Ndugu zangu,
IJUMAA
alfajiri ya Septemba 7 niliondoka nyumbani Iringa kuelekea Njombe
kikazi. Jana yake, alhamisi usiku, Mwandishi Gershom Malegesi wa Redio
Ebony FM alinipigia simu kuniomba nishiriki kwa simu kwenye kipindi
chake maarufu cha ' Morning Talk'.
Nikamjibu,
kuwa kwa vile nina safari ya Njombe, basi, nikifika kijijini Nyololo,
Mufindi, nitasimama na kuongea na wakazi wawili watatu waniambie
wanachofikiri juu ya kilichotokea. Kisha Maregesi aniunganishe kwa simu
nikiwa hapo Nyololo tuongee redioni. Tukakubaliana.
Baada
ya kutoka Mafinga na kuumaliza msitu wa Sao Hill, nilianza kuiona
Nyololo kutoka mlimani. Nilipaki gari yangu takribani nusu kilomita
kabla ya kuingia kijijini Nyololo. Nikaanza kutembea kwa miguu kuelekea
kijijini bila kushika kamera wala mkoba.
Sweta
nililovaa siku hiyo la rangi ya zambarau huenda lilinifanya nionekane
kama ' wapasua mbao' wengine! Ilinisaidia, maana, kwenye meza ya kwanza
ya biashara pale kijijini, niliwakuta akina mama watatu wakisikiliza
kwa makini ' Morning Talk' ya Ebony FM. Kulikuwa na watu waliokuwa
Nyololo siku ya tukio wakitoa ushuhuda wao studioni.
Nilimwandikia
meseji mtangazaji Malegesi kuwa angeweza kuniunganisha hewani kwa
wakati huo. " Kaka, nimeshafika Nyololo!" Nilimwandikia. Naye akanijibu;
" Kuna jamaa wanatoa ushuhuda wao studioni, nitakuunganisha baada ya
dakika 15".
Taratibu
nami nikajivuta karibu zaidi kwenye meza ile ya biashara ya mboga mboga
iliyozungukwa na akina mama waliokuwa wakifuatilia kinachosemwa kuhusu
kilichotokea mahali ambapo wao ndipo walipo kwa wakati huo.
" Kamwene!"- Niliwasalimia kwa Kihehe. Kisha nikajiunga kwenye kusikiliza ' Morning Talk'.
Niliwasikiliza
akina mama wale wakijadiliana pia katika baadhi ya waliyokuwa
wakiyasikia. Niliwaona wakitingisha vichwa kukubali baadhi ya
yaliyokuwa yakisemwa na mashuhuda. Niliwaona pia wakitingisha vichwa
kuyakataa baadhi ya yaliyokuwa yakisemwa na mashuhuda.
Nikavuta pumzi, kisha nikawauliza; " Mwenzenu napita njia tu, hivi siku ile ya Jumapili ilikuwaje na mlijisikiaje?"
Nikawaona
walivyo na hamu ya kumsimulia ambaye hakuwepo. Nikawasikiliza. Mmoja
anasema; hakuwahi hata siku moja kusikia mlio wa bomu. Ilkuwa ni mara
yake ya kwanza. Mwingine akaniambia; " Yaani , mimi , niloposikia mabomu
tu, nikajifungia ndani na kulala!". Naam, huyu aliugeuza mchana kuwa
usiku.
Akina
mama wale wanasema, kuwa usiku ule wa Jumapili walikosa hata hamu ya
kula chakula. Hawakula chakula. Walilala kwa mashaka pia.
Kando
ya meza ile nikawaona watoto wakisogelea na kusikiliza mazungumzo.
Nilizioona sura za watoto wenye hofu. Msichana wa miaka 13 akasimulia
jinsi alivyokimbilia porini kuhofia maisha yake.
Ndio, kuna watoto wengi wa Nyololo leo ambao wangehitaji msaada wa kisaikolojia kuelewa kilichotokea na kuwapunguzia hofu yao.
Nikiwa
nimesimama pale kwenye meza ya biashara nikaisikia simu yangu ikiita.
Ni Mtangazaji Gershom Malegesi wa Ebony FM aliyekuwa tayari
kuniunganisha na studio. Lakini, kwa nilichokuwa nikikiona na kukisikia
pale kutoka kwa wakazi wenyewe wa Nyololo, nikashindwa kuijibu simu ya
Malegesi. Sikutaka tena kuunganishwa hewani. Nilihitaji muda wa
kutafakari.
Hakika,
niliyoyaona kutoka kwa wakazi wa Kijijini Nyololo ni pamoja na hofu,
mashaka, hasira na zaidi maswali ya ' Kwa nini?". Kuna wanaojisikia
vibaya sana kuona tukio lile baya limetokea kijijini kwao. Kuna
wanaojisikia kukatishwa tamaa na mambo ya siasa. Kuwa ambao hawaipendi siasa
kwa sasa. Kuna wanaojisikia aibu kuwa Kijiji chao kimejulikana sasa kwa
sifa mbaya ya mauaji. Kuna wanajisikia kuwa watu wa kutoka nje wamekuja
na kufanya mambo mabaya kijijini kwao.
Nilizunguka
kwa miguu kwenye mitaa ya kijiji cha Nyololo. Niliziona teksi mbili
tatu kuu kuu ambazo hufanya safari za kutoka barabara kuu hadi vijiji
vya ndani. Kuna ambao siku ya tukio gari zao zilikodishwa kuwakimbiza
majeruhi au waliotaka kuikimbia Nyololo kwa haraka.
Ndio,
niliwaona vijana wale wa Nyololo, wa kike na wa kiume, ambao kwa
kawaida ukipita Nyololo huonekana kuchangamka sana, lakini, Ijumaa ile
niliyopita Nyololo niliwaona wakiwa kama ' Kuku waliomwagiwa' maji.
Wengi hawakuchangamka.
Hata kwenye sura za baadhi yao unaweza kuona, kuwa kuna jambo kubwa limewatokea na wako kwenye kutafakari na labda hofu pia. Maana, redio, runinga na magazeti bado yanazungumzia kilichowatokea.
Hata kwenye sura za baadhi yao unaweza kuona, kuwa kuna jambo kubwa limewatokea na wako kwenye kutafakari na labda hofu pia. Maana, redio, runinga na magazeti bado yanazungumzia kilichowatokea.
Na
kikubwa nilichokiona ni kuwa; wakazi wa kijijini Nyololo wana ukweli
ambao huenda wengine hawaufahamu. Ni wajibu wa wote wenye jukumu la
kuusaka ukweli mzima wa kilichotokea kuwasikiliza wakazi wa Nyololo pia.
Na
bila shaka, kama Taifa, Nyololo inaweza kutusaidia kufungua ukurasa
mpya wa namna iliyo bora na salama ya kwenda mbele kama ndugu wa Taifa
moja. Kwamba kilichotokea Nyololo kisitokee tena.
Maggid,
No comments:
Post a Comment