Tuesday, August 7, 2007

MWONGOZO SAHIHI WA ULAJI


YUO ARE WHAT YOU EAT

Asalaam aleikum jaman! Bwana Yesu asifiwe sana! Tunakutana tena katika kona hii kuelimishana kuhusu staili ya maisha tunayopaswa kuitumia ili tuishi maisha yaliyo huru na maradhi, magonjwa na mateso mengine ya kiafya.

Wiki hii nataka kuwafundisha mwongozo bora wa ulaji sahihi kwa kufuata vipengele 10 katika ulaji wako wa kila siku, vitu unavyopaswa kuvila ambavyo vitaimarisha afya ya mwili wako na kukupa kinga madhubuti dhidi ya maradhi mengine.

Kuwa na afya njema inaweza kuwa kitu rahisi sana iwapo utazingatia vipengele 10 vya msingi vifuatavyo, ambavyo vitakupa angalau mwanga wa kitu gani kinafaa kufuatwa katika staili yako ya kula kila siku .

Jaribu kadri uwezavyo kufuata vipengele hivi na kuvifanya kuwa sehemu ya maisha yako. Hata hivyo usijilazimishe sana kama hutawezi kuvifuata vyote. Ukishindwa kuvifuata vyote, basi angalau jaribu kufuata ile sheria ya asilimia 80 kwa 20.

Sheria hiyo inasema kwamba iwapo utakuwa ukila na kunywa vizuri kama inavyotakiwa kwa kiwango cha silimia 80, basi hata kama ikitokea ukala na kunywa vibaya kwa kiwango cha asilimia 20, bila shaka mwili wako utaweza kukabiliana na vitu hivyo vya asilimia 20 na vitadhibitiwa kirahisi.

1: KULA MLO WA ASUBUHI (breakfast)

Anza siku kwa kula mlo mzuri ili upate kiwango kizuri cha nishati mwilini na kuwa na uwezo wa kujidhibiti na utakacho kula baadae siku hiyo, ikiwa ni pamoja na kula kiwango kidogo cha sukari na kahawa. Upe mwili wako nishati ya kutosha kwa kunywa uji wa ulezi, mtama au mahindi ya lishe.

2. KUNYWA MAJI YA KUTOSHA (drink enough water)

Kunywa lita mbili za maja kila siku, maji ni muhimu sana kwa ufanisi wa mwili wako. Unaweza kukaa wiki kadhaa bila kula, lakini huwezi kukaa muda huo bila kunywa maji. Kama hujazoea kunywa maji kiasi hicho, basi anza kujizoesha taratibu kwa kunywa kiasi kidogo hadi mwili utakapoweza kufikisha lita 2.

Unaweza kunywa maji kiasi utakachoweza kisha kiasi kingine ukakifidia kwa kunywa sana juisi za matunda, matunda yenyewe, kama vile papai, machungwa, lakini epuka kunywa kahawa. Kama tulivyoona wiki iliyopita, ukiona mkojo wako ni wa njano au kahawia na una harufu kali, elewa mwili wako umepungukiwa maji.

Kipimo kizuri cha kutambua kama umekunywa maji ya kutosha kwa siku, ni kujiwekea mazoea ya kununua au kutumbea na chupa ya maji ya ujazo wa lita moja, ambayo utainywa mara mbili kwa vipindi tofauti vya siku ili kufikia kiwango cha lita 2.

3. TUMIA KAHAWA KIASI KIDOGO

Punguza unywaji wa kahawa, kwa sababu kahawa huwa ni chanzo cha upungufu wa maji mwilini na la msingi zaidi kahawa hukausha maji mwilini! Vile vile kahawa huharibu virutubisho na madini mengi yanayoingia mwilini na vile vile inaweza kukuchangamsha kupita kiasi na kusababisha matatizo ya kiakili.

Jiwekee ukomo wa kunywa kikombe kimoja cha chai au kahawa kwa siku, usizidishe. Pombe vile vile nayo ina kilevi cha kuchangamsha mwili, hivyo nayo inapaswa kunywewa kwa kiasi kidogo na kwa uangalifu.

4. NUNUA VITU ASILIA (buy fresh)

Penda kununua vitu asilia na hai, kwani kadri vyakula hivyo vitakavyokuwa katika hali yake ya asili ndivyo ambavyo vitakavyoweza kukupatia virutubisho vingi mwilini. Usipenda kununua vyakula vya kwenye makopo na kuacha kununua vitu asilia sokono. Jaribu kununua kila kitu kikiwa halisi, mfano; kama ni nyaya iwe halisi na siyo ya kwenye kopo. Kama maharage, pika mwenyewe, usile ya kwenye kopo.

5. ANDAA MLO WAKO MWENYEWE (prepare your meal)

Andaa chakula chako mwenyewe, vyakula vilivyokwisha pikwa na vile viliivyokwisha tayarisha kabisa, huwa siyo bora kiafya, kwani mara nyingi huwekewa dawa za kuhifadhi na kuongeza maisha ya kukaa dukani, dawa hizo zaweza kuwa na madhara kiafya zinapotumiwa kwa wingi. Aidha vyakula hivyo huwa na kiasi kikubwa cha sukari, chumvi na mafuta mabaya. Unapoandaa mwenyewe chakula, utajua kipi kizuri ukiweke na kipi kibaya ukiache.

Itaendelea wiki ijayo.....

No comments: