Thursday, August 30, 2007

RAY MBARONI CHINA


Na Kulwa Mwaibale
Mkali wa filamu na Michezo ya kuigiza nchini, Vincent Kigosi 'Ray', hivi karibuni alionja joto ya jiwe baada ya kutiwa mbaroni na Askari Polisi wa China.

Chanzo chetu cha habari kilichopo nchini humo, kinaeleza kuwa wanausalama hao walifikia hatua hiyo baada ya kumhisi kuwa alikuwa akitaka kufanya ugaidi.

Aidha chanzo hicho ambacho hakikupenda kuandikwa jina lake gazetini, kilieleza kuwa Ray alifika nchini humo akiwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Tollywood Movie, Eric Shigongo, kwa kazi ya kurudufu filamu ya Fake Pastors.

"Mimi nilikuwa mwenyeji wao, walikuja kwa ajili ya kurudufu filamu hiyo ili waweze kuiuza kwa bei nafuu Tanzania, lakini wakiwa hapa wakapata mkataba na kampuni nyingine kwa ajili ya kutengeneza filamu moja”, kilisema chanzo hicho.

Habari zaidi zinasema, Ray aliingia mkataba na Kampuni ya Chinese Film Production kwa niaba ya Kampuni ya Tollywood Movie ya nchini Tanzania kwa makubaliano ya kutengeneza filamu moja iliyopewa jina la From China With Love.

Kati ya wasanii ambao wameshiriki katika filamu hiyo kutoka China ni pamoja na mwanamuziki maarufu Irene Maltino ambaye ni raia wa Ufilipino anayefanya shughuli zake za muziki nchini humo.

"Baada ya kuwapata wasanii hao, wapiga-picha wa Kampuni ya Chinese Film Production wakiwa na Ray na mastaa hao, walikwenda ufukweni usiku kupiga picha za filamu hiyo," kilieleza chanzo hicho.

Habari zaidi zinaeleza kuwa wakiwa ufukweni hapo wakiendelea na zoezi la upigaji picha, polisi walifika na kuwatia mbaroni ambapo waliwahoji na kumtaka Ray aoneshe kibali cha kupiga picha na hati yake ya kusafiria, vitu ambavyo hakuwa navyo, hali iliyosababisha Ray kufikishwa kituoni.

"Alipokuwa kituoni alimpigia simu Mkurugenzi wake (Eric Shigongo) ambaye alikwenda kuchukua hati ya kusafiria pamoja na kibali katika hoteli waliyofikia, kisha akavipeleka polisi ambapo aliachiwa," kilihitimisha chanzo hicho.

Akizungumza na Ijumaa baada ya kuwasili nchini, Ray alikiri kukamatwa na askari nchini China ambao walifikiri alikuwa akipiga picha hizo kwa nia ya kufanya uhalifu, lakini walipogundua sivyo walimwachia.

"Ni kweli kaka, nilipatwa na dhoruba kidogo lakini baadaye waliniachia huru! Unajua nilikosea kitu kimoja tu, kutembea bila hati yangu na kibali cha kupiga picha, kama ningekuwa navyo nisingepata usumbufu huo. Hata hivyo kila kitu kilikwenda sawa, namshukuru Mungu nimerudi nyumbani salama salimin," alisema Ray.

No comments: