Tuesday, September 22, 2009

LISHE YA WAGONJWA WA MOYO


HAKUNA kitu muhimu kwa mtu mwenye matatizo ya kiafya kama kujijua aina ya mlo anaopaswa kula na kutokula. Watu wengi wanasumbuliwa na maradhi sugu, kama vile ‘presha’, vidonda vya tumbo, magonjwa ya moyo, n.k, lakini hawajui mlo wanaopaswa kula au kutokula.

Katika makala ya leo, ambayo inarudiwa kwa mara ya pili baada ya kuombwa na wasomaji wengi, tunaangalia aina ya vyakula anavyopaswa kula mwenye ugonjwa wa moyo, ambavyo vinaweza, ama kudhibiti hali yake isiendelee kuwa mbaya ama kuponya kabisa, hali kadhalika kuepuka vyakula ambavyo akila hufanya hali yake kuwa mbaya zaidi.

ZABIBU: Matunda na mbogamboga kwa ujulma wake, ndiyo vyakula muhimu kwa magonjwa mengi ya moyo, vyakula hivyo vina uwezo wa kudhibiti ugonjwa na kuimarisha moyo, lakini zabibu ndiyo tunda linaloongoza kwa ubora linapokuja suala la kuimarisha afya ya moyo. Ili kupata matokeo mazuri, andaa ratiba maalum ya kula zabibu peke yake kwa siku kadhaa mfululizo, juisi ya zabibu inafaa zaidi na ahueni utakayoipata kutokana na zabibu ulizokula, huonekana mara moja.

APPLE: Tunda lingine lililo bora kwa mgonjwa wa moyo, hasa wenye matatizo ya kuwa na moyo dhaifu, ni epo (apple), pendelea kula epo mara kwa mara, ikiwemo juisi yake na matokeo yake yatakuwa mazuri.

KITUNGUU: Unaweza kukidharau, lakini kitunguu kina faida kubwa kwa mgonjwa wa moyo, wataalamu wetu wamekifanyia uchunguzi na kugundua kwamba kitunguu kina uwezo mkubwa wa kurekebisha mafuta ya kolestro mwilini na kuuweka mwili katika hali yake ya kawaida. Kwa matokeo mazuri, kunywa kijiko kimoja (cha chakula) cha juisi ya kitunguu, kila siku asubuhi kabla ya kula.

ASALI: Asali ina virutubisho vya ajabu sana ambavyo vina uwezo wa kuzuia aina zote za matatizo ya moyo. Inaelezwa kwamba asali ina ng’arisha moyo na kuboresha mzunguruko wa damu mwilini, halikadhalika inaondoa matatizo mengine ya moyo. Kijiko kimoja (cha chakula) cha asali kikitumiwa kila siku mara baada ya mlo, kina uwezo wa kutoa kinga dhidi ya maradhi yote ya mwili.

Baada ya kuvijua vyakula vya mgonjwa wa moyo, ni vyeme pia kuelewa vyakula unavyotakiwa kuviondoa kwenye orodha yako ya mlo wa kila siku, ambavyo ni pamoja na bidhaa zote zitokanazo na unga mweupe, chai, kahawa, sigara, chumvi, sukari na vitu vingine vitamutamu.

Hayo yakizingatiwa, mgonjwa anaweza kuishi na tatizo la moyo pasinakusumbuliwa kwa kiasi kikubwa na hata dawa anazopewa na daktari wake zitafanyakazi vizuri zaidi. Kwa kila ugonjwa ulionao, ni vyema ukajua nini kizuri, nini kibaya kwa afya yako.

No comments: