Wednesday, August 18, 2010

Kufunga kuna faida gani kiafya?


Umekuwepo mjadala wa kisayansi wa muda mrefu kuhusu kufunga kama kuna manufaa kwa afya ya mtu ama la. Kufunga ni sehemu muhimu ya imani nyingi za kidini, kuanzia Waislamu, Wakristo hadi Wayahudi. Wengi wana mashaka kama faida ya kiroho inayopatika kutokana na funga huwa na uhusiano na afya ya mwili.

Jumuiya nyingi za wataalamu wa tiba mbadala, wanaamini kwamba funga inaweza kufanya maajabu makubwa katika mwili wa binadamu. Katika makala haya, tutajaribu kuangalia hoja zinazotolewa na wataalamu hao wa tiba mbadala katika jitihada za kuihabarisha jamii umuhimu wa funga kiafya.

Kitaalamu, funga huanza kufanya kazi ndani ya saa 10 za kwanza hadi saa 24. Kwa sababu ili athari za funga zianze kuonekana ni mpaka akiba ya wanga iliyomo mwilini inapoanza kutumika kama chanzo cha nishati. Mtu huanza kusikia njaa, pale akiba ya protini inapokwisha mwilini kama nishati.

Kwa kawaida, mwili huwa na uwezo wa kijisafisha wenyewe kwa kutoa sumu mwilini (Detoxification) na hii ndiyo hoja kubwa inayotumiwa na wataalamu wa tiba mbadala wanaoamini funga ni tiba na kinga ya maradhi mengi. Detoxification ni mchakato wa mwili kuua na kutoa sumu mwilini kupitia haja kubwa, ini, figo, mapafu na kwa njia ya ngozi (jasho, n.k).

Faida nyingine ya funga inayoelezewa ni ule mchakato wa uponyaji unaofanyika mwilini wakati mtu anapokuwa amefunga. Inaelezwa kuwa wakati wa funga, ile nishati inayoelekezwa kwenye mfumo wa usagaji chakula, huelekezwa kwenye mfumo wa ‘metabolizi’ na mfumo wa kinga ya mwili. Katika kipindi hicho, magonjwa na mauvimbe ya ajabu ajabu huweza kudhibitiwa na hatimaye kutoweka kabisa.

Vile vile ukarabati wa seli zilizoathirika huko nyuma, huweza kutengenezwa upya na kuwa imara zaidi. Mwisho, faida kubwa iliyothibitishwa kisayansi itokanayo na funga, ni kwamba mtu anayefunga, mwili wake huimarika na miaka yake ya kuishi huongezeka! Faida hii inatokana na ukweli kwamba wakati wa funga uzalishaji wa protini mwilini huwa mkubwa, kasi ya ‘metaboliz’ hushuka, mfumo wa kinga ya mwili huimarika zaidi.

Kuongezeka kwa uzalishaji wa homoni za mwili ndiko kunakochangia faida hizi za muda mrefu. Pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa homoni za ukuwaji wa mwili, homoni za kuzuia uzeekaji wa mwili nazo huzalishwa kwa wingi wakati wa funga, hivyo kumfanya mtu anayefunga mara kwa mara kuonekana kijana kila siku.

Kwa kuhitimisha, inaonekana kuna sababu nyingi za msingi za kuamini kuwa funga ina faida nyingi kwa afya ya binadamu. Hata hivyo, bado kuna baadhi ya madaktari wengine hukataza watu kufunga kwa muda mrefu bila kupata ushauri wao kwa madai kuwa kufunga kuna madhara katika afya, na hii imetokana na ukweli kwamba jamii imekuwa ikiamini kwamba ili mtu uishi unahitaji kula, iweje leo mtu usipokula utaishi sana? Lakini wanasahu kuwa Mungu aliyetuamrisha kufunga anajua zaidi yetu!



3 comments:

Disminder orig baby said...

Haswaa Mungu aliyetuamrisha kufunga anajua zaidi.

Kaka mimi nina desturi ya kufunga kila Monday na Thursday!! Huwezi amini mwili wangu uko very light, japo nina umbo kubwa lakini huwezi amini najisikia huru sana.
Funga ni dawa!!
Ntakupa siri moja, kuna wakati mtu unaweza hizi tumbo liko vibaya, gesi si gesi, ilimradi tafrani tu, aah uwa naamua kufunga siku inayofuata, Wallah baada ya hapo najisikia huru.

Mungu ni mkubwa. Ramadhani Mubarakh.

Anonymous said...

Hao wanaosema kufunga eti mpaka upate ushauri wa madaktari naona wana matatizo yao tu ya kimisimamo. Maana inajulikana tangu zamani kuwa kufunga ni tiba.

Kingine kula sana kunazeesha mwili maana unafanyisha mwili wako kazi ya ziada unapokula chakula kingi. Kula kiasi tu kama tulivyoamrishwa na Mtume SAW kuligawa tumbo katika sehemu tatu (ya maji, hewa, na chakula). Jaribu hiyo uone maajabu yake hutakaa uzeeke hovyo hovyo na ngozi yako itakuwa nzuri daima,

Anonymous said...

Lakini kaka mbona kuna utafauti wa kufunga kati ya dini mbalimbali? je hawa wanaofunga kula nyama lakini maji wanakunywa na vyakula vingine vigine wanatumia,kuna hata wanaofunga kula vyakula wavipendavyo hawa wanafaida kweli ya kufunga kama ulivyotoa muelezo?