Monday, March 23, 2009

WIKIENDA SHOWBIZ!

Bushoke kujiachia Bukoba Pasaka
Akiwa bado anaendelea kupiga kitabu ndani ya Chuo cha Sanaa Bagamoyo, Mkoani Pwani, msanii Ruta Maxmiliani Bushoke ‘Bushoke’ anatarajia kuendelea na ziara ya utambulisho wa albamu yake, ‘Dunia njia’ pande za Bukoba, siku ya Sikukuu ya Pasaka.

Akipiga stori na safu hii, Bushoke alisema kwamba akiwa Bukoba, Mkoani Kagera ataangusha shoo mbili mfululizo akianzia ndani ya Ukumbi wa Linas Pub siku ya Pasaka ambapo kiingilio kitakuwa ni shilingi 10, 000 (VIP) na 5, 000 kawaida, ikifuatiwa na ndani ya Uwanja wa Kaitaba siku itakayofuata kiingilio kikiwa ni buku moja kwa kila kichwa.

“Katika msafara huo nitakuwa na baadhi ya wasanii ambao nilizunguka nao mwanzo katika uzinduzi wa albamu hiyo, ambao ni Ngwea, Blue, Maunda Zorro na wengine kibao ambao nitawataja hivi karibuni. Watu wa Bukoba na sehemu za jirani wajitokeze kwa wiingi siku hiyo ili tule sikukuu pamoja,” alisema Bushoke.
**********

Hemedi apata dili Mr. HB
Baada ya ‘kuhaso’ huku na kule akitafuta kutoka, msanii Hemedi Suleiman aliyepitia kunako shindano la ‘Tusker Project Fame’ na kuambulia za uso, sasa ameanza kula matunda ya jasho lake nikimaanisha kuwa, ngoma yake mpya ‘Unachotaka ni mapenzi’ imempa dili la kupiga shoo kunako shindano la kumtafuta Mr. Handsome litakalofanyika Machi 28, mwaka huu, Imelda Mtema anajiachia nayo.

Mratibu wa mpambano huo, Methuselah Magese alisema na safu hii kwamba, Hemedi ni miongoni mwa wasanii chache waliopata bahati ya kusimama katika jukwaa la mpambano huo ambao utapigwa katika Hoteli ya New Africa, Dar es Salaam.

“Katika shindano hilo ambalo litawakutanisha vijana watanashati zaidi ya kumi majaji watakuwa ni Nasreen Kareem, Big Brother 2007, Richard Bezuedenhout na Steven Kanumba,” alisema Magese.
***********

Kikosi kutambulisha 3 na studio yao mpya
Kutoka pande za Kinondoni, Dar es Salaam, kundi la muziki wa Hip Hop lenye jina la Kikosi cha Mizinga linaloongozwa na msanii Kalama Masoud ‘Kalapina’ linatarajia kudondoka ndani ya Ukumbi wa Msasani Club na kutambulisha ngoma zao mpya pamoja na studio yao waliyoipa Kikosi Records, Edna Katabalo anashuka nayo.

Akipiga stori na safu hii, Kalapina alisema kwamba, tukio hilo kubwa litafanyika ndani ya Ukumbi wa Msasani Club, siku ya Pasaka na nyimbo watakazotambulisha ni Pamoja na Pata potea na Hip Hop Agaist Albino.

“Ngoma zote tutakazotambulisha siku hiyo zimetengenezwa ndani ya studio yetu, Kikosi Records, mashabiki wajitokeze kwa wingi ili tuungane katika vita dhidi ya mauaji ya albino ambayo tumeianzisha kupitia sanaa yetu.
**********

No comments: