Wednesday, August 15, 2007

CHINJACHINJA


Na Richard Manyota
Mapambano makali kati ya Wananchi wenye hasira na majambazi yaliibuka hivi karibuni eneo la Tabata Matumbi, jijini Dar es Salaam, kiasi cha kuufanya usiku wa manane wa Agosti 10 mwaka huu kuwa wa chinja nikuchinje.

Tukio hilo la aina yake lilitokea baada ya wakazi wa eneo hilo kuchoshwa na oparesheni ya wizi na ujambazi iliyokuwa imetangazwa na kundi la vijana wasiojulikana.

Wakazi wa eneo hilo kwa nyakati tofauti waliliambia gazeti hili ambalo nalo lilituma kamera yake eneo la tukio kuwa, siku za hivi karibuni wananchi wa Tabata walikuwa wakiishi maisha ya hofu kufuatia matukio ya wizi na ujambazi.

Walisema baada ya kuchoshwa na vitendo hivyo, waliamua kukutana ili kujadili njia ya kukomesha wizi na ujambazi ambapo walikubaliana kuendesha msako mkali ulioambatana na ulinzi wa doria ya usiku.

“Baada ya kuona maisha yetu yako hatarini tuliamua kuwasaka wezi hawa, maana ilikuwa haipiti siku bila kusikia mtu kaibiwa, tulianza doria ya kulinda mitaa yetu hasa usiku wa manane.

“Leo hii tukiwa kwenye lindo zetu kundi la hao vijana wakiwa na zana za kukatia nyavu, kuvulia simu dirishani na silaha kadhaa kama mapanga na nondo tuliwabamba, tulipowasimamisha walianza kutushambulia, nasi tukaanza kupamabana nao.

“Tuliwashinda nguvu, wengine walikimbia hawa wawili tuliwanasa wakiwa na zana hizi, wananchi walipokuja wakaanza kuwapiga,” alisema Saidi Amir mkazi wa eneo hilo huku akimwonesha mwandishi zana na majambazi hayo yakiwa hoi.

Aidha katika harakati za kuwanasa wengine zaidi mitaa ya eneo hilo ilifungwa na mayowe kutawala eneo la tukio huku taarifa za wahalifu hao zilipelekwa kituo cha polisi kupitia namba ya dharura ya 112 ambapo msaada wa askari ulitolewa.

Katika hali iliyoonekana kuwa kundi hilo la wezi lilikuwa limeamua kufanya uhalifu baadhi ya watuhumiwa hao walikuwa wamevaa nguo za kininja na magauni yaliyodaiwa kutumika kuwahadaa watu na kuficha silaha za kutumia katika ujambazi wao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Masindoki Masindoki alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo aliwasifu wananchi wa eneo hilo kwa ushirikiano wao na kuongeza kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea.


MTOTO ABAKWA

Na Waandishi Wetu.
Mtoto wa kike mwenye umri wa mika 17 anadaiwa kubakwa mara kadhaa na kijana Jabir Said mkazi wa Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam, na kupewa ujauzito.

Imedaiwa na chanzo chetu cha habari kuwa, binti huyo mdogo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili (jina lake na shule yake linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili) alirubuniwa kimapenzi na kijana huyo kiasi cha kushindwa kuhudhuria vyema masomo yake.

Kufuatia vitendo vya ubakaji wa mara kwa mara alivyokuwa akifanyiwa mtoto huyo, wasamaria wema walitoa taarifa hizo kituo cha polisi na kwa waandishi wa habari hizi ambapo mtego wa kuwanasa uliandaliwa.

Mwishoni mwa wiki iliyopita kijana huyo akiwa na binti huyo chumbani wakidaiwa kufanya mapenzi, walifumwa na askari polisi wa kituo cha Magomeni ambapo mtuhumiwa alitiwa mbaroni.

Mmoja wa wasamaria wema ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini alisema kuwa, wao kama wazazi na walezi hawakupendezwa na kitendo cha kijana huyo kumdanganya mwanafunzi ndiyo maana waliamua kutoa taarifa hizo polisi.

"Yaani nashangaa sisi wazazi tunajinyima ili watoto wetu wasome matokeo yake wanaishia kwa wanaume, hapana tuliona ni vema hatua zikachukuliwa ili liwe fundisho,” alisema msamaria huyo.

Katika hali nyingine ambayo Amani ilipata taarifa zake ni kwamba binti huyo mdogo baada ya kupelekwa kituoni hapo na baadaye kupelekwa hospitali kupimwa iligundulika kuwa, tayari alikuwa na ujauzito wa miezi miwili.

Naye Baba mlezi wa mwanafunzi huyo Bw.Mrisho Swedi akiongea na waandishi wetu alisema kwamba alikuwa akimuonya mara kwa mara binti yake huyo azingatie masomo na aachane na tabia mbaya lakini hakumsikia.

“Walimu wake walikuwa wakiniambia kuwa mahudhurio yake sio mazuri na kila siku walikuwa wakitoka shuleni saa 8.30 mchana, lakini alikuwa akifika nyumbani kuanzia saa 12 hadi saa 1 usiku, nikimuuliza ananijibu alikuwa tuisheni,” alisema Bw.Mrisho kwa masikitiko.

Gazeti hili linalaani vitendo vya ubakaji vinavyofanywa na baadhi ya wanaume, hasa kwa watoto wadogo ambao mara nyingi wamekuwa wakiumizwa na kuambukizwa magonjwa ya zinaa zikiwemo mimba za utotoni.

No comments: