
Hatimaye shindano jipya kabisa na la kijanja ‘Dar es Salaam Hands Up’ (Dar es Salaam Mikono Juu), tayari limeanza na hawa ndio wakali wa muziki wa Bongo Flava waliotajwa kuiwakilisha Wilaya ya Kinondoni kunako mpambano huo kama tulivyowaomba wasomaji wiki iliyopita.
Wasanii hao kutoka pande za Kinondoni ni Jaffarai, Ray C, Prof. Jay, Fid Q, Kalapina (Kikosi cha Mzinga), A.Y, Mr. Nice, Ngwea, Witness na K-Sher. Nakukumbusha tena, shindano hili linazihusu Wilaya tatu za Dar es Salaam, Kinondoni, Ilala na Temeke ambapo wewe msomaji na mpenzi wa burudani hii utatuambia ni ipi ina wasanii wakali. Baada ya kuwapata wakali kumi kutoka Kinondoni, sasa tunaigeukia Wilaya ya Ilala.
Unachotakiwa kufanya kwa sasa kabla hatujaingia kwenye zoezi kubwa la kuzipigia kura wilaya ni kututajia jina la masanii ambaye unadhani anafanya vyema ndani ya Wilaya ya Ilala kwa kuandika ujumbe mfupi (SMS) ukilitaja jina lake kisha tuma kwenda simu namba 0787-110 173. Kumbuka kwamba kila wilaya itawakilishwa na wasanii kumi.
***********

Miss Utalii 2006-2007, Consolata Rushau ambaye pia ni mwalimu wa shule moja ya msingi Mkoani Tanga, ameonesha yuko karibu zaidi na fani hiyo kwa kuwapeleka wanafunzi wake kunako makumbusho ya mapango ya Amboni yaliyopo mkoani humo kila anapopata nafasi, Imelda Mtema alipiga naye stori.
Akisema na ShowBiz alipotembelea ndani ya ofisi zetu zilizopo Sinza, Bamaga, Dar es Salaam hivi karibuni, mrembo huyo alitamka kwamba, japo amebahatika kuwa mwalimu, mambo ya utalii yako kwenye damu yake na ndio maana hupenda kuwapeleka wanafunzi wake ili wafahamu zaidi mambo ya kiutalii.
“Urembo ni sehemu ya maisha yangu, nafikiria kuwa mwanamitindo maarufu, japo kuna fani nyingine nazipenda kama uigizaji wa filamu na nyingine. Bado sijakata tamaa wala sijaridhika na taji nililonalo, naendelea kutafuta nafasi nzuri zaidi katika tasnia ya urembo ili nifikie levo za kina Naomi Campbell,” alisema.
*******

Ukiisikiliza ngoma yake mpya, ‘Mungu yuko bize’ unaweza kudhani kwamba, mchizi sasa anaelekea kwenye wokovu ukizingatia kuwa siku hizi pia hupendelea kutoka ‘kipapaa’, yaani kiutu uzima, mashati ya mikono mirefu na tai shingoni kitu ambacho yeye binafsi hajaweka wazi.
Namzungumzia kijana kutoka pande za Tanga, Joseph Rushahu ‘Bwana Misosi’ ambaye baada ya kuisikia kazi hiyo mpya tuliamua kumtafuta ili kujua nini hasa kimemsukuma akaamua kutoka na ngoma hiyo iliyomshirikisha mwana TMK Family, Said Juma ‘Chegge’.
“Mungu yuko bize’ ni sanaa tu, si vinginevyo ila ni kazi ambayo iko pande zote na kwa madhehebu yote haijambagua mtu. Kuna baadhi ya binadamu huwa wanajifanya wako bize zaidi wakati Mungu yuko ‘bize’ zaidi. Kuhusu mavazi, Misosi nimeshakuwa mtu mzima, ndiyo sababu iliyonifanya nikanyoa rasta zangu,” alisema Misosi.
********
No comments:
Post a Comment