Friday, October 30, 2015

Uchambuzi: Zanzibar Inaumiza Kichwa..

Ndugu zangu,
MFALME Suleiman aliambiwa ndotoni aombe kitu chochote kwa Mola wake, naye akajibu; " Ewe Mola wangu, nipe mimi mtumwa wako moyo wa adili ili niwahukumu watu wako, na kupambanua mema na mabaya, maana ni nani awezaye kuwahukumu hawa watu wako walio wengi?"
Hivyo basi, Mfalme Suleiman aliichagua hekima.
Maana, ni Mfalme Suleiman huyo anayekaririwa na vitabu vya dini akitamka, kuwa; " Watu wangu wanaangamia kwa kukosa hekima".
Naam, hekima ndilo jambo lililo bora kabisa kwa mwanadamu kuwa nalo. Mwanadamu aliyepungukiwa hekima ana hasara kubwa maishani. Hekima ni tunu na kipaji ambacho Mwenyezi Mungu amewajalia waja wake, ili nao waweze kupambanua na kuamua kati ya yalo mema na maovu. Duniani hakuna shule ya kujifunza hekima.
Matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar yamefutwa, lakini, visiwani kunafukuta sasa siasa za chuki baina ya wenye kukinzana. Ndio, hali ya hewa ya kisiasa kule Zanzibar inaelekea kuchafuka.
Ni hali inayotutaka wenye kufuatilia mambo kurejea pia kwenye maandiko. Kwenye historia.
Uzoefu unatuambia, kuwa Bara kukitulia na Unguja kunatulia, na Unguja nako kukitulia bara nako kunatulia.
Maana, moto ukiwaka Zanzibar ni wa kwetu pia, Na hekima inatuongoza katika kutambua, kuwa ukiupuuzia moto unaowaka kwenye nyumba ya jirani yako, basi, nyumba yako pia imo hatarini kuungua . Na ndio mantiki ya kusema; Jambo la Zanzibar ni letu Bara.
Siasa za visiwani zina tofauti kubwa na bara. Kwenye kupigania uhuru wa Zanzibar kulikuwa na ASP iliyotokana na African Association na Shiraz Association. Kukawa na ZNP na ZPPP kwa maana ya Zanzibar Nationalist Party na Zanzibar And Pemba Peoples Party. Kulikuwa na itikadi na mitazamo ya kirangi pia. Umma Party ilitokana na ZNP na ZPPP. Unguja ndiko ASP ilipokuwa na mizizi na kukubalika zaidi, ZNP na ZPPP ilipata kukubalika zaidi Pemba.
Ali Muhsin wa ZNP aliyekuwa kiongozi mkuu Zanzibar ilipopata uhuru mwaka 1963 alionekana kuwa ni kibaraka. Mapinduzi ya Januari 12 1964 yaliongozwa na ASP. January 20 kukawa na army mutiny bara. Ulikuwa ni wakati mgumu kwa Julius Nyerere wakati Karume pia alimfukuza Balozi mdogo wa Marekani Carlucci kwa tuhuma za ujasusi.
1985 Julius Nyerere alikutana na upinzani mkubwa wa wahafidhina wa Zanzibar alipojaribu kulipenyeza jina la Salim Ahmed Salim kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano. Abdulahman Babu na Salim Ahmed Salim wamepata kuwa wafuasi wa Umma Party kilichokuwa na mwelekeo wa Kikomunisti na kilichotoana na ZNP na ZPPP. Hoja ya U-Hizbu inachipukia hapo.
Zanzibar inaumiza kichwa, na katika mazingira ya sasa, hekima inatuelekeza kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ndio suluhu ya mgogoro wa kisiasa Visiwani. Vinginevyo, kuna hatari ya visiwa kuyumba na hata vikazama na roho za watu.
Maggid,
Iringa.

No comments: