Tuesday, July 24, 2007

KITCHEN PARTY YA HOYCE TEMU YAZUA JAMBO!!

Tanzania July 25, 2007

Na Mwandishi Wetu

Kitchen Party ya aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1999, Hoyce Temu ilikuwa ya aina yake kufuatia watu wa Usalama wa Taifa ‘system’ kuweka ulinzi wa ‘kufa mtu’ huku mwandishi wa gazeti hili akitishiwa bastola.


Shughuli hiyo ambayo ilifanyika Julai 22, mwaka huu katika Ukumbi wa Water Front jijini Dar es Salaam, ilihudhuriwa na watu maarufu lukuki akiwemo mke wa Rais mstaafu, mama Anna Mkapa.


Mwandishi wetu (jina tunalihifadhi) ambaye alifanikiwa kupata mwaliko wa ‘kitchen party’ hiyo akiwa amejikoki kisawasawa, alitinga katika ukumbi huo na kuchagua meza moja iliyopangwa mahususi kwa ajili ya wageni waalikwa.


Alipotulia, mwandishi huyo alianza kusoma mazingira huku akiweka sawa kamera yake ili aweze kuchukua baadhi ya matukio yaliyojiri katika ukumbi huo.


Hata hivyo, kabla ya kufanya chochote alitokea mtu mmoja ambaye anadaiwa kuwa ni wa usalama na kumkataza mwanahabari huyo asipige picha ndani ya ukumbi huo.


Habari ambazo mwandishi wetu alizipata baadaye zilidai kuwa mtu huyo alimfuata baada ya kutonywa na paparazi mmoja ambaye alipewa tenda ya kupiga picha katika shughuli hiyo.


Mwandishi wetu alipoona hivyo, akaona ‘isiwe tabu’ alirudisha kamera hiyo katika mkoba wake na kutoa simu yake ya kamera kisha kuanza kuchukua matukio.


Tukio ambalo mwandishi huyo alikusudia kulichukua ni lile la Hoyce kwenda mbele kuchukua chakula , lakini kabla ya mwanahabari huyo kufanikiwa kupiga picha alijikuta akiporwa simu hiyo na mtu aliyekuwa amesimama nyuma yake.


‘’Wakati akinipora simu alikuwa akiipekuwa kuona kama nimeshapiga picha ama la, huku akiniambia kuwa sikutakiwa kupiga picha na kwamba tayari alishanionya kwani hawakupenda matukio yanayojiri kuvuja nje ya ukumbi huo,’’ alisema mwandishi huyo.


Hata hivyo, alirudishiwa simu yake na kusisitiziwa kutokufanya hivyo, kama ataonekanaa kukaidi angetolewa nje. Aidha alipokosa nafasi ya kupata matukio hayo, aliamua kutoka nje ya ukumbi huo na kuwasiliana na watu wa ofisini kwake kuhusu ugumu wa zoezi hilo lakini ghafla alizingirwa na wana usalama waliotaka kujua alikuwa akiwasiliana na nani.


Mwanahabari huyo alikata simu na kurejea ukumbini na kufuatilia matukio mengine yaliyokuwa yakiendelea ambapo waalikwa walikuwa wakifanya vitu vyao wakiongozwa na mwenye shughuli hiyo Hoyce.


Muda mfupi kabla ya shughuli hiyo kuisha, mwandishi wetu aliamua kuondoka ukumbini humo, ambapo alistukia akifuatwa na watu wanne akiwemo dada mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Angela.


Watu hao walimtaka kutoa simu aliyokuwa nayo huku mwanaume mmoja akimtishia kumtoa roho baada ya kumtolea bastola na kumuwekea mbavuni ili asilete pingamizi na kumtaka ampatie Angela .


Mwandishi huyo alitii amri hiyo na kumkabidhi simu Angela ambaye alidai yeye ni afisa uhusiano wa taasisi ambayo hakutaka kuitaja.


‘’Alipochukua simu hiyo aliikagua kwa kufungua ili kusoma kilichomo akitaka kujua kama kuna meseji yoyote au picha iliyochukuliwa kuhusiana na shughuli hiyo’’, alisema mwandishi.


Baada ya kushindwa kuona chochote kinachohusiana na kitchen party hiyo alimrudishia simu mwandishi na kuanza kumpa vitisho kuwa hapendi habari au picha za tukio hilo kuonekana kwenye magazeti kwani akifanya hivyo ataondolewa duniani.


Mwandishi wetu aliondoka katika eneo la tukio na kwenda kutoa taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi (Central Police) na kupewa namba ya jalada CD/RB/8986/07 - tishio la kutaka kuua kwa bastola.

Hoyce Temu anatarajia kufunga pingu za maisha hivi karibuni.


Mbunge, mumewe sasa matatani

Na Salum Mnette

Ndoa ya Mbunge wa Chama cha Wananchi CUF, Meryce Mussa Emmanuel na Maberana Bashinde imeingia matatani baada ya mume wake wa awali Musa John Buganga kufungua kesi kupiga ndoa hiyo na mambo mengine kadhaa.

Buganga amefungulia wanandoa hao kesi ya madai Civil Case Number 37 ya 2007 katika mahakama ya Wilaya ya Ilala (Samora) Julai 16, mwaka huu.

Mwandishi wetu alifanikiwa kuiona hati ya wito (summons) inayokwenda kwa Mbunge Meryce na Bwana Maberana ikiwataka wawili hao kusimama kizimbani Agosti 7, mwaka huu saa 2.30 asubuhi.

Katika hati hiyo ya madai, Buganga anataka mahakama itengue ndoa hiyo kwa vile mwanamke huyo ni mkewe na itangaze kuwa ndoa yake na mkewe imeshavunjwa.

Hati hiyo, pia inaitaka mahakama itoe amri ya kuachana kwa ndoa hiyo mpya, uvunjwaji wa ndoa yake aliyodumu nayo kwa zaidi ya miaka 20, ulinzi wa watoto, fidia ya shilingi milioni 60 kwa wote wawili kwa kufanya uzinzi.

Buganga anadai pia kuwa malipo hayo alipiwe riba tangu siku ya kutolewa kwa madai haya hadi fedha hizo zinamalizika kulipwa pamoja na chochote ambacho hakimu ataona kinafaa.

Akiongea na mwandishi wetu, Buganga alisema kuwa ameamua kufanya hivyo ili kupata haki yake ya msingi.

“Nimeamua kuwaburuza mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake na iwe fundisho kwa watu wanaodandia ndoa za wengine, sikubali kuona mke wangu anaoolewa na mtu mwingine, huko ni kudhalilishana,” alisema Buganga huku akiwa ameshikilia hati hizo za wito.

Mbunge Meryce na Maberana walifunga ndoa ya serikali hivi karibuni, jambo lililolalamikiwa na Buganga akidai kuwa mwanamke huyo ni mke wake, hatua iliyomfanya afungue kesi dhidi ya wanandoa hao.

2 comments:

Anonymous said...

Napenda kujua Hoyce Temu anaolewa na nani?, na kwanini wazuie kupigapicha?.

Anonymous said...

Yeah hata mimi ningependa kujua hoyce anaolewa na nani????