Tufaha(Apple): Tunda lingine lenye maajabu mwilini!
Tumerudi tena kwenye makala za uchambuzi wa faida za matunda mwilini na leo hii tunalichmbua tunda maarufu la Tufaha au wengi wanalijua kwa jina la epo (apple).Tunda hili ni miongoni mwa matunda ghali na kwa kawaida huingizwa nchini kwa wingi kutoka Afrika Kusini. Wastani wa bei ya tunda hili jijini Dar es salaam ni shilingi 400 kwa tunda moja sazi ya ngumi ya mtoto.
FAIDA ZA TUFAHA KIAFYA
Utafiti wa hivi karibuni kuhusu tunda hili, umethibitisha kuwa ule msemo wa kiingereza wa siku nyingi usemao An Apple A day keeps the doctor away (tunda moja kwa siku humuweka daktari mbali nawe) ni wa kweli kwani kuna virutubisho muhimu vya Fiber, Flavonoids, na Fructose-translate ambavyo hutuweka katika afya njema.
Kwa mujibu wa watafiti wa tunda hili, mtu akila shufaa moja na maganda yake anapata kiasi kisichopungua gramu 3 za kirutubisho aina ya fiber (ufumwele), kiasi ambacho ni kikubwa kwa asilimia 5 zaidi ya kile kinachopendekezwa na wataalamu mtu kula kwa siku. Na faida za kirutubisho hizi ni nyingi.
Baadhi ya faida kubwa na za msingi za kirutubisho hicho katika mwili wa binadamu, ni uwezo wake mkubwa wa kuteketeza kabisa kiasi cha mafuta mabaya mwilini (cholestrol levels), kuondoa hatari ya kuziba kwa mishipa ya damu, kupatwa na mshituko wa moyo na kiharusi.
Kwa maana nyingine ukiwa mlaji mzuri wa tunda hili, utajiepusha kwa kiwango kikubwa na matatizo ya shinikizo la damu au kupatwa na kiharusi (stroke), matatizo ya kiafya ambayo katika maisha ya siku hizi yamekuwa ni ya kawaida na watu wengine huyahusisha na imani za kishirikina.
Aidha epo linasifika kwa kuwa askari mzuri wa kupambana na matatizo ya tumbo, kama vile kujaa gesi, kuharisha, kukosa choo kwa muda mrefu na matatizo mengine kama hayo. Mtu mwenye matatizo hayo anapolila tunda hilo, basi hupata ahueni haraka na kama huna matatizo hayo, basi utakuwa unajitengenezea kinga madhubuti.
Utafiti mwingine kuhusu tunda hili, umeonesha kuwa epo linasaidia katika kuongeza kinga ya mwili na kinga dhidi ya saratani mbalimbali za mwilini kutokana na kuwa na kiwango kikubwa sana cha kirutubisho aina ya Flavonoids.
TUNDA ZURI KWA WAGONJWA WA KISUKARI
Epo lina kiasi fulani cha sukari ya asili, ambayo ni nzuri kwa watu wenye ungonjwa wa kisukari, kwani inapochanganyika na kirutubisho aina ya fiber husadia sana kuweka kiwango cha sukari mwilini katika hali inayotakiwa.
HUZUIA MAWE KWENYE FIGO
Kama unataka kupata kinga madhubuti dhidi ya ugonjwa wa mawe kweye figo (kidney stones), basi kunywa juisi ya epo. Utafiti uliochapishwa hivi karibuni kwenye jarida la masula ya lishe la Uingereza (British Journal of Nutrition), umeonesha kwamba, kwa kunywa nusu au lita moja ya juisi ya epo kila siku, unaondoa uwezekano kabisa wa kupatwa na tatizo hilo ambalo hujitengeneza lenyewe kwenye figo.
Kwa ujumla ulaji wa epo na matunda mengine, kuna faida sana katika mwili wa binadamu na kunaepusha mwili kupatwa na maradhi ya mara kwa mara. Hatuna budi kuheshimu ushauri tunaopewa na wataalamu wetu kama kweli tunajali afya zetu.
No comments:
Post a Comment