Tuesday, May 15, 2012

WASANII WATAKIWA KUJIPANGA KUKABILI TEKNOLOJIA MPYA

Msimamizi wa vipindi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Mwanga Kirahi akisisitiza jambo wakati akiwasilisha mada iliyohusu Teknolojia ya kisasa (Digital) Katika Utengenezaji Filamu kwenye Jukwaa la Sanaa la BASATA wiki hii.Kulia kwake ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Matukio BASATA, Malimi Mashili.
   
Mkongwe wa Muziki wa dansi Mzee Kassim Mapili akionesha manjonjo yake baada ya kufurahishwa na mada kuhusu Mfumo Digital iliyowasilishwa kwenye Jukwaa la Sanaa wiki hii.
   
Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Mawasiliano ya Umma Ngalimecha Ngahyoma akichangia mada hiyo kwenye Jukwaa la Sanaa. Alishauri Wasanii kujipanga katika kuukabili mfumo wa Digital.
 Sehemu ya Wadau wa Jukwaa la Sanaa waliohudhuria mjadala huo wakifuatilia kwa makini.   


Wasanii nchini wameshauriwa kujipanga katika kutumia fursa na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza wakati Ulimwengu ukijiandaa kuingia kwenye mfumo wa digital kutoka ule wa nalogia ifikapo mwaka 2014.
Ushauri huo umetolewa wiki hii na Msimazi wa Vipindi vya televisheni wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Mwanga Kirahi wakati akiwasilisha mada iliyohusu Teknolojia ya kisasa Katika Utengenezaji Filamu kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya BASATA Ilala Sharif Shamba.
Alisema kuwa kuhama kutoka mfumo wa analogia kwenda digitali kutazalisha fursa mbalimbali za kuendeleza Sanaa nchini lakini pia ni mwanzo wa kuibuka kwa changamto nyingi ambazo kama wasanii hawatakuwa makini basi wanaweza kupotea na kushindwa kushindana ipasavyo.
“Mfumo wa digitali utaleta ushindani katika kuandaa programu za televisheni, utazalisha fursa kwa kazi za wasaniii wetu kuonekana ulimwengu mzima lakini unaweza kuwa mwanzo wa kufa kwa ubunifu kama wasanii watategemea vifaa vya kisasa tu pasipo kuingiza ubunifu binafsi” alisisitiza.
Katika hili aliwashauri wasanii kutengeneza kazi zenye ubora na zisizo za kunakiri kutoka kwa wengine lakini pia zenye ubunifu binafsi pasipo kutegemea vifaa hivi vya kisasa pekee kwani kinyume chake ni kukataliwa kwa kazi zao na hatimaye kupwaya.
“Digital maana yake ni kazi za Wasanii wetu kuonekana Ulimwengu mzima, sasa kama zitakuwa za kunakiri kutoka kwa wengine na kutegemea vifaa hivi vya kisasa tu pasipo ubunifu binafsi hatutafanikiwa. Haya pekee yanazifanya kazi zetu zisivume muda mrefu kwani zinakuwa si original (halisi)i” alizidi kusisitiza.
Aliongeza kuwa, wasanii hawana budi kubadilika sasa na kuacha tabia ya wao kufanya kila kitu kikuanzia umeneja, utunzi, uongozaji (directing), uzalishaji (producing) na kadhalika kwani kwa kufanya hivyo kunazifanya kazi zao kuwa na radha moja pekee ambayo haiwezi kudumu muda mrefu.
Wadau wengi waliofika kupata elimu hiyo kupitia programu ya Jukwaa la Sanaa waliiomba Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kupanga kukutana na wasanii ili kuwapa elimu juu ya mchakato wa kuhama kutoka mfumo wa analogia kwenda digitali.

1 comment:

emuthree said...

Kweli kabisa, maana hilo teke jipya, usipoliangalia unaweza ukang'olewa meno,tujipange na tuwe pamoja na syanasi na teke linalokujia, au sio