Punguza Matumizi ya Posho SIYO Matumizi ya Reli, Barabara, Elimu na Afya
Mwezi Disemba mwaka 2011 Waziri wa Fedha
na Uchumi alimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha Duniani
(IMF) kumwahidi mambo yepi Serikali ya Tanzania itafanya ili
kurekebisha Bajeti yake. Utaratibu huu hufanyika kila mwaka kupitia
mpango unaoitwa ‘Policy Support Instrument (PSI). Katika barua hiyo
Waziri wa Fedha wa Tanzania ameahidi kwamba Serikali itafanya juhudi
kupunguza matumizi ili kuweza kupunguza uwiano wa nakisi ya Bajeti na
Pato la Taifa (fiscal deficit to GDP ratio) kutoka asilimia 7.2
mpaka asilimia 6.6 ya Pato la Taifa.
Waziri wa Fedha na Uchumi ameiambia IMF
kwamba ifikapo mwisho wa Mwezi Disemba mwaka 2011 (wiki mbili
zilizopita) Baraza la Mawaziri la Tanzania limefikia maamuzi
ya kupunguza nakisi ya Bajeti kwa kiwango kilichotajwa. Maeneo
yanayotajwa ni Pamoja na Miradi ya Maendeleo ambapo jumla ya miradi
yenye thamani ya Tshs 157bn itakatwa. Waziri
wa Fedha ametaja miradi hiyo katika Ukarabati na Ujenzi wa Miundombinu.
wa Fedha ametaja miradi hiyo katika Ukarabati na Ujenzi wa Miundombinu.
Kambi ya Upinzani Bungeni inapinga
kuondolewa kwa miradi ya maendeleo ili kupunguza matumizi ya Serikali.
Kimsingi wakati kama huu ambapo hali ya uchumi ni mbaya na vijana wengi
vijijini na mijini hawana ajira tunasisitiza umuhimu wa kutumia zaidi
kwenye miradi ya maendeleo.
Punguza matumizi ya kawaida
Kambi ya Upinzani Bungeni inarejea wito
wake kwa Serikali kupunguza matumizi ya kawaida ili kupata fedha za
kutosha kwa ajili ya maendeleo. Haiwezekani kamwe tukawa Taifa huru
iwapo miradi yetu yote ya maendeleo inafadhiliwa na wahisani. Kiwango
kidogo tulichokiweka katika Bajeti ya mwaka huu ndicho hicho sasa
kinakatwa na hivyo miradi yote ya maendeleo kubakia kwa wahisani ama kwa
mikopo au misaada. Kiwango cha Tshs 203bn sawa na 0.5% ya Pato la Taifa
ambacho Serikali imeahidi kupunguza ni kidogo mno na kinalenga kuumiza
watumishi wa kada ya chini ya Serikali na sio viongozi wakubwa. Bajeti
ya Mafunzo inayoenda kukatwa itaumiza Manesi na Walimu au watumishi
wanaoongeza ujuzi ili kuboresha kazi zao. Serikali ikate matumizi yote
yasiyo ya lazima na hasa posho (360bn), ipunguze matumizi ya magari na
yale yasiyo na uhitaji yapigwe mnada na viongozi wote isipokuwa Rais,
Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika na Jaji Mkuu washushwe madaraja ya
kusafiria kwenye ndege. Safari zote ambazo hazina mahusiano na miradi ya
maendeleo zipigwe marufuku kwa muda wote wa miezi sita ya Bajeti
iliyobakia.
Serikali ihakikishe matumizi katika Sekta
ya Elimu na Afya hayakatwi kabisa ili kuhakikisha tunalinda mafanikio
kiduchu ya upanuzi wa sekta hizi na kuongeza uwezo wa Serikali
kutoa huduma bora kwa wananchi hasa wa vijijini.
Matumizi ya Maendeleo yasiguswe, yaongezwe
Tayari imeonekana kwamba katika kipindi
chote cha nusu ya Bajeti Halmashauri za Wilaya hazijapata fedha za
maendeleo. Mfano Halmashauri ya Wilaya Kigoma imepata asilimia 0.3 tu ya
Bajeti ya Maendeleo ilhali Halmashauri ya Mji wa Mpanda imepata
asilimia 4 tu. Ni dhahiri miradi ya maendeleo kwa maeneo mengi ya
vijijini itakwama kwani ni wazi kabisa kwamba Halmashauri hazipati fedha
zote za Bajeti ya Maendeleo. Serikali itambue kwamba miradi ya
maendeleo sio anasa bali ndio vyanzo vya baadaye vya mapato ya serikali.
Miradi ya maendeleo hutoa ajira kwa wananchi na hivyo kuwapunguzia
umasikini wa kipato. Jumla ya Tshs 157bn zinazotakiwa kukatwa zisikatwe
bali ziongezwe ili kupata fedha za kurekebisha miundombinu kama Reli ya
Kati.Kwa mfano Reli ya Kati inahitaji Tshs 200bn katika kipindi cha
miaka 3 ili iweze kusafirisha mizigo tani 1.5m kwa mwaka kila siku na
kuzalisha faida.
Ongeza Mapato ya Ndani
Inashangaza kwamba katika mpango wa
Serikali kupunguza nakisi ya Bajeti mkazo umewekwa kwenye kuondoa miradi
ya maendeleo badala ya kuongeza mapato. Nakisi hupunguzwa ama kwa
kupunguza matumizi au kwa kuongeza Mapato. Serikali katika Taarifa yake
kwa IMF imeibua njia moja tu ya kuongeza mapato, kodi ya mapato kutoka
Kampuni ya Geita Goldmine. Huu ni uvivu wa kufikiri.
Serikali imeambiwa mara kadhaa suala la
kuanza kutumika kwa sheria mpya ya madini kwa Kampuni za Madini
zilizokuwapo. Makusanyo ya Mrahaba peke yake kwa sheria mpya, kiwango
kipya na kanuni mpya ya kukokotoa ingeongeza mrahaba mpaka Tshs
203bn kutoka Tshs 99bn za sasa. Kwanini Serikali ianvuta miguu katika
kutekeleza hili? Waziri wa Nishati na Madini aliahidi Bungeni kwamba
mazungumzo na Kampuni za Madini yanaisha Mwezi Septemba. Mbona Serikali
imekuwa BUBU katika hili?
Serikali iliahidi kuangalia suala la
mauzo ya mali za makampuni zilizoko Tanzania na kodi ambayo tunapaswa
kukusanya, Serikali imekuwa kimya kabisa katika suala hili.
Marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa kuondoa
msamaha kwenye ‘deemed capital goods yangeongeza mapato ya Serikali kwa
kiwango kikubwa na kupunguza mzigo wa
misamaha ya Kodi.
misamaha ya Kodi.
Uwajibikaji kwa Bunge
Inashangaza zaidi kwamba sasa imekuwa ni
mtindo kwa Serikali kutoa ‘commitments’ muhimu za kibajeti kwa Shirika
la IMF badala ya wananchi kupitia Bunge. Bunge limepitisha Bajeti,
mapitio yeyote ya Bajeti yanapaswa kuidhinishwa na Bunge. Bila kufanya
hivyo maana ya Bunge kupitisha Bajeti inakuwa haina mantiki na uhuru wa
Taifa letu unakuwa haupo kwetu.
Umuhimu wa Bunge kutunga haraka Sheria ya
Ofisi ya Bajeti ya Bunge (Parliamentary Budget Act) sasa unaonekana
waziwazi. Muswada umewasilishwa Bungeni na Wabunge binafsi kutaka
kuundwa kwa mfumo wa kuisimamia Serikali katika Bajeti. Ofisi ya Spika
wa Bunge ihakikishe muswada huu unachapishwa katika Gazeti la Serikali
mara moja ili usomwe kwa mara ya kwanza katika mkutano wa Sita wa Bunge
na kutungwa kuwa sheria katika mkutano wa Saba.
Kambi ya Upinzani inaitaka Serikali ilete
mpango wa kupunguza matumizi Bungeni ili ujadiliwe na kuidhinishwa na
Bunge kabla ya kuanza kutumika. Vinginevyo Mpango wa Serikali kwa IMF
utakuwa ni kudharau wananchi na kuuza uhuru wetu kwa Shirika la Fedha
la Kimataifa. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema mwishoni mwa miaka ya
Sabini ‘toka lini Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limekuwa Wizara ya
Fedha ya Kimataifa (International Ministry of Finance)?’
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Waziri Kivuli Fedha na Uchumi
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni (NKUB)
Dar es Salaam, 10 Januari 2012.
No comments:
Post a Comment