Monday, February 23, 2009

WIKIENDA SHOWBIZ!


Sarah Mvungi kujitoa kwa Yatima, Wazee

Msanii wa maigizo Bongo ambaye hivi sasa amejikitia zaidi kunako muziki wa Injili, Sarah Mvungi (pichani juu) amesema na safu hii kwamba utambulisho wa albam yake iitwayo ‘Asante Yesu’ unatarajia kufanyika Mei 17 mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.

Msanii huyo ambaye pia alifanya vyema ndani ya filamu ya Fake Pastors alisema kuwa, baada ya uzinduzi huo itafuata ziara aliyoipa jina la ‘Ukombozi’ itakayomuwezesha kuzunguka mikoa minne ya Tanzania Bara ikiwemo Iringa, Tanga na Kilimanjaro, lengo likiwa ni kusaidia watoto yatima, wazee wasiyojiweza na watu wenye shida mbalimbali katika jamii.
**********************************

Keri Hillson yupo kikazi zaidi, siyo mapenzi

Wasomaji wengi waliotutumia ujumbe mfupi (SMS) wakitaka kufahamu mkali wa muziki wa R&B, Keri Hilson amewahi kujiachia na mastaa wa kiume wangapi, leo kupitia hapa ‘Ebwana Dah!’ wanaweza wasiamini kwamba, pamoja na jina lake kuingizwa kwenye orodha ya mastaa wa muziki Marekani na duniani kwa ujumla, mrembo huyo ameonesha bado yupo yupo kwanza kwa kuwa hana listi hata ya dume mmoja aliyewahi kujirusha naye faragha.

Kwa mujibu wa mtandao wa ‘intaneti’, Keri ameonesha kwamba, hivi sasa yupo kikazi zaidi ili ngoma zake ziweze kubamba na kutambulika karibu ulimwengu mzima kila zinapotoka kama ilivyo sasa ambapo amesimamia miguu miwili na kazi kama ‘Energy’ na ‘Superhuman’ aliyoshirikishwa vyema na Chriss Brown, suala la mapenzi atalipa nafasi pale muda utakapofika. Lakini inawezekana mrembo huyu (pichani juu) anaye mwanaume ambaye hajulikani ndiyo maana kunako mtandao wetu hajaingizwa.

Akiwa alizaliwa kwa jina la (Keri Lynn Hilson), mrembo huyo aliletwa duniani na wazazi wake Oktoba 27, 1982, huko Atlanta, Georgia, Marekani, imesalia miezi kadhaa atimize umri wa miaka 27. Kama haujamfahamu vizuri staa huyo ambaye nyota yake ni Nge, anapendelea nywele za rangi nyeusi pia ni mwandishi mzuri wa nyimbo.
***********************
Crazy Buffa: Wanaobebwa wajishikie

Baada ya kupotea kwenye game ya muziki wa kizazi kipya kwa muda mrefu hatimaye msanii Khalid Yusuph Amour ‘Crazy Buffa’ amerudi tena na kuiambia safu hii kwamba, baada ya kuona ‘madogo’ wengi waliyobebwa kwenye game ya muziki kisha wakashindwa kujishika ameamua kuja kuendeleza mapambano.

Mchizi ambaye anapatikana ndani ya Familia ya Kino (Kinondoni) alisema kwamba katika ujio huu mpya hakutaka kurudi peke yake, bali ana kichwa kingine cha siku nyingi, ‘Zahran’ ambaye amesimama naye katika goma yake mpya, ‘Ukibebwa jishikie’ ambayo kasi yake imegongwa na mtoto wa Mzee Zahir Ally Zorro, namzungmzia Banana.

“Hivi sasa nimerudi kamili, mashabiki wategemee vitu vya ajabu zaidi kwani utu uzima dawa,” alisema Buffa.
***********************************************
Ijumaa Sexiest Girl: Wema vs Irene

Shindano la kumtafuta Staa wa kike mwenye mvuto wa kimapenzi ‘Ijumaa Sexiest Girl’ lililoandaliwa na gazeti ndugu na hili, ‘Ijumaa’ linaelekea ukingoni huku washiriki wawili, Wema Isaac Sepetu na Irene Uwoya waliyoingia fainali wakionesha kuchuana vikali.

Wakati kura zikiendelea kumiminika wasomaji na mashabiki wengi wa mpambano huo wameonesha kuwa na hamu ya kutaka kufahamu nani ataibuka na ushindi huo, ukizingatia kwamba kila mshiriki anaonesha kuwa juu kutokana na mvuto alionao, lakini kura za wasomaji ndiyo zitaamua nani aibuke na ushindi.

Mratibu wa mpambano huo, Oscar Ndauka amewataka wasomaji na wapenzi wa shindano hilo kuendelea kutuma kura zao katika raundi hii ya mwisho ili wamuwezeshe mshiriki mmoja kuibuka na ushindi. Namba ni ile ile 0784-275 714.

compiled by: mc george

1 comment:

Anonymous said...

Bahai mbaya niko nje ya nchi siwezi kutuma kura yangu kwa simu.Ila kura yangu kama naruhusiwa kuipiga hapa inaenda kwa Irene Uwoya.thnx