Tuesday, May 5, 2009

Mambo 5 ya kukuepusha na kisukari


UGONJWA wa kisukari ni miongoni mwa magonjwa hatari na yaliyoenea duniani. Ni ugonjwa ambao ukiupata hauna tiba na mara nyingi huua iwapo utashindwa kujua kanuani za kuishi nao. Wataalamu wanauita ugonjwa huu kama ‘lifestyle disease’ kutokana na ukweli kwamba staili yako ya maisha ndiyo inayoweza kusababisha ukaupata au ukauepuka.

Taarifa mbaya zaidi kuhusu ugonjwa huu ni ukweli kwamba kisukari kimekuwa si ugonjwa wa watu wazima pekee, bali sasa hata watoto na vijana wadogo wanaugua.
Utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa Desemba mwaka jana na Jarida la Diabetes Care umeonesha kuwa vijana wengi wa kati ya miaka 10-29 wanaugua ugonjwa wa kisukari kwa kasi kubwa duniani na kwamba unagharimu mabilioni ya dola kama gharama za matibu kwa wagonjwa.

Hivyo, ili kujiondoa katika hatari ya kupatwa na ugonjwa huu, ni vyema kuzingatia kanuni za ulaji na kula vyakula sahihi, kwani hiyo ndiyo kinga pekee na hakuna kinga ya vidonge wala sindano. Yafutayo ni mambo MATANO rahisi ya kubadili staili ya maisha yako ambayo yatapunguza uwezekano wa kupata kisukari (type II) na pengine kutougua kabisa;

1. Pendelea kula vyakula vyenye kiwango kikubwa cha ufumwele (fibre) na utumiapo mafuta, tumia yale yatokanayo na mimea na mboga (polyunsaturated fats), kama vile alizeti, ufuta, nazi, n.k badala ya kutumia mafuta yatokanayo na wanyama.

Vyakula vyenye kiwango kikubwa cha ufumwele ni pamoja na maharagwe, mahindi, ngano, soya, ndizi mbivu, maparachichi, matufaha (apples), n.k.

2. Kula kiasi kidogo sana cha vyakula vilivyopikwa kwa mafuta, hasa yale yatokanayo na wanyama na bidhaa zitokanazo na maziwa (transfats) ambayo kiafya siyo mazuri sana. Ukila kwa tahadhari mafuta haya yanayoongeza kolestro mwilini, utajiepusha pia na ugonjwa wa shinikizo la damu.

3. Kama wewe ni mvutaji wa sigara, acha. Moja ya staili ya maisha inayochangia mtu kupatwa na ugonjwa wa kisukari ni pamoja na uvutaji wa sigara. Licha ya athari hiyo, athari nyingine ya sigara inajulikana kuwa ni ugonjwa wa kansa.

4. Halikadhalika, kama wewe ni mnywaji wa kilevi (alcohol), punguza kiwango unachokunywa. Wastani unaokubalika kiafya ni ule usiozidi glasi mbili kwa siku, unywaji wa kupindukia ni hatari kwa afya yako kwa ujumla na ukiweza kuacha kabisa unywaji wa pombe, ni bora zaidi.

5. Mwisho kabisa, dhibiti uzito wako na kama tayari ni mnene, punguza uzito hadi ufikie kiwango kinachokubalika kulingana na urefu ulionao. Unaweza pia kuujua wastani wa unene wako kama unakubalika ama la kwa kupima saizi ya kiuno chako.

Kwa mwanamke mwenye uzito wa kawaida, saizi ya kiuno chake hakitakiwi kuzidi inchi 34 na mwanaume hatakiwi kuzidi inchi 36. iwapo unavaa suruali au sketi zaidi ya saizi hiyo, basi unashauriwa kuanza kuchukua hatua za kupunguza unene ili kujiepusha na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari ambao ukishaupata hauna tiba.

Kutokana na maombi ya wasomaji wengi, panapo majaaliwa wiki ijayo nitawaletea tena makala kuhusu ‘dayati’ anayopaswa kula mtu ambaye tayari ana ugonjwa wa kisukari.

1 comment:

Anonymous said...

ahsante sana kwa maada hii uliotuletea ukweli nimejifunza nini cha kufanya.