Friday, February 27, 2009

IJUMAA SHOWBIZ!



...na mshindi ni...
Mambo vipi Tanzania? Leo ndiyo Shindano la Ijumaa Sexiest Girl lililokuwa na msisimko wa aina yake linafikia ukingoni na Wema Sepetu, Irine Uwoya wameingia fainali, kwa ruhusa tuliyopewa na kamati ya maandalizi ya mpambano huu ikiongozwa na Mratibu wake, Oscar Ndauka, tunachukua fursa hii kutamka kwamba, mshindi ni...!

Samahanini sana wasomaji na wapenzi wa shindano hili, kwa mujibu wa mratibu Oscar Ndauka, mshindi amekwishapatikana lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu atatangazwa Ijumaa ijayo, kwani hivi sasa wanaweka mazingira mazuri kwa ajili ya kumtangaza mshindi, ikiwemo kumpatia zawadi.

“Hivi sasa hatutapokea kura tena, tunawashukuru wote waliolifanya shindano hili likafikia ukingoni kwa mafanikio, bila kuwasahau warembo wote walioshiriki kwenye mpambano huu, asanteni sana na kumbukeni kwamba, mwisho wa shindano hili ndiyo mwanzo wa mashindano mengine yajayo,” alisema Ndauka.
********************************
Hermy B Wasanii wengi wanapenda bure
Wiki iliyopita ShowBiz ilikuwa mitaa ya Kinondoni, ndani ya Studio za Bhitz Music Company na kupiga stori mbili tatu na mtayarishaji muziki Harmes Baric Lyimo ‘Hermy B’ ambaye hivi sasa kazi zake ziko juu, nazizungumzia ‘Habari ndiyo hiyo’ ya Mwana FA na A.Y, Bado nipo nipo, Msiache kuongea (Mwana FA) na nyingine kibao.

Hermy ambaye wiki hii ameachia ngoma mpya yenye jina la ‘Leo’ ya kwake Ambwene Yesaya ‘A.Y’ alisema na safu hii kwamba kikubwa kinawakatisha tamaa baadhi ya watayarishaji muziki wakali ni tabia ya baadhi ya wasanii wakiwemo wakongwe kupenda kufanyiwa kazi bure.

“Nafahamu kwamba wasanii wengi wa Bongo wanaanza muziki katika mzingira magumu, lakini siyo wakongwe pia ambao tayari wamekwishafanikiwa. Msanii anakupigia simu anakwambia anataka kufanya kazi na wewe ili akuze jina la studio, wakati kila kifaa kinachotumika studio nimekigharamia. Wasanii wanatakiwa wafahamu kufungua studio ni gharama kubwa, hiyo imewakatisha tamaa baadhi ya ‘maproducer’ wengi, sina haja ya kuwataja majina.

“Kitu kingine ni kwamba, wasanii wenyewe hawapendi kuumiza vichwa kuandika nyimbo nzuri na hata ukiwapa ‘idea’ wanakuwa wabishi kufanya wakati muziki kila siku unabadilika. Hiyo ni sababu mojawapo inayonifanya nisiwe na lebo katika studio yangu zaidi ya kufanya kazi na Mwana FA na A.Y ambao tunaelewana kwa kiasi kikubwa ikiwemo kwenye ishu ya mkwanja.
**************************************

Solo Thang Atanguliza ngoma mpya Bongo
Baada ya kujichimbia pande za Uingereza kwa takribani miaka kadhaa akipiga kitabu, msanii Msafiri Kondo ‘Solo Thang’ amevunja ukimya kwa kurusha ngoma yake moja mpya yenye jina la ‘Travellah’ ili kuwaweka sawa mashabiki wake, kwamba siku kadhaa zijazo atadondoka Bongo. Mengi zaidi kuhusu mchizi endelea kufuatilia ShowBiz.
*****************************
Kikosi cha Mzinga Sasa ni Hip Hop Against Albino Violence
Kutoka ndani ya Kundi la Kikosi cha Mizinga lenye maskani yake Block 41, Kinondoni, Dar es Salaam, ShowBiz imeambiwa na kiongozi wake, Karama Masoud ‘Kalapina’ kwamba limeandaa mapambano dhidi ya watu wanojihusisha na mauaji ya Maalbino.

Ndani ya safu hii, Kalapina alisema kuwa tayari wameandaa wimbo unaopinga mauaji ya Maalbino ambao utaanza kusika hivi karibuni kunako vituo kadhaa vya redio kwa kuwa wameguswa na janga hilo huku wakiitaja ‘Hip Hop Against Albino Violence’ kama kauli mbiu ya mapambano hayo.

“Wimbo huo utakuwa kwenye lugha mbili, yaani Kiswahili na Kingereza ili uende kimataifa zaidi. Sisi kama Kikosi tunaungana na serikali yetu katika kulikemea hili, kama tulivyopigana vita kuhusu utumiaji wa dawa za kulevya kupitia kauli mbiu, ‘Hip Hop Bila Madawa’,” alisema Kalapina. ShowBiz inawaunga mkono wasanii hao kwa kuwatakia mafanikio katika harakati hizo.
*********
Jhiko Man. Duh! Albam ya 9
Kati ya wasanii wachache wa muziki wa Reggae Bongo ambao wanaendelea kufanya ‘ubishi’ kwenye game hiyo ni pamoja mchizi kutoka pande za Bagamoyo, Pwani, Jhiko Manyika ‘Jhikoman’, kitu ambacho kiliifanya ShowBiz wiki hii iinue simu, kumuendea hewani na kupiga naye stori mbili tatu ambapo alisema kwamba, mwishoni mwa wiki hii anatarajia kutambulisha albamu yake ya tisa yenye jina la ‘Yapo’, tangu alipoingia kunako game ya muziki huo.

Jhiko alitamka kwamba, albamu hiyo ambayo imefanyika chini ya lebo ya Udu Mood aliyoingia nayo mkataba, itaanza kutambulishwa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii katika ukumbi wa Malaika, ikifuatiwa na sehemu nyingine kama Moshi, Arusha, Zanzibar, kisha kumalizia nyumbani kwao Bagamoyo.

“Ndani ya albamu hiyo yenye nyimbo 15 nimefanya vitu tofauti, siyo kama watu walivyozoea kusikia Reggae tupu kutoka kwangu, bali nimefanya muziki wa Kiafrika zaidi kwa kuwashirikisha wasanii wanne kutoka Finland ambao pia nitakuwa nao kwenye ziara ya uzinduzi mwanzo hadi mwisho. Baadhi ya kazi zinazopatikana ndani ya albamu hiyo ni Ubatili, Yapo, Nyerere, We nenda na nyingine,” alisema Jhiko.
*****

No comments: