Tuesday, October 16, 2007

YOU ARE WHAT YOU EAT!


VIDONDA VYA TUMBO:

Husababishwa na unavyokula!

Kama tulivyoona wiki iliyopita kwamba staili na aina ya chakula unakachokula ndicho kinachokufanya uwe mnene au mwembemba, leo pia tutaelezea kuhusu ugonjwa wa vidonda vya tumbo, ambao nao unatokana na jinsi unavyokula na unaweza kuudhibiti kwa vyakula tu.

Kitabibu au kitaalamu, vidonda vya tumbo vinaelezewa kama ni ile hali ya kuwepo kwa vidonda kwenye utumbo mrefu au mfupi, kwa ndani. Vidonda vilivyopo kwenye kona ya utumbo mfupi vinajulikana kama Duodenal ulcers na vile vya kwenye utumbo mpana (tumbo) ni Gastric ulcers.

DALILI KWAMBA UNA VIDONDA VYA TUMBO

Dalili kwamba una vidonda vya tumbo ni nyingi, lakini zinazojulikana zaidi ni kusikia maumivu makali sehemu ya juu ya tumbo kwa wenye vidonda kwenye utumbo mfupi. Maumivu ya vidonda kwenye utumbo mrefu, mara nyingi huja saa moja baada ya mlo na mara chache huja usiku.

Maumivu ya vidonda vya kwenye utumbo mfupi, mara nyingi huja kabla ya mlo, pale tumbo linapokuwa tupu, yaani mtu anaposikia njaa. Maumivu hayo huondolewa kwa chakula, hasa maziwa ambayo yameonekana kuwasaidia watu wengi kupoza maumivu yake.

Vidonda vinapoendelea kuwepo kwa muda mrefu, maumivu huwa makali zaidi na husababisha mwili kudhoofika na kukosa nguvu. Vile vile hali inapoendelea kuwa mbaya zaidi, kinyesi cha mwathirika hutoka na damu.

KITU GANI KINACHANGIA VIDONDA HIVI?

Kitu kinachochangia mtu kupata vidonda vya tumbo ni chakula tu. Aina ya chakula na jinsi unavyokila ndiyo 'mama' wa tatizo hili, matatizo mengine ya kimaisha na msongo wa mawazo au baadhi ya madawa ni miongoni mwa vitu vinavyofanya tatizo kuwa gumu zaidi lakini siyo chanzo. Stali yako ya ulaji inapokuwa nzuri, matatizo mengine hudhibitiwa kwa lishe tu.

Vidonda vya tumbo ni matokeo ya tumbo kuwa na gesi nyingi ambayo husababishwa na ulaji mbovu, kama vile kula na kushiba kupita kiasi, kula vyakula vyenye viungo vingi vikali kama pilipili, unywaji sana wa kahawa, pombe na uvutaji sigara. Ukiwa na staili ya maisha kama hii, lazima utapata vidonda vya tumbo na hakuna dawa ya kuponya ila kufuata kanuni za ulaji sahihi.

Wakati tukikueleza hapa baadhi ya vyakula vitakavyoweza kukupa nafuu ya vidonda, lazima staili yako ya ulaji pia nayo ibadilike.

NDIZI MBIVU KAMA TIBA YA VIDONDA VYA TUMBO

Inaelezwa na wataalamu wetu wa tiba mbadala kuwa ndizi mbivu ni moja kati ya tiba za nyumbani zenye nguvu sana katika kutibu tatizo la vidonda vya tumbo. Tunda hili, ambalo upatikanaji wake hauna shida wala msimu kwa kila mtu, linaaminika kuwa na virutubisho vya ajabu visivyojulikana, ambavyo kiutani wamevipachika jina la Vitamini U (against ulcers)!

Ndizi inapoliwa na ikifika tumboni, ina uwezo wa kutuliza makali ya gesi na kupunguza kuuma kwa vidonda kwa kuuwekea kinga utumbo mzima. Ili upate faida za ndizi kama tiba, hasa kwa wale ambao wako katika hatua za mwanzo za kuumwa vidonda, kula ndizi mbivu mbili pamoja na maziwa mara tatu au nne kwa siku. Fanya hivyo kama sehemu ya mlo wako kila siku.

KABICHI KAMA TIBA YA VIDONDA VYA TUMBO

Kama ilivyo kwa ndizi, kabichi nayo inaaminika kuwa tiba nzuri ya nyumbani ya kudhibiti vidonda vya tumbo. Chukua robo kilo ya kabichi, ichemshe na maji ya nusu lita hadi yabaki robo. Kisha yachuje na uyaache yapoe. Yakisha poa, kunywa mara mbili kwa siku.

Aidha, mbali ya kuchemsha na kunywa maji ya kabichi, pia unaweza kutengeneza juisi yake ambayo nayo ni bora kwa matatizo ya vidonda vya tumbo. Kwa kuwa juisi ya kabichi ina nguvu sana, itapendeza ikichanganywa na juisi ya karoti kwa kipimo cha nusu kwa nusu na kisha kunywa mara mbili kwa siku.

MAZIWA YA MBUZI KAMA TIBA YA VIDONDA VYA TUMBO.

Mbali ya kula ndizi mbivu pamoja na maziwa ya ng'ombe, kunywa maziwa ya mbuzi peke yake nayo ni dawa kubwa ya vidonda vya tumbo. Ili kupata matokeo mazuri na kwa muda mfupi, kunywa glasi moja ya maziwa ya mbuzi ambayo hayajachanganywa na kitu kingine, mara tatu kwa siku.

MLO WA MTU MWENYE VIDONDA VYA TUMBO

Mlo wa mtu mwenye vidonda vya tumbo unapaswa kupangiliwa kwa makini zaidi ili kutoa lishe inayotakiwa mwilini na wakati huo huo kutoa kinga kwa utumbo ulioathirika na vidonda. Maziwa, krimu, siagi, matunda, mboga mboga, vyakula vingine vya asili vyenye vitamini mbalimbali, ndiyo mlo wa kila siku anaopaswa kula mtu mwenye vidonda.

TIBA NYINGINE

Masaji (massage) ya mwili mzima pamoja na mazoezi ya kuvuta na kutoa pumzi ni miongoni mwa vitu vinavyosaidia kutuliza au kudhibiti vidonda vya tumbo. Mbali na yote hayo, mgonjwa anapaswa kuachana na mawazo na badala yake awe mwenye furaha, hivyo hana budi kutengeneza mazingira ya kuwa mbali na vitu vinavyomkasirisha na kumletea mawazo.

No comments: