Tuesday, April 19, 2011

UMAARUFU; CHANZO CHA WASANII KUPATA VVU

Katikati ni Muelimishaji rika Taji Liundi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirikika la Utangazati la Taifa (TBC International) akitoa elimu kwa wasanii na wadau wa Sanaa juu ya VVU/UKIMWI wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).Kulia kwake ni Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego na Mratibu wa Jukwaa hilo Ruyembe C.Mulimba.

Taji Liundi akiwaonesha wadau wa Jukwaa la Sanaa moja ya wasanii aliyefariki Dunia kutokana na kupata maambukizi ya VVU/UKIMWI.Alitoa mifano ya wasanii mbalimbali waliokwisha fariki kutokana na ugonjwa huu.
Katibu Mtendaji wa BASATA,Bw.Materego akitoa wito kwa wasanii kushiriki katika kujikinga na VVU/UKIMWI kwenye Jukwaa la Sanaa linaloandaliwa na Baraza hilo kila Jumatatu kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Sanaa na Utamaduni (CAJAtz).Kushoto kwake ni Taji Liundi na Bw.Ruyembe.
Mdau wa Jukwaa la Sanaa akiuliza swali kuhusu VVU/UKIMWI.
Wadau wengi wa sanaa humiminika kwenye Jukwaa la Sanaa kupata elimu na changamoto mbalimbali kuhusu tasnia.Hapa wadau wakifuatilia somo la VVU/UKIMWI kwa umakini mkubwa.

Na Mwandishi Wetu
Wasanii wametajwa kuwa hatarini kuambukizwa virusi vya UKIMWI kutokana na umaarufu walionao na kujikuta wakishawishika kuingia katika vitendo mbalimbali vya hatari kwa afya zao hasa vya ngono.

Hayo yamesemwa wiki hii na Muelimisha rika Taji Liundi wakati akiwasilisha mada kuhusu Umuhimu wa Msanii Kutunza Afya Yake kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambapo alisema kwamba, umaarufu, ushawishi na kutojitambua miongoni mwao ndiyo chanzo kikubwa cha wao kuwa hatarini kupata maambukizi hayo.

“Kutojitambua, umaarufu na ushawishi mkubwa walionao wasanii katika jamii huwafanya wawe hatarini kuathiriwa na ugonjwa wa UKIMWI kwani hufuatwa na kundi la watu na mara nyingi kujikuta wakishawishiwa kufanya ngono katika mazingira yasiyo salama” alisema Taji Liundi ambaye ni Kamishna msataafu wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS).

Aliongeza kwamba,kada ya wasanii imekuwa ikiathiriwa na ugonjwa huu toka umegunduliwa kwani katika nchi zilizoendelea kumekuwa na taarifa za vifo vya wasanii wengi vinavyotokana na UKIMWI huku akiweka wazi kwamba kutumia vibaya umaarufu ambako kumekuwa kukichanganywa na matumizi ya vilevi ni sababu nyingine kuu.

Alizidi kueleza kwamba,uwepo wa tunzi za kimapenzi katika kazi za sanaa ni changamoto nyingine kwani imezifanya kazi za wasanii kuwa za kusisimua na kuamsha utendaji ngono miongoni mwa wanajamii na kuwaacha wao wakiwa waathirika wakubwa.

“Ukitazama nyimbo za wasanii wa kizazi kipya utaona ni zenye maudhui ya rika la adolescence (umri wa makumi),zimebeba ujumbe wenye kuhamasisha mapenzi na ngono na hapa ndipo tunapoona mabadiliko makubwa ya vijana wakihamasika kufanya yale wanayoyaona na kuyasikia kupitia vyombo vya habari” alisisitiza Taji.

Alimalizia kwa kuwaasa wasanii kujitambua, kujilinda na kuwajibika katika kupambana na VVU/UKIMWI huku akiwaeleza kwamba,umaarufu na ushawishi walionao huathiriana na jamii (Two way effects) hivyo hawana budi kuwa makini.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA,Ghonche Materego alisema kwamba, wasanii wamekuwa mstari wa mbele kutoa elimu dhidi ya UKIMWI kwa jamii na kujisahau wao binafsi kwamba wako katika mazingira hatari ya kupata maambukizi.

Alisema kwamba,BASATA katika mpango mkakati wake wa 2011-2014 itajikita katika kutoa elimu kwa wasanii na kuwapa ufahamu juu ya ugonjwa huu hatari ambao umekuwa ukiwaua wasanii mbalimbali duniani.

No comments: