Friday, June 8, 2012
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI FURSA YA WASANII WA TANZANIA KUSHINDA EURO 5,000 KATIKA SHINDANO LA KUTUNGA WIMBO RASMI WA KUNDI LA MATAIFA YA AFRIKA, KARIBIANI NA PASIFIKI (ACP GROUP OF STATES)
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo limepokea mwaliko wa Wasanii wa Tanzania kujitokeza kushiriki shindano la kutunga wimbo utakaokuwa unatumiwa kama wimbo rasmi wa mataifa ya Afrika, Karibiani na Pasifiki (ACP Group of States).
Shindano hili ambalo litahusisha mataifa 79 wanachama wa umoja huu limeandaliwa na Sekretarieti ya ACP kwa lengo la kupata wimbo ambao utabeba dhana ya mataifa ya Afrika, Karibiani na Pasifiki.
Kwa mujibu wa taarifa ya Sekretarieti ya ACP, shindano hili linamhusu msanii mmoja-mmoja au Kikundi cha wasanii ambao watapaswa kutunga wimbo huo kwa kuzingatia lengo kuu la umoja huo ambalo ni Maendeleo Endelevu na Upunguzaji Umaskini sambamba na Ushawishi mkubwa kwenye Uchumi wa Dunia.
Aidha, wimbo huo utatakiwa uwe wenye kujenga moyo, fikra na kutangaza malengo ya kundi hili la mataifa ya Afrika, Pasifiki na Karibiani.
BASATA inatoa wito kwa wasanii wa Tanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki shindano hili kwani ni heshima na fursa pekee tumepewa kama taifa kuonesha vipaji na uwezo wetu kimataifa katika eneo la utunzi wa nyimbo.
Ni wazi kuwa, kujitokeza kwa wasanii wetu wengi kushiriki katika shindano hili si tu kutaonesha utayari wa sisi kama taifa katika kushindana na mataifa mengine wanachama bali utakuwa ni mwanya wa kuitangaza Sanaa yetu ya muziki nje ya mipaka yetu.
Ikumbukwe kuwa, ushindi wa Msanii kutoka Tanzania kwenye shindano hili kutamjengea heshima msanii husika na taifa kwa ujumla.
Maelekezo kuhusu Wimbo utakaotungwa
• Tungo zote lazima ziandikwe katika moja ya lugha rasmi za ACP ambazo ni Kiingereza, Kifaransa, Kiispaniyola na Kireno.
• Wimbo huo uliokamilika lazima uambatanishwe na tunzi (lyrics) zilizoandikwa na zitumwe katika mfumo wa MP3/DVD/WAV Format
• Tungo ziguse maeneo yafuatayo
i) Fikra ya umoja ambayo itaunganisha nchi wanachama wa ACP
ii) Utajiri na tamaduni mbalimbali zilizo katika nchi wanachama wa ACP
iii) Mataifa wanachama wa ACP na kuheshimu Demokrasia, Haki za Binadamu na Utawala Bora.
iv) Nchi wanachama wa ACP na msisitizo katika maendeleo yenye usawa pia kusimamia mikataba ya kimataifa ya Haki na Amani.
Jinsi ya Kushiriki
Nyimbo zilizotungwa kwa kufuata mwongozo huo wa ACP zitumwe kupitia anuani ifuatayo ;-
Josephine Latu-Sanft (Press Office)
Avenue Georges Henri
451,1200 Brussels, Belgium
E-mail : latu@acp.int.
Mwisho wa kutuma
Agosti 31, 2012
Imetolewa na;
Ghonche Materego
Katibu Mtendaji - BASATA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment