Friday, February 27, 2009

IJUMAA SHOWBIZ!



...na mshindi ni...
Mambo vipi Tanzania? Leo ndiyo Shindano la Ijumaa Sexiest Girl lililokuwa na msisimko wa aina yake linafikia ukingoni na Wema Sepetu, Irine Uwoya wameingia fainali, kwa ruhusa tuliyopewa na kamati ya maandalizi ya mpambano huu ikiongozwa na Mratibu wake, Oscar Ndauka, tunachukua fursa hii kutamka kwamba, mshindi ni...!

Samahanini sana wasomaji na wapenzi wa shindano hili, kwa mujibu wa mratibu Oscar Ndauka, mshindi amekwishapatikana lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu atatangazwa Ijumaa ijayo, kwani hivi sasa wanaweka mazingira mazuri kwa ajili ya kumtangaza mshindi, ikiwemo kumpatia zawadi.

“Hivi sasa hatutapokea kura tena, tunawashukuru wote waliolifanya shindano hili likafikia ukingoni kwa mafanikio, bila kuwasahau warembo wote walioshiriki kwenye mpambano huu, asanteni sana na kumbukeni kwamba, mwisho wa shindano hili ndiyo mwanzo wa mashindano mengine yajayo,” alisema Ndauka.
********************************
Hermy B Wasanii wengi wanapenda bure
Wiki iliyopita ShowBiz ilikuwa mitaa ya Kinondoni, ndani ya Studio za Bhitz Music Company na kupiga stori mbili tatu na mtayarishaji muziki Harmes Baric Lyimo ‘Hermy B’ ambaye hivi sasa kazi zake ziko juu, nazizungumzia ‘Habari ndiyo hiyo’ ya Mwana FA na A.Y, Bado nipo nipo, Msiache kuongea (Mwana FA) na nyingine kibao.

Hermy ambaye wiki hii ameachia ngoma mpya yenye jina la ‘Leo’ ya kwake Ambwene Yesaya ‘A.Y’ alisema na safu hii kwamba kikubwa kinawakatisha tamaa baadhi ya watayarishaji muziki wakali ni tabia ya baadhi ya wasanii wakiwemo wakongwe kupenda kufanyiwa kazi bure.

“Nafahamu kwamba wasanii wengi wa Bongo wanaanza muziki katika mzingira magumu, lakini siyo wakongwe pia ambao tayari wamekwishafanikiwa. Msanii anakupigia simu anakwambia anataka kufanya kazi na wewe ili akuze jina la studio, wakati kila kifaa kinachotumika studio nimekigharamia. Wasanii wanatakiwa wafahamu kufungua studio ni gharama kubwa, hiyo imewakatisha tamaa baadhi ya ‘maproducer’ wengi, sina haja ya kuwataja majina.

“Kitu kingine ni kwamba, wasanii wenyewe hawapendi kuumiza vichwa kuandika nyimbo nzuri na hata ukiwapa ‘idea’ wanakuwa wabishi kufanya wakati muziki kila siku unabadilika. Hiyo ni sababu mojawapo inayonifanya nisiwe na lebo katika studio yangu zaidi ya kufanya kazi na Mwana FA na A.Y ambao tunaelewana kwa kiasi kikubwa ikiwemo kwenye ishu ya mkwanja.
**************************************

Solo Thang Atanguliza ngoma mpya Bongo
Baada ya kujichimbia pande za Uingereza kwa takribani miaka kadhaa akipiga kitabu, msanii Msafiri Kondo ‘Solo Thang’ amevunja ukimya kwa kurusha ngoma yake moja mpya yenye jina la ‘Travellah’ ili kuwaweka sawa mashabiki wake, kwamba siku kadhaa zijazo atadondoka Bongo. Mengi zaidi kuhusu mchizi endelea kufuatilia ShowBiz.
*****************************
Kikosi cha Mzinga Sasa ni Hip Hop Against Albino Violence
Kutoka ndani ya Kundi la Kikosi cha Mizinga lenye maskani yake Block 41, Kinondoni, Dar es Salaam, ShowBiz imeambiwa na kiongozi wake, Karama Masoud ‘Kalapina’ kwamba limeandaa mapambano dhidi ya watu wanojihusisha na mauaji ya Maalbino.

Ndani ya safu hii, Kalapina alisema kuwa tayari wameandaa wimbo unaopinga mauaji ya Maalbino ambao utaanza kusika hivi karibuni kunako vituo kadhaa vya redio kwa kuwa wameguswa na janga hilo huku wakiitaja ‘Hip Hop Against Albino Violence’ kama kauli mbiu ya mapambano hayo.

“Wimbo huo utakuwa kwenye lugha mbili, yaani Kiswahili na Kingereza ili uende kimataifa zaidi. Sisi kama Kikosi tunaungana na serikali yetu katika kulikemea hili, kama tulivyopigana vita kuhusu utumiaji wa dawa za kulevya kupitia kauli mbiu, ‘Hip Hop Bila Madawa’,” alisema Kalapina. ShowBiz inawaunga mkono wasanii hao kwa kuwatakia mafanikio katika harakati hizo.
*********
Jhiko Man. Duh! Albam ya 9
Kati ya wasanii wachache wa muziki wa Reggae Bongo ambao wanaendelea kufanya ‘ubishi’ kwenye game hiyo ni pamoja mchizi kutoka pande za Bagamoyo, Pwani, Jhiko Manyika ‘Jhikoman’, kitu ambacho kiliifanya ShowBiz wiki hii iinue simu, kumuendea hewani na kupiga naye stori mbili tatu ambapo alisema kwamba, mwishoni mwa wiki hii anatarajia kutambulisha albamu yake ya tisa yenye jina la ‘Yapo’, tangu alipoingia kunako game ya muziki huo.

Jhiko alitamka kwamba, albamu hiyo ambayo imefanyika chini ya lebo ya Udu Mood aliyoingia nayo mkataba, itaanza kutambulishwa Dar es Salaam mwishoni mwa wiki hii katika ukumbi wa Malaika, ikifuatiwa na sehemu nyingine kama Moshi, Arusha, Zanzibar, kisha kumalizia nyumbani kwao Bagamoyo.

“Ndani ya albamu hiyo yenye nyimbo 15 nimefanya vitu tofauti, siyo kama watu walivyozoea kusikia Reggae tupu kutoka kwangu, bali nimefanya muziki wa Kiafrika zaidi kwa kuwashirikisha wasanii wanne kutoka Finland ambao pia nitakuwa nao kwenye ziara ya uzinduzi mwanzo hadi mwisho. Baadhi ya kazi zinazopatikana ndani ya albamu hiyo ni Ubatili, Yapo, Nyerere, We nenda na nyingine,” alisema Jhiko.
*****

Tuesday, February 24, 2009

Ijue ‘Piramidi’ sahihi ya chakula-2

Watu wengi tunakula vyakula ambavyo baadae vinageuka kuwa sumu na kutudhuru bila sisi wenyewe kujijua kutokana na kutokuzingatia ile dira ya vyakula. Hili ndilo suala ambalo kila mmoja wetu anapaswa kulijua na kulizingatia kila inapokuja suala la kula. Kabla hujala chakula chochote, ni vyema ukajua kinafaida gani mwilini mwako na unatakiwa ukile kwa kiwango gani.

NAFAKA (cereals)
Kwa mujibu wa dira ya vyakula, (FOOD PYRAMID) ambayo imependekezwa na wanasayansi wetu maarufu duniani, vyakula vinavyopaswa kuliwa kwa wingi ni vyakula vyote vitokanavyo na nafaka, kama vile ugali, mikate, wali, uji, tambi, n.k.
Katika kundi hili inasisitizwa sana kupenda kula vyakula hivyo kutokana na nafaka halisi ambazo hazijaondolewa virutubisho vyake vya halisi, ili kupata faida inayopatikana kwenye vyakula hivi. Mfano, ugali uliyo bora ni ule uliyotayarishwa kutokana na unga wa mahindi yasiyokobolewa, kwa maana nyingine ugali utokanao na unga mweupe sana hauna virutubisho vya kutosha.

Matayarisho ya vyakula vitokanavyo na nafaka hizo ni muhimu sana, kwani watu wengi huandaa nafaka hizo na katika mchakato hujikuta wanaondoa virutubisho muhimu na kubaki na chakula kisichokuwa na virutubisho muhimu. Kwa mfano kitendo cha kokoboa na kuloweka mahindi kwa muda mrefu huondoa virutubisho vyote muhimu.

Matunda na mboga (Fruits & vegetables)
Vyakula vinavyofuata kwa umuhimu ni matunda na mboga mboga. Vyakula hivi vinatakiwa kuliwa kwa wingi, hasa mboga za majani, wastani wa milo 3-5 kwa siku. (mlo mmoja ni sawa na kisahani kimoja cha chai) na matunda yaliwe wastani wa milo 2 – 4.

Orodha ya vyakula hivi ni muhimu sana katika mwili wa binadamu kwa sababu katika mboga na matunda tunapata kinga ya maradhi mbalimbali yanayoweza kujitokeza iwapo mwili hauna kinga ya kutosha. Hivyo ulaji wa mboga za majani na matunda si umasikini wala anasa, bali ni suala muhimu na ni la lazima katika mwili wa binadamu.

Nyama, Samaki, Maziwa, Mayai
Kundi linalofuatia kwa umuhimu ni vyakula kama vile nyama, samaki, maziwa, mayai, karanga, maharage, n.k. Kundi hili nalo ni muhimu, lakini linahitaji tahadhari katika ulaji wake, hasa kwa upande wa nyama na maziwa. Nyama iliwe kwa kiasi kidogo na iwe ‘steki’ isiyokuwa na chembe ya mafuta (lean meat), kwani mafuta ya wanyama kwa ujumla yana madhara kiafya hivyo haishauriwi kula nyama zenye mafuta.

Kwa upande wa maziwa, tahadhari pia inapaswa kuchukuliwa kwani si maziwa yote ni mazuri kwa afya yako. Maziwa bora kwa afya ni yale yasiyokuwa na mafuta (skim milk) au fat free. Usipende kunywa maziwa aina ya full cream, kwani aina ya mafuta yaliyomo kwenye maziwa hayo si mazuri kwa afya. Kama unaandaa mwenyewe maziwa, engua utandu wa juu (malai) ndiyo unywe maziwa hayo, malai ndiyo kiini cha mafuta mabaya, hivyo yaepuke.

SUKARI NA MAFUTA
Fungu la mwisho ni vyakula vyenye sukari, mafuta aina zote (fats na Oils) na vyakula vingine vitamu vitamu kama vile soda, ice cream, pipi, n.k. Kundi hili la vyakula linapaswa kuliwa kwa uchache sana, kwani mahitaji yake mwilini ni madogo na virutubisho vyake vinaweza kupatikana kwenye makundi mengine ya vyakula, kama mboga na matunda.

Huo ndiyo mpangilio sahihi wa vyakula ambao ukizingatiwa ipasavyo mwili huwa salama na si rahisi kushambuliwa na maradhi. Lakini kwa bahati mbaya sana, ‘piramidi’ hiyo imegeuzwa. Vyakula vinavyotakiwa kuliwa kwa uchache ndiyo vinaliwa kwa wingi na vile vinavyotakiwa kuliwa kwa wingi, vinaliwa kwa uchache! Mwisho kabisa, usiache kufanya mazoezi kila siku!

Monday, February 23, 2009

WIKIENDA SHOWBIZ!


Sarah Mvungi kujitoa kwa Yatima, Wazee

Msanii wa maigizo Bongo ambaye hivi sasa amejikitia zaidi kunako muziki wa Injili, Sarah Mvungi (pichani juu) amesema na safu hii kwamba utambulisho wa albam yake iitwayo ‘Asante Yesu’ unatarajia kufanyika Mei 17 mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Msanii huyo ambaye pia alifanya vyema ndani ya filamu ya Fake Pastors alisema kuwa, baada ya uzinduzi huo itafuata ziara aliyoipa jina la ‘Ukombozi’ itakayomuwezesha kuzunguka mikoa minne ya Tanzania Bara ikiwemo Iringa, Tanga na Kilimanjaro, lengo likiwa ni kusaidia watoto yatima, wazee wasiyojiweza na watu wenye shida mbalimbali katika jamii.
**********************************

Keri Hillson yupo kikazi zaidi, siyo mapenzi

Wasomaji wengi waliotutumia ujumbe mfupi (SMS) wakitaka kufahamu mkali wa muziki wa R&B, Keri Hilson amewahi kujiachia na mastaa wa kiume wangapi, leo kupitia hapa ‘Ebwana Dah!’ wanaweza wasiamini kwamba, pamoja na jina lake kuingizwa kwenye orodha ya mastaa wa muziki Marekani na duniani kwa ujumla, mrembo huyo ameonesha bado yupo yupo kwanza kwa kuwa hana listi hata ya dume mmoja aliyewahi kujirusha naye faragha.

Kwa mujibu wa mtandao wa ‘intaneti’, Keri ameonesha kwamba, hivi sasa yupo kikazi zaidi ili ngoma zake ziweze kubamba na kutambulika karibu ulimwengu mzima kila zinapotoka kama ilivyo sasa ambapo amesimamia miguu miwili na kazi kama ‘Energy’ na ‘Superhuman’ aliyoshirikishwa vyema na Chriss Brown, suala la mapenzi atalipa nafasi pale muda utakapofika. Lakini inawezekana mrembo huyu (pichani juu) anaye mwanaume ambaye hajulikani ndiyo maana kunako mtandao wetu hajaingizwa.

Akiwa alizaliwa kwa jina la (Keri Lynn Hilson), mrembo huyo aliletwa duniani na wazazi wake Oktoba 27, 1982, huko Atlanta, Georgia, Marekani, imesalia miezi kadhaa atimize umri wa miaka 27. Kama haujamfahamu vizuri staa huyo ambaye nyota yake ni Nge, anapendelea nywele za rangi nyeusi pia ni mwandishi mzuri wa nyimbo.
***********************
Crazy Buffa: Wanaobebwa wajishikie

Baada ya kupotea kwenye game ya muziki wa kizazi kipya kwa muda mrefu hatimaye msanii Khalid Yusuph Amour ‘Crazy Buffa’ amerudi tena na kuiambia safu hii kwamba, baada ya kuona ‘madogo’ wengi waliyobebwa kwenye game ya muziki kisha wakashindwa kujishika ameamua kuja kuendeleza mapambano.

Mchizi ambaye anapatikana ndani ya Familia ya Kino (Kinondoni) alisema kwamba katika ujio huu mpya hakutaka kurudi peke yake, bali ana kichwa kingine cha siku nyingi, ‘Zahran’ ambaye amesimama naye katika goma yake mpya, ‘Ukibebwa jishikie’ ambayo kasi yake imegongwa na mtoto wa Mzee Zahir Ally Zorro, namzungmzia Banana.

“Hivi sasa nimerudi kamili, mashabiki wategemee vitu vya ajabu zaidi kwani utu uzima dawa,” alisema Buffa.
***********************************************
Ijumaa Sexiest Girl: Wema vs Irene

Shindano la kumtafuta Staa wa kike mwenye mvuto wa kimapenzi ‘Ijumaa Sexiest Girl’ lililoandaliwa na gazeti ndugu na hili, ‘Ijumaa’ linaelekea ukingoni huku washiriki wawili, Wema Isaac Sepetu na Irene Uwoya waliyoingia fainali wakionesha kuchuana vikali.

Wakati kura zikiendelea kumiminika wasomaji na mashabiki wengi wa mpambano huo wameonesha kuwa na hamu ya kutaka kufahamu nani ataibuka na ushindi huo, ukizingatia kwamba kila mshiriki anaonesha kuwa juu kutokana na mvuto alionao, lakini kura za wasomaji ndiyo zitaamua nani aibuke na ushindi.

Mratibu wa mpambano huo, Oscar Ndauka amewataka wasomaji na wapenzi wa shindano hilo kuendelea kutuma kura zao katika raundi hii ya mwisho ili wamuwezeshe mshiriki mmoja kuibuka na ushindi. Namba ni ile ile 0784-275 714.

compiled by: mc george

Sunday, February 22, 2009

TATIZO LA MIMBA UTOTONI

Little family ... Alfie (shoto), Chantelle na mtoto wao Maisie



Tatizo la mimba za utotoni si la Afrika tu, bali hata Ulaya lipo. Mtoto Alfie Patten, mwenye umri wa miaka 13, alimpa mimba mtoto mwenzie, Chantelle Steadman mwenye umri wa miaka 15 na kuzaa mtoto salama salimini…ishu hii ya aina yake imetokea nchini Uingereza hivi karibuni.

Dogo alimpachika mimba dogo mwenzie katika usiku mmoja tu waliofanya sex kwa mara ya kwanza, tena bila kondom na hawakujua kama wamepeana mimba hadi baada ya wiki 12 kupita. Mama wa msichana alimstukia binti yake baada ya kumuona ananenepa na kitumbo kinamtoka.

Dogo Alfie bado ana akili za kitoto kiasi kwamba hata bei ya nepi haijui, lakini wazazi wa pande zote mbili wako nao pamoja na wanawapa msaada unaohitajika kama watoto, ingawa wazazi nao ni ‘choka mbaya’, wanaishi kwa ‘posho ya serikali’ tu.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sun la Uingereza, Alfie anakuwa ‘Baba’ mdogo wa pili nchini Uingereza baada ya Sean Stewart ambaye alikuwa baba katika umri wa miaka 12, mwaka 1998, ambaye nae alimapachika mimba jirani yake, Emma Webster, aliyekuwa na umri wa miaka 15… Hii imekaaje jamani?

DAR CITY FC: TIMU MPYA MACHACHARI


Dar City FC ni timu mpya inayoshiriki katika ligi ya Wilaya ya Kinondoni huku ikiwa inaongoza katika kundi lake na tayari imeshaonesha mafanikio makubwa katika kipindi kifupi tangu ianzishwe na mchezaji wa zamani wa Timu ya Taifa, Athumani Tippo. Pichani ni baadhi ya wazee club na mlezi wa klabu hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na vijana hao ambao wameonesha kuwa na vipaji vya hali ya juu vya kusakata kabumbu na tayari watatu wao wapo kwenye Timu ya Taifa ya vijana.