atibu
Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego akionesha kitabu kilichoandaliwa
na Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, Martin
Mandalu kinachohusu Tasnia ya Muziki Mkombozi Kwa Vijana kwenye Jukwa la Sanaa wiki hii. Kulia ni mtunzi huyo, Bw. Mandalu.
Mdau
wa Jukwaa la Sanaa akitaka kupewa maeleza kuhusu utafiti huo ambapo
alitoa wito kwa watu wengine kujaribu kufanya utafiti ili kuja na
maboresho katika fani hiyo. Na Mwandishi Wetu
Utafiti
uliofanywa kwenye muziki wa kizazi kipya ukilenga kubaini changamoto na
mafanikio yake umebainisha kuwa, kukosekana kwa umoja miongoni mwa
Wasanii ni moja ya sababu kubwa ya kudumaa kwa maendeleo yao.
Sababu
zingine zilizotajwa ni pamoja na Wasanii kutokuzingatia mikataba kwenye
kazi zao, utengenezaji wa kazi za sanaa zenye ubora hafifu, usimamizi
dhaifu wa kazi zao, kukosekana kwa viongozi thabiti katika tasnia ya
muziki na sababu zingine.
Akiwasilisha
utafiti wake alioukamilisha Mwaka huu kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) mapema wiki hii , Mhadhiri Msaidizi wa Chuo
Kikuu cha Mtakatifu Agostino, Martin Mandalu alisema kuwa, bila wasanii
kuzifanyia kazi changamoto hizo bado kutakuwa na safari ndefu katika
kuyafikia mafanikio ya kweli.
“Asilimia
80 ya Wasanii waliohojiwa kwenye utafiti huu hawakuwa na taarifa ya
uwepo wa umoja unaowaunganisha. Hii ni hatari kwa sababu nilipofika
katika vyombo rasmi nilipata taarifa za uwepo wa vyama na mashirikisho
ya wasanii. Hii ina maana wasanii hawatambui uwepo wa umoja huo” alisema
Mandalu.
Kwa
mujibu wa utafiti huo, Wasanii wengi waliohojiwa walikiri kuwa,
wamekuwa wakipata mapato kidogo ikilinganishwa na kazi wanazofanya
lakini hili likielezwa kuwa linasababishwa na kutozingatia mikataba,
kukosekana kwa ushirikiano miongoni mwao na Wasani kutaka kufanya kila
kitu yaani utunzi wa nyimbo, usambazaji na hata umeneja.
“Wasanii
wengi waliohojiwa walionekana kukosa uongozi na usimamizi thabiti.
Walionekana kufanya kila kitu kuanzia utunzi wa nyimbo, kuzifanyia
matangazao, kutafuta kazi za maonyesho na umeneja kwa ujumla”
alisisitiza Mandalu wakati akifafanua utafiti wake.
Kuhusu
utayari wa Wasanii kutoa taarifa au kufika maeneo wanayohitajika,
Mhadhiri huyo msaidizi alisema kuwa, ni tatizo kubwa kwani wasanii wengi
wamekuwa wazito katika hilo na hata kutokutoa ushirikiano wa kutosha katika masuala yanayowahusu.
“Wengi
wa wasanii niliokuwa napanga kukutana nao, walikuwa hawaoneshi
ushirikiano. Anaweza kukwambia tukutane saa tano lakini ukifika muda huo
anakwambia ana kazi nyingine kwa hiyo haitawezekana” alisema Mhadhiri
huyo wakati akieleza changamoto alizokumbana nazo.
Utafiti huo ambao umechapishwa kwenye Kitabu cha Tasnia ya Muziki Mkombozi kwa Vijana umefanywa na Mhadhiri huyo kama sehemu ya kupata shahada yake ya uzamili katika stadi za Maendeleo.
No comments:
Post a Comment