Friday, May 8, 2009

IJUMAA SHOWBIZ!

Jaffarai: Game gumu, wakongwe wajipange
Kutoka pande za Makumbusho, Dar es Salaam katikati ya wiki hii, ShowBiz ilipata kupiga stori na msanii Jafari Ally Mshamu a.k.a Jaffarai ambaye bado anang’aa na ngoma yake ‘Napenda nini’ ambapo alitamka kwamba wasanii wengi wa Bongo Flava waliowahi kukimbiza siku za nyuma wanashindwa kurudi kwenye game kwakuwa hawajipangi.

Msanii huyo alisema kwamba, ili msanii uweze kurudi vizuri kwenye game baada ya kukaa kimya muda mrefu inabidi ujipange kwa kufanya kazi bora vinginevyo kila ukitaka kutoka unapotea tena kwakuwa game la muziki hivi sasa imekuwa na changamoto kubwa hasa kutoka kwa chipukizi wengi wanaoibuka kunako tasnia hiyo.“Si unaona mimi ninavyofanya kazi zangu, huwa nakaa muda mrefu bila kusikika, lakini ninaporudi nakuwa kivingine zaidi kitu ambacho kinaendelea kuniweka juu. Wasanii wenzangu wa kitambo ambao wapo kimya kwa muda mrefu na wanaotamani kurudi kwenye game letu wajaribu kufanya kazi zenye ubora ambazo zitawafanya waonekane wapya,” alisema Jaffarai.

Kuhusu game lake la muziki, Jaffarai alisema kwamba, kinachofuata baada ya kutoka na ngoma yake, ‘Napenda nini’ aliyomshirikisha Fatma ni ngoma yenye jina la ‘Saa Nyingine’ ambayo pia imefanyika kupitia studio za Fish Crab chini ya ‘prodyuza’ Lamar. “Ndani ya ngoma hiyo nimemshirikisha Naaziz kutoka Kenya, huo utakuwa ni utambulisho wa albamu yangu mpya yenye jina la ‘Wali Nazi’ itakayokuwa na jumla ya kazi kumi zikiwemo Msijisahau, Jaffaryhmes, Saa Nyingine, Napenda Nini na nyingine kibao”.

Pia mchizi alisema kwamba, akiwa ni mmoja kati ya wakali wa muziki huo wanaounda kundi la ‘Wateule’, siku chache zilizopita wameachia wimbo mpya wa kundi ambao unakwenda kwa jina la ‘Msela’ ukiwa pia ni utambulisho wa albamu yao ambayo pia imekamilika. “Kazi tumefanya mimi, Mchizi Mox, Jay Moe na Solo Thang ambaye bado yuko Uingereza,” alisema.
*************************************
Kassim naye atokea Mombasa
Wimbi la wasanii wa muziki wa kizazi kipya kutimkia Mobasa, Kenya ambalo kila kukicha huzidi kuongezeka pia limemkumba mkali wa staili ya kubembeleza, Kassim Maganga kutoka ndani ya familia ya Tip Top Connection ambaye hivi karibuni amedondoka na video ya ngoma yake mpya ‘Sijali’.

Akipiga stori na ShowBiz, meneja wa familia hiyo, Babu Tale alisema kwamba, video hiyo imefanyika Mombasa chini ya mtayarishaji John Kallaghe lengo kubwa likiwa ni kutanua soko la muziki wao. Mbali na video hiyo, Kassim pia ameachia redioni wimbo uliyobeba jina la albamu yake wenye jina la ‘Usiende kwa mganga’.

Wasanii wengine wa Bongo Flava ambao hupenda kufanyia kazi zao Mombasa ni pamoja na Q-Chillah, Matonya, Z-Anto na wengine.
************************************
Wachaji zote wasambaratika
Wale ‘madogo’ waliowahi kutoka na ngoma kadhaa zikasikika kupitia baadhi ya vituo vya redio, ‘Wachaji zote’ wametengana huku kila mmoja akiamua kupiga ishu zake. ShowBiz ilipata nafasi ya kucheki na mmoja wa wasanii wa kundi hilo, Herry Willbard a.k.a Mtoto wa Binti Makombora au ‘Mchaji’ ambaye alikiri kutokea kwa upepo huo mbaya, Rhobi Chacha anashuka nayo.

“Binafsi sikujua kilichotokea au kilichomsibu mshikaji wangu, kwanza alisafiri kwenda kwao Morogoro, aliporudi akaniambia yeye ameamua kuachana na muziki na kwamba anakwenda kipiga ishu nyingine. Kiukweli nilijisikia vibaya lakini kwa kuwa mimi muziki bado upo kwenye damu nikaamua kukomaa mpaka nikafanikiwa kupata lebo kupitia studio za Apex zilizopo Mburahati, Dar es Salaam. Tayari nimefanya kazi kadhaa ikiwemo ‘Utarudi’ ambayo iko hewani kupitia baadhi ya vituo vya redio,” alisema Mchaji.
******************************************
MPAMBANO WA WAKALI WA WILAYA: Ngoma droo
Ndani ya mpambano huu wa kijanja, Dar es Salaam Hands Up (Dar es Salaam Mikono Juu) ambao unazishirikisha wilaya tatu za mkoa wa Dar es Salaam, wiki iliyopita tulishuhudia Wilaya ya Ilala ikitolewa baada ya kuambulia kura chache kutoka kwa wasomaji na wapenzi wa mpambano huu ambao ndiyo majaji. Leo hakuna aliyetoka kati ya Temeke na Kinondoni kwakuwa wameambulia kura sawa, yaani ‘ngoma droo’.

Kwa matokeo hayo tunawaomba muendelee kutuma kura zenu mkituambia ni wilaya ipi kati ya Kinondini na Temeke yenye wasanii wakali wa muziki wa kizazi kipya. Shindano hili ambalo limetokea kuwavutia wapenzi wengi wa burudani karibu nchi nzima pia limepongezwa na baadhi ya wasomaji ambao wamedai kuwa ni ubunifu wa hali ya juu ambao utaleta changamoto kwa wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya.

Ili wilaya moja iibuke na ushindi kati ya Kinondini na Temeke, unachotakiwa kufanya msomaji ni kuandika ujumbe mfupi (SMS) ukitaja jina la wilaya ambayo unadhani ina wasanii wakali kisha tuma kwenda simu namba 0787-110 173.

Compiled by mc george

No comments: