Tuesday, December 16, 2008

UJUE MWILI WAKO UNAHITAJI NINI ZAIDI!

Mwili wa binadamu unajengwa na vyakula vitokanavyo na nafaka, kama vile mahindi, mchele, ngano, mtama, nk. Aina hii ya vyakula ndiyo msingi mkubwa wa afya ya binadamu. Je, ni wangapi na kwa kiasi gani tunakula vyakula hivi?

Kwa mujibu wa wanasayansi, mwili wa binadamu una jumla ya chembechembe hai (cells) zaidi ya trioni 70. Katika chembechembe hizo ndipo ulipo uhai, zikifa na binadamu nae hufa, zikiwa dhaifu na binadamu nae huwa hivyo hivyo. Binadamu hawezi kuwa na afya njema kuliko chembechembe zake. Chembechembe ndizo zinazopokea virutubisho na kutoa uchafu mwilini, ikiwemo sumu.

Ili chembechembe hizo ziwe hai zinahitaji kula na chakula chake ni virutubisho tu ambavyo asilimia kubwa na muhimu inapatikana katika vyakula vya nafaka. Ndani ya nafaka, kama vile mchele, ngano na soya, mbali ya vitu vingine, kuna aina mbili muhimu za mafuta (fats), ambazo ni Lipids na Steroids.

Kwa mujibu wa wanasayansi wetu, aina hizo mbili za mafuta ni muhimu sana kwa uhai na ustawi wa chembechembe za mwanadamu. Mafuta aina ya Lipids hufanya kazi ya kulisha na kukarabati ukuta wa chembechembe na Steroids hufanyakazi ya kuzalisha nishati zinazompa binadamu nguvu ya kufanya kazi kazi zake.

Madhara ya kuwa na chembechembe dhaifu ni makubwa na unaweza kuyasikia mwenyewe. Kwanza mwili huwa mchovu, usio na nguvu, unapotumia dawa hazifanyi kazi upesi mwilini, kama ni dozi ya malaria, ni lazima utumie zaidi ya moja au dawa kali zaidi! Katika hili wengine wanasema fulani ana malaria sugu, lakini ukweli ni kwamba chembechembe zako zimekauka, hazina tena uwezo wa kupenyeza kitu na kutoa sumu mwilini.

MATUNDA NA MBOGAMBOGA
Hili ni kundi la pili la chakula ambalo nalo ni muhimu sana. Baada ya kujenga mwili (chembechembe hai), sasa unahitaji kuulinda ili uwe imara na unaofanya kazi yake sawasawa. Kazi hiyo inafanywa kwa kula matunda na mbogamboga kwa wingi, chakula hiki ndicho kinachojenga kinga ya mwili (Body Immunity System), hivyo kuupa mwili wako uwezo wa kujikinga dhidi ya wavamizi, ambao ni maradhi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani (WHO), binadamu anatakiwa kula milo ya matunda na mboga kati ya 5-9 kila siku. Mboga na matunda zina virutubisho muhimu vinavyotoa kinga mwilini (Anti-oxidant) ambayo hupambana na kuondoa viini vya magonjwa (free radicals).

Kwa bahati mbaya sana, baadhi ya watu hula matunda kwa nadra sana na wengine hawali kabisa! Msimu wa matunda unaingia mpaka unaisha, mtu hajala hata tunda moja au kama kala, basi ya kuhesabu, wengine mpaka waagizwe na daktari.

Kwa upande wa mboga za majani hali ni mbaya zaidi, watu hawapendi kula mboga za majani, zinachukuliwa kama chakula cha kimasikini, bila kujua kwamba kwa kuacha kula mboga za majani unaunyima mwili wako kitu muhimu sana.

Ni vizuri ikaeleweka kwamba binadamu hatuwezi kula kama zinavyotaka nafsi zetu, bali tunapaswa kula kama miili yetu inavyotaka. Sisi hatuwezi kuwa muhimu kuliko miili yetu. Mwili ukiamua kugoma huwa hatuna ujanja. Unapopatwa na kiharusi na kupooza mwili, kwa mfano, hapo mwili huwa umegoma kufanyakazi na chanzo huwa ni wewe mwenyewe!

Mwili umeumbwa kama mnyororo, unategemeana sehemu moja na nyingine, sehemu moja inapopatwa na tatizo, mwili mzima unataabika. Ukipatwa na jipu au uvimbe kwenye kidole chako cha mwisho, mwili mzima utakosa raha na hata usingizi unaweza usipate kwasababu ya maumivu! Hivyo hatuna budi kutii miili yetu kwa kula vyakula ambavyo inavihitaji.

DONDOO ZA LEO
Baada ya saa 11 jioni, usipende kula na kushiba sana. Kula sana mchana, usiku kula kiasi. Punguza idadi ya vyakula vyenye mafuta katika milo yako ya kila siku, mafuta siyo mazuri kiafya.

Kunywa maji mengi asubuhi na kiasi kidogo sana usiku. Wakati mzuri wa kulala ni kati ya saa 4:00 usiku na saa 12:00 alfajiri. Haipendezi kuzidisha muda huo….ni hayo tu kwa leo.

1 comment:

Anonymous said...

Kweli umetupa live... wasomaji wako...nikweli kula matunda mpaka Dactari aseme....wengine hata kunywa maji mpaka asikie KIU ndipo anywe maji, ina maana bila kuhisi KIU maji hanywi kabisaa.

Hongera kwa nakala hii....maisha bila AFYA si maisha....