Monday, March 30, 2009

WIKIENDA SHOWBIZ!

Dar es Salaam Hands up
Baada ya kuwapata mastaa wa Bongo Flava watakao iwakilisha Wilaya ya Ilala (PICHANI JUU) kupitia shindano la kijanja, ‘Dar es Salaam Hands Up’ (Dar es Salaam Mikono Juu) linaloendeshwa na Gazeti la Ijumaa linalotoka kila siku ya Ijumaa kupitia safu yake ya burudani, ‘ShowBiz’ sasa ni zamu ya Temeke.

Unachotakiwa kufanya wewe msomaji na mpenzi wa mpambano huo ni kutuma ujumbe mfupi (SMS) ukimtaja msanii wa Bongo Flava ambaye unadhani anastahili kuiwakilisha Wilaya ya Temeke katika shindano hilo kisha tuma kwenda simu namba 0787-110 173.

Kumbuka wewe msomaji na mpenzi wa burudani Bongo ndiyo jaji wa mpambano huo ambao tayari umeanza kuvuta hisia wa watu wengi.
**********************************
Jade; Enzi za uhai wake Aliwahi kujiachia na wanaume hawa!
Leo ndani ya ‘Ebwana Dah!’ tunamuangalia mrembo aliyejipatia umaarufu kupitia Shindano la Big Brother lililofanyika nchini Uingereza 2002, Marehemu Jade Goody aliyefariki hivi karibuni kwa ugonjwa wa kansa.

Kwa mujibu wa mtandao unaodili na uhusiano wa kimapenzi wa mastaa wa Ulaya, enzi za uhai wake, Jade aliwahi kujiachia na mastaa wa kiume watatu akiwemo Jack Tweed aliyefunga naye ndoa siku chache kabla ya kifo chake ambaye hivi sasa anaonekana kuchanganyikiwa kwa msiba huo mzito japo alifahamu mkewe atafariki dunia.

Kabla hajakutana na Jack, Jade alianza kujirusha na kijana Jeff Brazier, mwaka 2002 kabla hajadondokea katika penzi la Ryan Amoo mwaka 2005, ambaye baadaye waliachana na kuanzisha uhusiano na Jack. Jade ambaye alifariki dunia Machi 22, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 28 ameacha watoto wawili wa kiume.
************************************
Suma Lee: Park Lane limebaki jina tu
Kutoka pande za Tanga msanii, Ismail Sadiq ‘Suma Lee’ ambaye ni mmoja kati ya wasanii wawili waliokuwa wanaunda kundi la ‘Park Lane’ hivi karibuni amechomoka upya na ngoma yenye jina la ‘Ndani ya One Week’ na kutamka kwamba, ule uvumi ulioenea kuwa aliamua kurudi nyumbani kwao Tanga baada ya kushindwa game hauna ukweli wowote, bali alitokomea kwenye mishemishe nyingine za kutafuta maisha.

Mchizi ambaye mwishoni mwa wiki iliyopita alidondoka ndani ya safu hii akiwa na afya tele na muonekano mpya, alisema kuwa huo ulikuwa ni uvumi tu, sasa amerudi upya kama yeye na kwamba ndoto za kulirudisha kundi lao la Park Lane haipo tena.

“Kundi lina raha yake na matatizo yake, lakini mtu ambaye hafahamu hawezi kujua, hivi sasa hatuna mpango wa kurudi kama kundi, kila mmoja ataendelea kupiga ishu zake kama yeye. Mimi na Cpwaa huwa tunakutana club na kupiga stori za kawaida tu siyo kuhusu kundi, kinachoendelea kwangu ni ujio wa albamu itakayokuwa na jina la ‘Hesabu za mapenzi’ na jumla ya ngoma kumi, baada ya ‘Ndani ya One Week’ nitaachia kazi nyingine yenye jina la ‘UK Dubai’ iliyofanyika kupitia studio za MJ Records.
**************************************
Mnyalu kuendeleza mpambano wa Inspector na Mwana FA
Msanii Mike Mwakatundu a.k.a Mike T au Mnyalu ambaye hivi karibuni aliachana na ukapera kwa kufunga ndoa na mchumba wake wa siku nyingi ameibuka na kuendeleza malumbano yaliyoanzishwa na Inspector Haroun aliyejibu wimbo wa Mwana FA, ‘Bado nipo nipo’, Chile Kasoga anashuka nayo.

Akipiga stori na safu hii, Mike T alisema kwamba, wimbo wake mpya wenye jina la ‘Wala wasielewe’ aliomshirikisha Mwana FA aliyeimba wimbo wa ‘Bado nipo nipo’ unawazungumzia wana ndoa ambao huzisaliti ndoa zao na kutafuta wapenzi wengine wa pembeni.

“Kwa kifupi nataka kuleta changamoto kwa wasanii wengine waliowahi kufanya nyimbo za aina hiyo wakiwemo Mwana FA na Inspector Haroun, sipendi watu wanifikirie vibaya kwa kuwa yote ni sanaa tu na si vinginevyo,” alisema Mnyalu.
***************************
Maunda, Mwasiti kumtoa Bushoke Pasaka
Kutoka katika familia yenye vipaji vya muziki, msanii Maunda Zorro (PICHANI JUU) na Mwasiti Almasi ndiyo wasichana pekee watakaompiga tafu Rutta Maximilian ‘Bushoke’ kutoka Zizzou Entertainment katika uzinduzi wa albamu yake, ‘Dunia njia’ utakaopigwa ndani ya Ukumbi wa Linas Pub uliyopo mjini Bukoba siku ya Sikukuu ya Pasaka.
Akisema na safu hii, Bushoke alitamka kwamba, mbali na mabinti hao, wasanii kama Ngwea, Blue, Steve na wengine kibao wataungana naye katika zoezi hilo la utambulisho wa albamu yake yenye takribani ngoma kumi na moja.
“Shoo ya pili tutaangusha ndani ya Uwanja wa Kaitaba siku itakayofuata, tunategemea kupata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wa Bukoba ukizingatia hiyo itakuwa mara yetu ya kwanza kudondoka pande hizo. Viingilio katika shoo hizo vitakuwa ni shilingi 10, 000 Linas Pub na 5,000 Kaitaba,” alisema Bushoke.
**********************************

No comments: