Kwa mujibu wa watafiti wa ugonjwa wa kansa (saratani), asilimia 30 ya watu wanapatwa na ugonjwa huo kutokana na kukosa kula vyakula sahihi. Lishe bora na vyakula sahihi ndiyo silaha yenye nguvu kubwa kupambana na ugonjwa wa saratani ambao umeonekana kuwa tishio kubwa duniani, zikiwemo nchi tajiri.
Vyakula vyenye uwezo mkubwa wa kutoa kinga mwilini dhidi ya aina nyingi za saratani, vinatokana na mimea ya asili, nafaka, matunda na mboga za majani. Ni jambo linalowezekana kwa binadamu kutumia vyakula hivi ili kujikinga na madhara ya ugonjwa huu hatari.
Inajulikana kuwa ugonjwa wa kansa ni hatari na mtu akishaupata hauna tiba. Tumeona au kusikia watu matajiri, wenye uwezo mkubwa wa kifedha, wameugua na hatimaye kufariki dunia kutokana na maradhi ya kansa.
Mfano hai wa hivi karibuni, ni wa mwanadada maarufu wa Uingereza, Jade Goody, ambaye alikufa kutokana na ugonjwa wa kansa ya kizazi, licha ya umaarufu na uwezo wa kifedha aliokuwa nao, hakuweza kutibiwa na kupona.
Hakuna kinga bora dhidi ya saratani zaidi ya kula vyakula sahihi vinavyoshauriwa na wataalamu wetu wa masuala ya afya. Ili mtu ujiepushe na hatari ya kupatwa na saratani, unatakiwa kula matunda na mboga kila siku, kwa kiasi cha angalau kisahani cha chai kimoja hadi visahani vitano vya matunda mchanganyiko na mboga.
Kwa bahati mbaya sana, utafiti unaonesha kuwa ni watu wachache sana wasiozidi asilimia 20 ndiyo wanaokula kiwango cha matunda na mboga kinachoshauriwa na mamlaka za afya.
Utafiti huo umefanyika katika nchi iliyoendelea kama Marekani na bila shaka kwa nchi masikini kama yetu, hali inaweza kuwa mbaya zaidi na ndiyo maana idadi ya wagonjwa wa saratani imekuwa ikiongezeka katika hospitali zetu kila siku.
Kuthibitisha umuhimu wa matunda na mboga, hivi karibuni Taasisi ya Saratani ya Taifa (NCI) nchini Marekani ilikubaliana na taarifa isemayo: “Mlo mwingi wa matunda na mbogamboga unaweza kupunguza hatari ya kupata baadhi ya kansa na magonjwa mengine hatari”. Ingawa ni dhahiri kuwa vyakula vyote vitokanavyo na mimea vina vitamini, madini na ‘enzymes’ muhimu kwa mtu kuwa na afya bora, ni watu wachache sana wanaovijali vyakula hivyo.
Katika makala haya, tutaangalia orodha ya vyakula vinavyoongoza kwa kuwa na virutubisho vingi vyenye uwezo wa kutoa kinga madhubuti dhidi ya saratani mbalimbali, kama vilivyoainishwa na wataalamu wa masuala ya afya:
1.NYANYA
Inaelezwa kuwa nyanya inaongoza katika orodha ya mboga zenye virubisho vyenye uwezo wa kuzuia kansa kutokana kuwa na kiwango kikubwa cha kirutubisho kijulikanacho kwa jina la ‘lycopene’.
Kirutubisho hicho kimeonesha uwezo mkubwa wa kupunguza hatari ya mtu kupatwa na kansa ya kibofu (prostate) na Kansa ya kizazi. Nyanya pamoja na bidhaa zake zote zina manufaa makubwa kwa kinga dhidi ya saratani hiyo.
2.BROKOLI (BROCCOLI)
Brokoli ni aina fulani ya mboga za majani jamii ya kabichi ambazo maua yake huliwa. Mboga hii inapatikana kwa wingi nchini Tanzania, hasa katika masoko ya Kariakoo, kisutu na kwingineko. Mboga hii ni chanzo kizuri cha kirutubisho aina ya ‘sulforaphane’ ambacho huondoa hatari ya mtu kupatwa na saratani ya tumbo, matiti na ngozi. Halikadhalika kabichi nayo ni muhimu katika kundi hili.
3. MAHARAGE YA SOYA
Kama ulikuwa unadhani maharage ya soya (Soyabeans) ni mlo wa kimasikini, kuanzia sasa ondoa dhana hiyo, kwani jamii hii ya maharage ambayo Tanzania inapatikana kwa wingi pia, ni chanzo kikubwa cha kirutubisho kiitwacho ‘Isoflavones’ ambacho humuondolea mlaji hatari ya kupatwa na saratani ya matiti na kibofu.
Itaendelea wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment