Ndugu zangu,

Ukitaka kuukata  na kuuangusha mbuyu usianze kufikiria unene wake.
Jana  usiku jirani zetu Zambia wameafanya maajabu ya soka. Vijana wa Chipolopolo wamatwaa ubingwa wa Afrika kwa kuwafunga Ivory Coast.
Ndio, Zambia jana wametufanya tujisikie, kuwa; “ We are all Zambians”. Kwamba sote ni Wazambia.

Siri ya ushindi wa Zambia?

Ni Uzambia. Ni utaifa. Ni uzalendo.   Tuliwaona vijana wa Chipolopolo wanaojituma uwanjani. Vijana waliokuwa tayari kufia uwanjani, Vijana kama akina Kampamba, Mulenga, Sunzu, Nkausu, Chansa na wengineo.

Na katika maisha, ili mwanadamu afanikiwe unahitaji kuwa na ‘ K’ tatu; Kujitambua, Kujiamini na Kuthubutu.
Vijana wa Chipolopolo wamejitambua. Wameijua  historia yao. Wamejua walikotoka. Wamejua, kuwa  kuna baba zao, mwaka 1993  walikuwa njiani kwenda Senegal kucheza mechi muhimu kufuzu kutafuta tiketi ya kucheza Kombe La Dunia.   Usafiri ulikuwa mgumu. Walipanda ndege ya jeshi. Ndege ilianguka pwani ya Gabon, wachezaji wote 18 walipoteza maisha.  Walikufa kwa ajili ya nchi yao.

Ndio maana jana, kwa kuitambua historia hiyo. Wazambia wale waliingia uwanjani wakiwa tayari kufia uwanjani kwa ajili ya nchi yao.  Tulimwona beki  Joseph Mussonda akiumia vibaya. Alijikaza kuendelea. Ikaonekana haiwezekani kabisa. Akatolewa nje. Alitokwa na machozi kwa muda mwingi. Si kwa maumivu ya mguu tu, ni kwa kuona uchungu wa kukosa kuwa uwanjani kuipigania nchi yake. Huo ni moyo mkubwa wa uzalendo.
Wazambia wale hawakuwa wakifikiria posho zao, bali taifa lao. Na hakuna ahadi yoyote ya fedha waliyopewa kabla ya mechi ya jana.

Ndio, Wazambia wale walionyesha kujiamini sana. Walicheza mpira wao. Walikuwa focused muda wote.Hawakujali majina makubwa kama ya akina Drogba, Kolo Toure, Yahya  Toure, Koite, Gervinjo, Gosso Gosso na mengineyo. Hawakujali kama walicheza na nyota wanaovichezea vilabu vikubwa huko Ulaya. Chipolopolo walicheza mchezo wao. Mwanzo hadi mwisho.  Hata pale Ivory Coast walipokuwa wakijaribu kubadilisha mbinu na hata  kubadilisha nafasi za wachezaji uwanjani, bado Zambia waliendelea kucheza mpira wao. 
Kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa jirani zetu wa Zambia. Nitaendelea na uchambuzi wangu…
Maggid Mjengwa,
Iringa.