Monday, November 19, 2007

SHOWBIZ

Chid Benz achomoa bifu na Ngwea

Mwana Hip Hop bora 2007 kupitia Tunzo za James Dandu, Rasheed Abdalla Makwiro a.k.a Chid Beenz (juu) mwenye maskani yake Ilala Flat, Dar es Salaam, amechomoa kwa nguvu zote kuwa hana bifu na Albert Mangwea wa Chamber Squard kama baadhi ya Wabongo wanavyovumisha, Violet Mushi alipiga naye stori.

Akikazia zaidi kuhusu hilo, Benz alitamka kwamba ameshangazwa na maneno yaliyozagaa mtaani kwamba yeye ana bifu na Ngwea wakati hajawahi hata siku moja kufikiria kuwa na ugomvi na msanii huyo: 'Nimesikia tu ishu za chinichini kuwa anajitangazia kuwa na bifu na mimi, lakini siwezi kuamini kwasababu ninapokuwa naye haoneshi kama ananisema vibaya'.

Akiwa anafanya vizuri na kazi yenye jina la Naitwa nani ambayo amemshirikisha mrembo Jaqueline Ntuyabaliwe 'K-Lyin', mshikaji yuko mbioni kudondoka na albamu yake ya kwanza aliyoipa jina la Chid Benz itakayosheheni nyimbo 17.


C2C kufunga mwaka kwa taarab

Ule mpambano wa bendi nne za taarab, ulioandaliwa na Kampuni ya QSSP kupitia kituo cha televisheni cha C2C na Lino Promotions, unatarajiwa kufikia ukingoni kwa shughuli kubwa itakayofanyika ndani ya ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Novemba 30 mwaka huu, Richard Bukos anakuhabarisha.

Ndani ya safu hii, maratibu wa mpambano huo, Suleiman Ling'ande alisema kwamba siku hiyo kura za mashabiki ambazo zilianza kupigwa Agosti 5, mwaka huu, zitahesabiwa na mshindi kutajwa 'live'. Aliyataja makundi hayo kuwa ni East African Melody, Jahazi Modeln Taarab, Zanzibar Stars na Dar Modern Taarab.

Kwa upande wake Meneja wa kituo cha C2C, Bahati Sigh amewataka mashabiki wa makundi hayo kuendelea kuyapigia kura: 'Mashabiki wa East African Melody wanatakiwa kutuma neno EAM kupitia simu zao za mkononi kwenda namba 15551

'Mashabiki wa Kundi la Zanzibar Stars wanatakiwa kutuma neno ZSM kwenda 15551, wale wa Dar Modern Taarab wanatakiwa kutuma neno DMT kwenda 15551 halikadharika mashabiki wa Jahazi waandike neno JMT kwenda 15551 ili kulipatia ushindi kundi lao.'

Kundi la T.O.T Taarab ambalo pia lilikuwemo katika mpambano huo unaoendeshwa kupitia kituo hicho cha televisheni lilitolewa Novemba 6 mwaka huu baada ya kupata kura chache kutoka kwa mashabiki.

Kampuni ya Global Publishers wachapishaji wa magazeti ya Uwazi, Amani, Risasi, Championi, The Bongo Sun, Ijumaa, Ijumaa Wikienda pamoja na jarida la S&C ni miongoni mwa wadhamini wa shindano hilo.


CCM Kirumba itakuwa full nyomi

Zikiwa zimesalia siku chache kuifikia Desemba Mosi, siku ya Ukimwi dunia, wakazi wa Mwanza na vitingoji vyake wanatarajia kupata burudani ya kutosha kutoka kwa mastaa mbalimbali wa muziki.

Katika tamasha hilo kubwa litakalofanyika ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba na kutabiriwa kujaza watu kibao (full nyomi) ambalo mwaka jana lilikusanya watu zaidi ya 25,000 na kuacha gumzo kubwa katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam, vijana wataongea kuhusu gonjwa hatari la Ukimwi.

Mbali na vijana kupiga stori na wenzao kuhusu Ukimwi, wasanii kibao wataangusha mistari ya nyimbo zilizowahi na zinazotamba hivi sasa. Nawazungumzia Fareed Kubanda 'Fid Q', Joseph Haule 'Profesa Jay', Hamis Baba 'H. Baba', Hardmad, Ambwene Yesaya 'AY', Flora Mbasha na wengine kibao. Hebu piga picha halafu ujiulize, siku hiyo CCM Kirumba itakuwaje?

Siyo wakongwe peke hayo ambao watapata nafasi ya kupiga shoo, bali kutakuwa na chipukizi kibao wa Mwanza ambao wataonesha uwezo wao katika game hiyo ngumu ambayo ukiipatia inakutoa kimaisha.

Kwa mujibu wa wa waandaaji wa tamasha hilo ambao ni Kamati ya Umoja wa Vijana CCM 'inayodili' na mapambano dhidi ya Ukimwi, vikundi vya watu binafsi, asasi za kiraia na taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali, zitatoa mada kuhusu ukimwi na kuchana live kauli mbiu isemayo, 'Zuia Ukimwi, tunza ahadi'.

No comments: