Tuesday, May 18, 2010

BROKOLI: UTAFITI WATHIBITISHA TENA KUHUSU KUZUIA SARATANI


Brokoli ni mboga jamii ya kabichi lakini yenyewe inachipua na kuota kama uyoga au maua, imo katika ‘spishi’ ya kabichi ambazo maua yake huliwa. Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Michigan Comprehensive Cancer Center, umeendelea kuthibitisha kuwa mboga hii ina uwezo mkubwa wa kuzuia seli za saratani mwilini.

Katika utafiti wao mwingine wa hivi karibuni, waliofanya kwa kutumia panya, wameweza kuthibitisha pasina shaka kuwa virutubisho aina ya ‘sulforaphane’ vilivyomo kwenye mboga hii, huua chanzo kinachosababisha kumelea kwa saratani na ina uwezo wa kuzuia kuibuka kwa chembe nyingine mwilini.

Kwa maana nyingine, ulaji wa mboga hii ni muhimu kwetu sote, kwani itatupa kinga ya ugonjwa hatari wa saratani (cancer) ambao ukishaupata hauna tiba na umekuwa tishio duniani kwa sasa kutokana na watu wengi kuishi staili ya maisha ambayo kupata saratani kumekuwa kawaida.

INAPATIKANA WAPI?
Mboga hii inalimwa nchini sehemu mbalimbali na upatikanaji wake ni rahisi. Kwa wakazi wa Dar es Salaam, ukienda katika soko la Kisutu au ‘super markets’ kubwa, utaipata mboga hii kwa wingi na kwa bei ya kawaida tu, mbali ya kuwa na virutubisho vyenye uwezo wa kupambana na chembechembe za saratani, brokoli inaaminika pia kuwa na vitamin C nyingi kuliko chungwa.

HUZUIA SARATANI
Licha ya Brokoli kuwa na madini ya calcium kama yanayopatikana kwenye maziwa, ina virutubisho vingi vyenye uwezo wa kupambana na ugonjwa hatari wa saratani, hasa maua yake ambayo yana kiwango kikubwa sana cha viambata vyenye uwezo wa kuzuia saratani katika mwili wa binadamu.

Ulaji wa mboga ya Brokoli mara kwa mara, inatoa kinga madhubuti katika mwili wa binadamu dhidi ya saratani ya tumbo. Pia ulaji wa mboga hii mara kwa mara hupunguza uwezekano wa mtu kupatwa na vidonda vya tumbo. Ngozi iliyoungua kwa jua nayo itapata nafuu ukitumia mboga hii na hii ina maana kwamba utaweza pia kujikinga na saratani ya ngozi (Skin Cancer).
UGONJWA WA MOYO NA MTOTO WA JICHO
Kwa kula Brokoli mara kwa mara, pia utakuwa unaupatia mwili wako kinga ya ugonjwa wa moyo au utapunguza kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kupatwa na ugonjwa huo. Aidha, kama unasumbuliwa na tatizo la ‘mtoto wa jicho’, kula maua ya Brokoli angalu mara mbili kwa wiki na tatizo lako litapungua kwa kiasi kikubwa. Vile vile unapokula mboga hiyo utakuwa unaimarisha kinga yako ya mwili.

Mboga hii ina uwezo wa kuimarisha kinga ya mwili kutokana na kuwa na kiwango kikubwa cha madini aina ya Zinc na madini mengine yanayohitajika. Ieleweke kuwa mboga hii ni muhimu sana kwa wajawazito kwa sababu ina madini aina ya Folic Acid ambayo ni muhimu sana kwa kina mama wenye mimba. Madini haya ni adimu sana hivyo kwa kupatikana kwenye mboga hii inaifanya kuwa ya kipekee, kwani madini haya ndiyo yanayosaidia ukuaji wa mtoto tumboni bila kuleta madhara yoyote.

UGONJWA WA PUMU NA BARIDI YABISI
Inaelezwa pia kuwa ulaji wa Brokoli hutoa ahueni kubwa kwa watu wanaosumbuliwa na ugonjwa wa pumu au baridi yabisi. Kiwango kikubwa cha vitamin c kilichomo kwenye mboga hii, hutoa nafuu kubwa ya maumivu kwa wagonjwa hao, hivyo kwa kula mboga hii dalili za pumu hudhibitiwa mara moja pamoja na maumivu ya baridi yabisi.

Mbali ya faida hizo zilizoorodheshwa, faida nyingine zinazopatikana kwa ulaji wa mboga hii mara kwa mara ni pamoja na kutuliza maumivu ya moyo na kutoa ahueni kwa wagonjwa wa kisukari. Hivyo ushauri unatolewa kwa watu kuila mboga hii na mboga nyingine ili kuupa mwili kinga inayotakiwa mwilini dhidi ya maradhi mbalimbali kama ilivyoanishwa hapo juu.

Ajabu nikwamba, pamoja na kuwa na faida hizo lukuki, lakini ni miongoni mwa mboga za majani ambazo hazipendwi na watu wengi. We angali kwenye sherehe za harusi inapokuwepo mboga hii na vile ambavyo watu hukwepa kuichukua. Kumbuka unavyoijali afya yako leo, ndivyo nayo itakavyokujali kesho utakapokuwa mzee.

1 comment:

Unknown said...

Duh nawapa pole sana. Katika kitu sikosi kwenye vegetable yangu ni hii mboga, na Wallah nilikuwa sijui kama inafaidi nyingi hivi.

Mrisho bro. Asante sana.
Hivi sasa naongeza manjonjo zaidi.
Na raha ya mboga hii uipike isiive iwe kachkachkach ndiyo utapata raha yake.