Elvan Stambuli na Makongoro Oging’ (Gazeti la Uwazi - Okt 16)
Mufti wa Tanzania, Sheikh Shaaban Simba ambaye alialikwa katika karamu ya Sikukuu ya Idd ya Rais Jakaya Kikwete Ikulu na kumtuma msaidizi wake Naibu Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zuberi akiwa na Masheikh wengine, walijikuta wakitimuliwa Jumamosi iliyopita.
Habari zilizolifikia gazeti hili siku ya tukio zinasema wakati wa kwenda Ikulu jijini Dar es Salaam, Naibu Mufti Sheikh Zuberi alifuatana na viongozi wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) akiwemo Katibu wa Baraza la Ulamaa na Kamishna wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Sheikh Hassani Chizenga na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Abdallah Nyasi.
Wengine ni Katibu wa Hija, Sheikh Sued Sued, Mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje wa BAKWATA, Sheikh Iddi Hussein, Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Nguruko na Katibu wake Alhaji Suleiman Magubika.
Habari za uhakika zilizolifikia gazeti hili zinasema Masheikh hao walikwenda Ikulu baada ya kualikwa na Rais Kikwete huku Naibu Mufti, Sheikh Zuberi akimuwakilisha Mufti wa Tanzania Sheikh Shaaban Simba ambaye alikuwa katika shughuli za sikukuu ya Iddi za kitaifa iliyofanyika mjini Lindi na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein.
Mara baada ya kupata habari hizo waandishi wetu walikwenda Makao Makuu ya BAKWATA na kuwakuta viongozi wote waliotimuliwa Ikulu wakiwa wanatafakari hali hiyo chini ya mwembe ambapo baada ya kuulizwa kuhusu habari hizo walikiri kutokea.
Hata hivyo, Naibu Mufti alimruhusu Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ali Nguruko kuzungumza na Uwazi ambapo alisema wamefedheheshwa sana na waliyofanyiwa Ikulu.
Akifafanua zaidi Sheikh Nguruko alisema Rais Kikwete aliswali swala ya Iddi katika Msikiti wa Al Farouk, Makao Makuu ya BAKWATA na akaagiza Naibu Mufti na viongozi wenzake waende Ikulu katika karamu aliyoiandaa bila kukosa.
"Rais Kikwete aliagiza kuwa Naibu Mufti na jopo lake waende Ikulu kwa sababu ameandaa karamu, tuliondoka baada ya kuagana na Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi ambaye pia aliswali hapa, tulipofika getini Ikulu tulipekuliwa kwa kufunuliwa kanzu zetu, hata Naibu Mufti alifunuliwa, tulisikitika sana, tulijiuliza hawa hawajui kuwa Masheikh hawa ndio waliomswalisha Rais leo," alisema Sheikh Nguruko.
Aliongeza kuwa kilichowasikitisha zaidi ni kuona raia wa kigeni wakipita na kuingia Ikulu bila kupekuliwa kama alivyofanyiwa Naibu Mufti na wao lakini kibaya zaidi alisema ni kitendo cha jopo zima la Bakwata kutoruhusiwa kuingia Ikulu kama alivyoagiza Rais Kikwete.
"Kwanza wale watu tuliowakuta getini walipaswa kujua kwamba Naibu Mufti ana heshima yake kitaifa na pia alikuwa akimuwakilisha Mufti wa Tanzania, sasa kumpekua mpaka kwenye mkanda na kumkatalia kuingia tumeona kuwa wamemdharau na kumdhalilisha kiongozi wetu, "alisema Sheikh Nguruko.
Naye Katibu wa Ulamaa, Sheikh Chizenga alisema kwamba hii ni mara ya kwanza kwa viongozi wakuu wa BAKWATA kukataliwa kuingia Ikulu katika sherehe ya Iddi kwani viongozi wa awamu zote tatu za serikali zilizopita walikuwa hawafanyi hivyo, hivyo kuwatupia lawama watendaji wa Ikulu na sio Rais Kikwete.
"Kiongozi Mkuu wa nchi kama Rais Kiwete anapotoa agizo watendaji ni lazima watekeleze, hatukuona sababu ya kutoruhusu msafara wa Naibu Mufti kukwama kuingia Ikulu kwani licha ya kumwakilisha Mufti Mkuu Tanzania, Rais Kikwete alitoa mwaliko hadharani na kusisitiza kwamba shughuli yake itachelewa kuanza kutusubiri sisi, tukakwama getini," alisema Sheikh Chizenga.
Alibainisha kuwa walijaribu kuwasihi maofisa waliokuwa getini wawaruhusu kuingia lakini walikataa kata kata na kwamba japokuwa yeye (Sheikh Chizenga) aliruhusiwa kuingia hakukubali kufanya hivyo kwa kuwa Naibu Mufti alikataliwa hivyo naye kususa kuingia kwenda kwenye shughuli hiyo ya Rais Kikwete.
Aidha Sheikh mwingine aliyesusa kuingia Ikulu ni Sheikh Yahya Hussein ambaye alipofika getini aliruhusiwa lakini mtoto wake wa miaka mitano alizuiliwa na akaambiwa yeye aende lakini mtoto abaki getini.
"Nilisema haya mambo ni ya ajabu, nitamuachaje mtoto getini? Walikataa kumruhusu mtoto basi tukakusanyana na masheikh wengine tukajiondokea na kuja nyumbani kwangu kunywa chai,'' alisema Yahya.
1 comment:
Hii habar km ni ya kweli basi ni mtihani sana....
Post a Comment