Tuesday, August 28, 2007

HATARI!

Na Mwansishi wetu
Kitendo cha baadhi ya wabunge vijana katika Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania kulipua mabomu imeelezwa kuwa ni hatari kwa maisha yao.

Wakizungumza na mwandishi wetu wiki iliyopita kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi waliohojiwa jijini Dar es Salaam walisema kuwa asilimia kubwa ya vigogo wanaodaiwa kuhusika na kashfa mbalimbali mara nyingi hawapendi kutajwa majina yao, hivyo hujenga chuki kwa wale wabunge wanaowataja wakati wa kulipua mabomu.

Aidha Bw. Abdallah Juma mkazi wa Mikocheni alisema kuwa marehemu Amina Chifupa alipokuwa amelivalia njuga suala la dawa za kulevya bungeni kuwa kuna baadhi ya vigogo wanaohusika na biashara hiyo walimuona kama adui.

"Amina alifungua njia baada ya kuanza kufichua maovu mbele ya jamii yanayofanywa na watu wachache bila kujali maslahi ya Taifa lakini alipata vitisho baadaye alifariki dunia kwa kifo cha kutatanisha bila kuwataja vigogo hao hadharani ingawa alisema alikuwa na orodha ndefu ya wahusika," alisema Bw. Juma.

Aliendelea kusema kuwa Mhe. Zitto Kabwe ambaye alilitaka bunge liunde tume ya kuchunguza usainishwaji wa mkataba wa madini huko Uingereza uliofanywa na Waziri wa Nishati na Madini Bw. Nazir Karamagi alijikuta akifungiwa kwa kipindi cha miezi mitano kutojihusisha na shughuli za bunge hali iliyolalamikiwa na watu wengi.

Naye Mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini alisema kuwa sasa umefika wakati Bunge kusikiliza hoja na kuzifanyia kazi kwa maslahi ya taifa badala ya kuingiza itikadi za kisiasa.

Aliongeza kwa kusema kuwa endapo hoja za msingi zinazotolewa bungeni hazitaangaliwa kuwa ni mbunge wa chama gani katoa, nchi itapiga hatua kimaendeleo.

Akielezea sakata la Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Karamagi juu ya utiaji saini wa mkataba wa madini Uingereza, mhadhiri huyo alisema kunahitajika uchunguzi wa kina ambao utawatoa wananchi wasiwasi na kubaini nani ni mkweli kati yake na Mhe. Kabwe.

“Endapo madai ya Mhe. Kabwe yatafanyiwa kazi na kubainika kuwa yana ukweli basi Waziri Karamagi atakuwa mashakani kupoteza nafasi yake ya uongozi ingawa uamuzi wa mwisho juu ya suala hilo utakuwa mikononi mwa Rais Jakaya Kikwete" alisema mhadhiri huyo.

Mhadhiri huyo alisema kuwa siku hizi inaonekana kuwa ni jambo la hatari kwa waheshimiwa wabunge kutoa hoja nzito zinazohitaji ufafanuzi kwani wengi waliojaribu kufanya hivyo wamepata misukosuko na wengine hata kutishiwa maisha yao.

Wakati huo huo, marafiki na ndugu wa karibu wa Bw. Mohamedi Mpakanjia wamekuwa wakimuombea apone haraka ili arudi kushirikiana na jamii katika masuala ya maendeleo.

Aidha rafiki yake mkubwa, Kapteni John Komba alisema juzi kuwa kitendo cha mtu kuvumisha kuwa Mpakanjia amefariki kilisababisha mshituko mkubwa kwa watu mbalimbali bila sababu za msingi.

" Kitendo hicho si cha kiungwana na nashindwa kujua mtu huyo alikuwa na nia gani, imenisikitisha sana, napenda watu waelewe kuwa Medi hajafa na yupo Hospitali ya Lugalo akitibiwa. Ana matatizo ya kisaikolojia," alisema Komba.

Naye Dk. Maneno Tamba ambaye pia ni rafiki wa karibu wa Mpakanjia aliliambia gazeti hili juzi kwa njia ya simu kuwa mgonjwa anaendelea vizuri tofauti na mwanzo alipofikishwa hospitalini hapo.
(habari nyingine bonyeza hapa: http://www.globalpublisherstz.com/index.php)

No comments: