Saturday, August 25, 2007

KOFFI AFANYA 'LAANA!'

Joseph Shaluwa na Zubagy Akilimia
Kinara wa Muziki wa Bolingo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Koffi Olomide, amefanya manunuzi (shopping) ya nguo zilizogharimu kiasi cha milioni tatu na laki nne za Kitanzania, hali iliyotafsiriwa kuwa ni sawa la kufanya laana.

Koffi alifanya manunuzi hayo hivi karibuni katika duka maarufu la nguo liitwalo Zizzou Fashion lililopo Sinza jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuwasili nchini hivi karibuni.

Baada ya kupata habari hizi, waandishi wetu walikwenda dukani hapo na kuzungumza na mmiliki wa duka hilo Athumani Tippo ambaye alithibisha ukweli wa manunuzi hayo yaliyofanywa na Koffi.

“Ni kweli Koffi alifika dukani kwangu wiki iliyopita na kufanya ‘shopping’ ambayo haijawahi kutokea tangu nimefungua duka langu,” alisema Tippo.

Aidha alisema kuwa, kwa kuwa duka lake ni la rejareja, ilikuwa maajabu sana kwake kupata mteja aliyenunua bidhaa za kiasi kikubwa cha fedha kama hicho.

Tippo alisema kuwa ‘zali’ hilo alipewa na rafiki yake aliyemtaja kwa jina la Joseph Kusaga ambaye ndiye aliyempeleka Koffi akiwa na familia yake dukani kwake na kufanya manunuzi hayo.

“Joseph (Kusaga) mwenyewe alinifanyia ‘surprise’ kwa sababu muda mfupi kabla hajafika dukani kwangu, alinipigia simu na kuniuliza kama nilikuwa dukani, nilipomjibu ndio akaniambia nisitoke alikuwa njiani akija, ingawa hakuaniambia kuwa alikuwa akija na Koffi kwa ajili ya kufanya ‘shopping’,” alisema.

Tippo alitaja vitu alivyonunua mwanamuziki huyo kuwa ni viatu, fulana, kapero, mikanda, suti za michezo na vinginevyo na kwamba vitu vilivyokaa dukani kwa muda mrefu zaidi ndivyo alivyonunua kwa wingi zaidi.

“Nguo ambazo zilikaa muda mrefu zaidi dukani, ndizo alizozichukua, naweza kusema Watanzania hatujui mitindo vizuri,” alisema Tippo.

Aliongeza kuwa siku ya kwanza Koffi alifanya manunuzi ya kiasi cha shilingi milioni 2.6 kwa ajili yake pekee, kisha siku iliyofuata alifika tena dukani hapo na kumnunulia mkewe nguo na vitu vidogovidogo vyenye thamani ya shilingi laki nane.

Aidha alisema kuwa pamoja na kufanya manunuzi, pia alimpongeza kwa ubunifu wa lebo mbalimbali za nguo, zikiwemo Jezi za Timu ya Taifa ambazo zimebuniwa na Zizzou Fashion.

“Huwezi kuamini kuwa tayari tuna mpango wa kuanzisha lebo pamoja, itakuwa na jina langu na lake. Tumepanga kuitangaza duniani kote, naamini tutafanikiwa,” alisema.

Watu mbalimbali waliokuwepo wakati Koffi akifanya manunuzi hayo na kubahatika kuongea na waandishi wetu walishangaa na kusema kuwa hawajawahi kuona mtu akifanya laana ya matumizi kama alivyofanya mwanamuziki huyo.

“Ama kweli Koffi ni kiboko, alichokionyesha hapa ni laana ya kutumia”, alisema kijana mmoja aliyejiita ni ‘mtu wa matumizi’.

Koffi Olomide alikuja nchini kwa ajili ya Tamasha la Fiesta (Boda 2 Boda) lililodhaminiwa na Straigh Music, ameondoka juzi Alhamisi Agosti 23, 2007.

No comments: