Sunday, November 1, 2015

Neno La Leo: Rasilimali Akili..

Ndugu zangu,
Tumepokea habari za matokeo ya ufaulu kwa Darasa la Saba. Na hakika, Maendeleo yetu kama taifa hayatawezekana bila uwepo wa maendeleo kwenye elimu. Nchi inahitaji watu wenye akili. Na akili ndio rasilimali muhimu nchi inahitaji kuwekeza kwa watu wake.
Dunia nzima watu wamekubaliana juu ya umuhimu wa elimu. Elimu ina
manufaa kwa jamii, inachangia kuinua uchumi.
Hata kwa mtu mmoja mmoja, mwenye akili ya elimu ya darasani na uzoefu wa maisha ana nafasi nzuri ya kupata ajira, kujiongezea kipato. Kuridhika na kazi yake, hata kufurahia muda wake wa mapumziko. Ni mwenye kuwa nafasi zaidi ya kuwa na siha ( afya) njema. Ni nadra akawa mhalifu, ni mwenye kuwa na moyo wa kujitolea.
La mwisho ni lenye kuhusiana na zoezi tulilolimaliza juzi tu, mwenye akili ya elimu ya darasani na uzoefu wa maisha, ni mtu mwenye kujitambua, kujiamini na kuthubutu. Ni mtu ambaye, zoezi la kushiriki kupiga kura, kwake atalichukulia kuwa ni wajibu wake wa kikatiba na kizalendo kwa nchi yake, bila sababu za msingi, mtu huyo hawezi, ' kutoroka' zoezi la kupiga kura.
Hivyo, tuwekeze kwenye akili za watu wetu. Ndio, rasilimali akili.
Ni Neno La Leo.
 ( Pichani nilipoalikwa kama mgeni rasmi. Mwanafunzi wa darasa la saba, Lucy Boaz, akinisomea risala ya wanafunzi waliohitimu darasa la saba shule ya msingi Ibigi, Katumba, Tukuyu Mbeya, mwezi uliopita.)
Maggid,
Iringa.

No comments: