Friday, June 26, 2009

IJUMAA SHOWBIZ!


MKALI WA MWEZI (MONTHLY BEST PERFORMER Ikiwa leo ni Ijumaa ya mwisho kwa mwezi huu, kupitia shindano hili, msanii Lawrance Malima ‘Marlaw’ ametajwa kuwa bora mwezi huu (Juni) kwa kupata kura nyingi zilizotumwa na wasomaji wa safu hii.
Msanii huyo ambaye hivi sasa anafanya vyema na ngoma yake, ‘Pii pii’ amepigiwa kura nyingi zaidi na wasomaji na wapenzi wa burudani Bongo kuliko mastaa wengine tisa waliotajwa kuingia kwenye shindano hili ambalo kila mwezi litakuwa likimpata staa bora kupitia kura za wasomaji.
ShowBiz inatoa pongezi kwa Marlaw, huku ikielekeza mashambulizi katika kumpata mshindi wa Julai . Namba zetu ni zilezile 0787 110 173, tutumie SMS.
********


BABY BOY
Baby Boy, msanii kutoka Bukoba ni kichwa kingine kinachopatikana katika lebo ya Zizzou Entertainment inayokamilishwa na wasanii wengine kama Ngwea, Blue, Bushoke, Steve na wengine ambaye alisema na ShowBiz kwamba muda wake umefika.

Ndani ya safu hii dogo alisema kwamba, ‘Tunapendana’ ndiyo kazi yake mpya itakayompa nafasi katika mradi wa muziki wa kizazi kipya na kulifanya jina lake liwe juu kama walivyo mastaa wengine niliowataja hapo juu.

“Naamini ni kazi itakayonitambulisha vyema katika game ya muziki Bongo, naishukuru Zizzou Entertainment kwa kukiona kipaji changu na kunipa nafasi,” alisema Baby.
*******
CHEGGE MENO NJE
Anayo kila sababu ya kutabasamu kama siyo kucheka kwasababu aliiambia ShowBiz kwamba, baada ya kukesha kwa takribani siku kadhaa amefanikiwa kukamilisha video ya ngoma yake mpya, ‘Karibu Kiumeni’.

Mchizi ambaye kundini kwake anasifika kwa kuzisimamisha ngoma kadhaa kwa korasi alisema kwamba, ilimchukua takribani siku kadhaa, usiku na mchana kupiga video ya wimbo huo ambao hivi sasa una-bang kupitia vituo kadhaa vya redio.

“Video hiyo tayari imeshakamilika na nimeshaisambaza kupitia vituo kadhaa vya televisheni, lakini furaha yangu itaongezeka mara dufu siku nikifanikiwa kukamilisha albamu yangu mpya itakayokuwa na ngoma kumi na bee ambayo itawashirikisha atisti kibao kutoka nje ya TMK Wanaume Family,” alisema Chibunda a.k.a Mtoto wa Mama Said.
****** *************

KALA: SIKUWAKWEPA MAFISADI NIMERUDI NA WIZI MTUPU
Mwana Hip Hop, Kala Jeremiah ni miongoni mwa wakali wa Bongo aliyeibukia ndani ya ShoBiz wiki hii na kupiga stori mbili tatu kuhusiana na kupotea kwake tangu alipoacha maswali mengi kwa mashabiki na wadau wa burudani Bongo kupitia ngoma yake, Tanzania aliyomshirikisha Nakaaya Sumari.

Dogo alisema kwamba, siyo kuwa aliwakimbia mafisadi aliyowachana kwenye Tanzania, bali alikuwa chimbo akitengeza matraki mengine ya kijanja ambayo baadhi yake aliibuka nayo kunako safu hii kama ushahidi.

“Hapa nina ngoma mbili ambazo zipo kwenye audio na video, ‘Ushamjua’ niliyomshirikisha ‘Noorah’ na ‘Wizi mtupu’ ambazo siku chache zijazo zitakuwa hewani kupitia redio na televisheni”.

ShowBiz ilipata bahati ya kuzikiliza na kuziona kazi hizo na kugundua kwamba, kila kukicha uwezo wa msanii huyo kutoka pande za Mwanza unazidi kuwa juu kwani alichokifanya ni mapinduzi mengine katika game ya muziki wa kizazi kipya.
**********

FAKE SMILE IMEONDOKA MIKONONI MWA WADAU
Muvi ya Fake Smile iliyochezwa na mastaa wa ukweli waliojiajiri kupitia sanaa hiyo, imedondoka kitaani ikiwa ndani ya DVD, VCD na VHS, hiyo ni kauli ya mmoja kati ya wadau wa kazi hiyo, Steven Kanumba.

Akipiga stori na ShowBiz hivi karibuni jijini Dar, Kanumba alisema kwamba sababu kubwa iliyowafanya washindwe kuidondosha sokoni mapema kama walivyoahidi hapo awali ni baada ya kuipeleka nchini Malaysia kwa ajili ya kuifanyia ‘editi’ ili iwe ya kimataifa zaidi.

“Unajua baada ya kukamilisha zoezi la kupiga picha hapa Bongo, tuliituma Malaysia kwa ajili ya kuiboresha na kuifanya iwe katika kiwango cha kimataifa, ili kazi zetu ziende mbali zaidi,” alisema Kanumba.
*********

ZIFF KUWAKUTANISHA MASTAA KIBAO KESHO
Tamasha la Ziff ambalo litaanza kesho Visiwani Zanzibar, linatarajiwa kupamba na burudani za kutosha zikiwemo shoo kutoka kwa wakali wa muziki wa Bongo Flava.

ShowBiz ilidondoshewa ishu na waandaaji kwamba, mbali na washereheshaji wa Kibongo, pia kutakwa na shangwe zaidi kutoka pande za nje, namzungumzia mkali wa muziki wa reggae aliyepata kutamba miaka ya nyuma, Alpha Blondy.

Kutoka Bongo, wasanii kama Mwasiti Almasi, Mrisho Mpoto, Khadija Shaaban ‘K-Sher’ na Kassim Maganga watapanda stejini na kugonga shoo katika tamasha hilo. Pia vikundi mbalimbali kutoka Mexico, India, Zimbabwe, Kenya na Comoro tayari vimekwishatia timu eneo la tukio kwa kwa ajili ya kuipaisha Ziff matawi ya angani.
********
compiled by mc george








No comments: