Wednesday, February 4, 2009

HIVI NDIVYO UTAKAVYO PUNGUZA UZITO WAKO!-2

Wiki iliyopita tulianza kuzungumzia suala la kupunguza uzito na kuona hatua kadhaa anazopaswa mtu kuzichukua ili kufikia lengo alilojiwekea katika kupunguza au kuongeza uzito, endelea..

Kama nilivyotangulia kusema hapo awali, suala la kupunguza uzito linahitaji mahesabu na nia, lakini kwa kuwarahisishia wasomaji wangu, nisingependa kuyachambua sana mahesabu hayo, muhimu uelewe tu kwamba unachokula ndicho kinachotengeneza kalori na kazi unazozifanya ndizo zinazotumia kalori zako, hivyo kalori ni kama mafuta kwenye gari.

Kwa kuwa tumeshajua maana ya kalori na kwamba ili upunguze uzito unahitaji kuingiza kalori chache mwilini na utoe nyingi, basi ieleweke kwamba ili mtu upungue uzito, unatakiwa upunguze kula, lakini uongeze kufanyakazi au mazoezi.

Kwa kuanzia, punguza kiwango cha chakula unachokula kwa asilimia 50 na uongeze kiwango cha shughuli zako au mazoezi mara mbili. Kama asubuhi ulikuwa ukinywa chai vikombe viwili vya maziwa, kunywa kikombe kimoja bila maziwa. Hivyo hivyo ufanye kwenye vitafunwa.

Kwa upande wa chakula cha mchana au jioni, nacho kula nusu yake, jizuie kula pale unapohisi hujashiba na chakula ni kitamu, ukiacha kula wakati bado hujashiba, ndiyo vizuri zaidi. Hii ni njia moja, lakini nyingine ni kupendelea kula matunda, mboga mboga na juisi mchana kutwa kwa kiwango kidogo, kwani kiwango chake cha kalori ni kidogo lakini zina virutubisho vyote muhimu mwilini.

Wakati ukipunguza kiwango cha chakula unachokula, ongeza kiwango cha kazi au mazoezi unayoyafanya, kama ulikuwa hufanyi mazoezi basi anza kufanya, japo kidogo. Kama ulipenda kupanda basi au gari hata kwa safari fupi, sasa anza kutembea kwa miguu, kama ukifika ofisini kwako unatumia lift, sasa acha na badala yake tumia ngazi, ili mradi ushughulishe mwili wako. (keep yourself busy).

Njia nyingine ya kupunguza uzito tena kwa haraka na salama zaidi ni kufunga kwa siku 30 – 60 mfululizo. Njia hii ni bora na salama kwani itakuhakikishia uzito unapungua na wakati huo huo unaimarisha afya yako. Unaweza kuamua kufunga kwa kutokula kitu chochote mchana au kwa kula juisi na matunda tu!

Wakati wa kufungua jioni, usile vyakula vya mafuta wala usile mpaka ukashiba sana. Kula vyakula laini na asili kama vile juisi, mbogamboga, uji au chai ya rangi, mihogo, viazi vitamu au viazi mviringo, maharagwe, kunde, n.k, itakuwa vizuri kama vyakula hivyo vikiwa vimetayarishwa bila mafuta.

Kwa kumalizia napenda kusisitiza tena kwamba, ili upunguze uzito, unahitaji kuwianisha kiwango cha chakula unachokula na kazi unazozifanya. (Kula kiasi + mazoezi/kazi nyingi= kupungua uzito au ingiza mwilini kalori chache + toa kalori nyingi mwilini= kupungua uzito ). Huwezi kupunguza uzito kwa kupunguza kula tu bila kuushughulisha zaidi mwili wako. Natumaini somo limeeleweka.

No comments: