Friday, July 9, 2010

IJUMAA SHOWBIZ!

Jipanguse rrraaaa!! rrraaaaa!!
Jipangusee, Rrraaaaaa!! Ndiyo kauli mbiu ya tamasha kubwa la Fiesta 2010 ambalo hufanyika mara moja kila mwaka na kuwakutanisha wasanii kibao kutoka ndani na nje ya Bongo.

Kwa mujibu wa waandaaji, Primetime Promotion, mwaka huu mpango mzima ulianzia pande za Morogoro Julai 7 na leo Julai 9 shughuli kubwa inahamia pale Matongee Club, Arusha ikifuatiwa na Kilimanjaro Julai 10, wilayani Moshi ndani ya Club La Liga.

Baada ya Kilimanjaro shoo itahamia Dodoma, Tanga, kabla ya kurudi Dar es Salaam mwisho wa mwezi huu, kisha Zanzibar, Musoma na sehemu nyingine kibao.
Wasanii kama Mwasiti Almasi ‘Mwasiti’ (picha kubwa), anayefanya vyema na ngoma yake, ‘Siyo kisa pombe’, Diamond, Madee na wengine kibao ni miongoni mwa vichwa vitakavyosababisha shangwe za ‘Kujipangusa’ katika tamasha hilo.

******************
Kassim, Desso Chupu chupu stejini
Walikuwa kama wanaekti muvi, pale walipodandia stejini kwa ajili ya kusababisha shangwe kwa mashabiki wao lakini cha kushangaza walishtukia jukwaa likiwapeleka chini kabla hawajagundua kuna mbao mbili zilizotumika kutengenezea steji hiyo zimevunjika, Hemed Kisanda anashuka nayo.

Nawazungumzia wakali wawili kutoka ndani ya familia ya Tip Top Connection, Kassim Mganga a.k.a ‘Kassim’ na Godfrey Mlawa a.k.a Desso ambao walikutwa na tafrani hiyo walipokuwa wanadondosha shoo mwishoni mwa wiki iliyopita ndani ya Uwanja wa Samora, uliopo Iringa mjini.

Mpango mzima ambao ulishuhudiwa na ShowBiz ulikuwa hivi, wasanii hao walikuwa kwenye ‘tua’ ya pamoja na kundi lao la Tip Top ambapo katika shughuli hiyo walipeana zamu kupanda, ilipofika kwa Kassim na Desso ambao walionekana kuvamia steji kwa shangwe za nguvu jukwaa lilishindwa kuvumilia na kuvunjika.

‘Niuzi’ zaidi kutoka pande hizo zinadai kuwa uzito mkubwa alionao mwana Bongo fleva Kassim ndiyo ulikuwa chanzo cha kuvunjika kwa jukwaa hilo licha ya yeye mwenyewe kukanusha na kudai kuwa jukwaa lilivunjika kufuatia makamuzi babu kubwa waliyofanya yeye na mtu mzima Desso.
xxxxxxxxxxxx

Alli kiba:Dhuluma imenikimbiza Bongo
Staa wa ngoma ya Sinderela aliyejiajiri kupitia game ya muziki wa kizazi kipya a.k.a Bongo Fleva, Alli Kiba amesema na ShowBiz kwamba dhuluma inayofaywa na baadhi ya mapromota ndiyo sababu kubwa inayomfanya kuzipa kisogo ‘shoo’ za Kibongo na ‘kulowea’kwenye steji za Ughaibuni, Hemed Kisanda alipiga naye stori.

Mkali huyo ambaye bado anauza kupitia kazi zake za muziki hapa ‘Tizii’ na nchi za jirani, ameuambia ukurasa huu ‘namba wani’ kwa burudani kwamba, kulikuwa na mlolongo wa matukio mengi ya kudhulumiwa mkwanja wa shoo na mapromota uchwara wa Kibongo, kitu ambacho kilikuwa kinamuumiza, akaamua kuziweka kando kwa muda shoo za kibongo

“Kuna watu fulani fulani hivi wanawaumiza sana wasanii, huku wakitangaza kuwasaidia na kuwainua, lakini ukweli ni kuwa jamaa ni watu wa dhuluma sana ndiyo maana mimi nakamua mbele kwa mbele ambako hakuna longolongo,” alitanabaisha staa huyo aliyewahi kukimbiza na ngoma yake, ‘Usiniseme.’
xxxxxxxxxxxxx

Kala:Mademu wa Kibongo wazinguaji
Wiki iliyopita kupitia hapa ShowBiz tuliandika ishu iliyomuhusu msanii Kala Jeremih iliyokuwa na kichwa cha habari “Kala asepa Kampala, akolea kwa demu wa Kiganda”, tukaahidi kumtafuta mchizi na kuweka kila kitu hadharani kuhusu ishu hiyo na safari yake huko kwa Museven.

Safu hii ilifanikiwa kumpata Kala kwa njia ya mtandao na kupiga naye stori kadhaa ambapo alisema kwamba. “Kweli kaka niko Uganda napiga madude ya nguvu (muziki) na hizo picha zinanionesha mimi na demu wangu wa huku, ila kwasababu maalum siwezi kumtaja jina hivi sasa mpaka hapo mambo yatakapokuwa swadakta.

“Niliondoka Bongo zaidi ya miezi miwili iliyopita baada ya kumpata mtu ambaye atasimamia kazi zangu fresh ambaye anaishi huku Uganda, kwa bahati nzuri pia nikafanikiwa kukutana na mrembo huyo ambaye nampenda kupita kiasi tukaanzisha uhusiano. Niliamua kufanya hivi baada ya kuumizwa na mademu wa Kibongo ambao kwangu nawaona kama wazinguaji,” alisema Kala.

Kala ambaye kimuziki alijulikana kupitia shindano la kusaka vipaji la BSS mwaka 2007 na kushika nafasi ya nne, alisema kwamba wasichana wengi wa Kibongo hawana mapenzi ya dhati zaidi ya kuweka mkwanja mbele kitu ambacho kinawafanya wasidumu na wanaume.

“Mimi pia nilikuwa nashangaa, hapo Bongo nilikuwa na bahati ya kupata wasichana wazuri lakini sikuwahi kudumu nao, naamini huyu wa huku baadaye anaweza kuwa mke wa milele,” alisema Kala ambaye alikiri kuwa kila akifikiria kuja Tanzania anashindwa kufanya hivyo pale anapomuona demu wake huyo.
xxxxxxxxx

Zay B Amchana dj maarufu!
Msanii wa kike aliyefungua njia kunako game ya muziki wa Hip Hop Bongo, mwanadada Zainabu Lipangile a.k.a Zay B ameibuka na kumchana ‘Laivu’ dj mmoja maarufu hapa ‘Tzii’ (jina lipo) akimtuhumu kuwa mmoja wa watu waliokuwa wanaweka ‘kauzibe’ kwenye ngoma zake, Hemed Kisanda anajiachia nayo.

Zay B aliyeibukia kwenye anga ya Bongo Fleva na ngoma ya ‘Niko gado,’ ameweka wazi hasira zake juu ya dj huyo kupitia ngoma yake mpya inayokwenda kwa jina la ‘Sina Shobo’ inayosikika kupitia vituo kadhaa vya redio huku akitamba kuwa licha ya jamaa kupanga njama za kumpoteza lakini hataweza na mwisho atapotea yeye (dj).

“Ni kweli nimemchana dj huyo (huku akitaja jina) kwakuwa kila nilipokuwa nikimpelekea kazi aliniambia hazina kiwango sasa ngoma hii ni zawadi yake na kama hataikubali nitamchana kwenye albamu nzima,” alisema Zay B.

Hata hivyo, juhudi za kumpata dj huyo aliyekuwa akipiga mzigo kwenye redio moja maarufu ili kujibu tuhuma hizi zilikwama baada ya kujulishwa kuwa ameishapigwa chini mzigo (kuachishwa kazi).

Compiled by mc george/ijumaa newspaper

No comments: