Thursday, July 26, 2007

MAMBO YA USWAHILINI!!


Na Dotto Mwaibale
Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Rose Elias, alifumwa usiku wa manane katika nyumba ya mkazi mmoja wa Kigamboni jijini Dar es Salaam (jina linahifadhiwa) akiwa uchi wa mnyama hali iliyowashangaza watu walioshuhudia tukio hilo.

Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa, mwanamke huyo aliyekadiriwa kuwa na kati ya miaka 38-44 alifumwa usiku wa Julai 21, mwaka huu akiwa katika hali hiyo, jambo lililohusishwa na imani za kishirikina.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi, mmiliki wa nyumba aliyofumwa mwanamke huyo alisema kuwa, tukio hilo limeishtua sana familia yake pamoja na majirani zake.

"Mbwa ndio walionishtua, nikaamua kutoka nje na panga ili kuangalia kuna nini, lakini nikashangaa kuona kivuli cha mtu, niliposogea karibu zaidi nikamuona mwanamke akiwa uchi wa mnyama amesimama barazani kwangu," alisema.

Aidha aliongeza kuwa baada ya kumfuma mama huyo alimweka chini ya ulinzi na kumhoji sababu za kuwa barazani kwake usiku wa manane tena akiwa uchi, ambapo alijibiwa kuwa alitelekezwa na wenzake 32 aliokuwa nao safarini kutoka Dodoma.

"Sikuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kuwaamsha wanangu na mke wangu ambapo pia niliwaamsha majirani zangu na kwenda kwa mjumbe kutoa taarifa," alisema.

Alisema kuwa baada ya mjumbe kufika eneo la tukio, waliendelea kumhoji mpaka kulipopambazuka ambapo walitoa taarifa polisi na baada ya muda mfupi walifika nyumbani kwake.

Habari zaidi zinaeleza kuwa, baada ya maaskari kufika walimchukua mama huyo pamoja na mwenye nyumba na kwenda nao kituoni, lakini baadaye walijitokeza ndugu zake wakidai alikuwa mgonjwa.

"Nilishangaa sana walipokuja ndugu zake wakidai eti ndugu yao ni mgonjwa na siku moja kabla ya tukio walimpa nauli ili aende nyumbani kwao Kimbiji mkoani Pwani kwa ajili ya matibabu," alisema.

Hata hivyo, mashuhuda wa tukio hilo walilihusisha na imani za kishirikina hasa baada ya mama huyo kutamka wazi kuwa alitelekezwa na wenzake 32 aliokuwa nao safarini kutoka Dodoma, bila kufafanua aina ya usafiri uliotumika.

Hadi tunaingia mitamboni, jitihada za kumpata mjumbe wa nyumba kumi, ili azungumzie sakata hilo hazikuzaa matunda.


Jack Pemba amtema mkewe!
Na Issa Mnally
Mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, Jack Pemba amedaiwa kugombana na mkewe Aunt Ezekiel, kisha kuachana naye jumla. Ijumaa limeelezwa.

Habari kutoka katika chanzo chetu (jina linahifadhiwa) zinasema kuwa, ugomvi wao ulisababishwa na mke wa kigogo huyo wa soka, Aunt Ezekiel kuwa na wivu na mumewe kupita kiasi.

Aidha imeelezwa kwamba, Aunt alikuwa na tabia ya kumjia juu mumewe kila alipochelewa kurejea nyumbani kwa madai kuwa alitoka kwa hawara zake.

"Unajua, Aunt alizidisha wivu kwa mumewe, kila Jack alipochelewa kurudi nyumbani akitokea kazini au katika shughuli zake alikuwa akimjia juu kama mtoto mdogo, huo ndio mwanzo wa mgogoro wao," kilieleza chanzo hicho.

Aliongeza kuwa, kufuatia tabia hiyo ya mkewe, nyumba yao ilitawaliwa na ugomvi wa mara kwa mara jambo ambalo halikumfurahisha Jack na kuamua kumtwanga talaka mkewe ili kukwepa adha hiyo.
"Siku nyingine nilikuwa nawaamulia ugomvi wao, kwani kila Jack akichelewa kurudi nyumbani basi ujue siku hiyo hapakaliki ni kutwangana kwa kwenda mbele," alisema mpashaji wetu.
Akizungumzia madai hayo, Jack Pemba alisema hakuna kitu cha ajabu katika hilo, ingawa hakutaka kuzungumzia sakata hilo kwa undani zaidi.

"Kwani kuna ajabu gani mtu kutengana na mkewe? Kwani mimi nitakuwa wa kwanza? Mbona Mandela aliachana na mkewe Winnie?" Alihoji na kukata simu.

Gazeti hili lilimtafuta Aunt Ezekiel kwa njia ya simu lakini simu yake haikupatikana.

2 comments:

Anonymous said...

Mbona haujatupa udaku wa wema?.

Anonymous said...

Bwana Mrisho unatupunja nyuzzzz za Wema Sepetu.Tafadhali Ustadh!