopigwa hapo hapo Shalobalo na Prodyuza Bob Junior,” alisema Top C.
compiled by mc george/ijumaa

No comments: