Thursday, October 25, 2007

MASIKINI WAZIRI SALOME MBATIA!!!!


Na Salum Mnette

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Salome Joseph Mbatia, amefariki dunia kwa ajali ya gari.

Mheshimiwa Mbatia alifariki leo jioni pamoja na watu wengine watatu akiwemo dereva wake, baada ya gari alilokuwa akisafiria kugongana na gari ya mizigo aina Fuso katika eneo la Kibena Wilaya ya Njombe mkoani Iringa.

Akizungumza kwa simu na gazeti la Championi, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Advocate Nyombi alisema Waziri Salome alipata ajali hiyo alipokuwa akitoka Iringa mjini kuelekea Njombe.


"Ni kweli Naibu Waziri Salome amefariki katika ajali mbaya iliyotokea saa kumi na moja kasoro robo jioni eneo la Kibena na hivi sasa niko njiani kuelekea kwenye eneo la tukio, nipigie baadaye naweza kukupa habari zaidi," alisema Kamanda Nyombi.

Habari zaidi zinasema kuwa Fuso lilikuwa limebeba shehena ya mbao na iliwachukuwa muda wa saa moja waokoaji kutoa miili ya marehemu na majeruhi wa ajali hiyo kwani gari la mizigo lilikuwa limeifunika gari ya Waziri Mbatia.

Hii ni ajali ya tatu kwa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, kwani mapema mwaka huu aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Juma Jamaldin Akukweti alipata ajali ya ndege mkoani Mbeya na kufariki dunia.

Kadhalika, mwezi uliopita, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mhe. Juma Kapuya alipata ajali ya gari na kuvunjika mbavu wilayani Urambo mkoani Tabora.

No comments: